TIMUA VUMBI : Simba inaanza kujichimbia kaburi yenyewe Ligi Kuu

Thursday February 7 2019

 

By Mwanahiba Richard

HADI leo Alhamisi ukiachana na mechi itakayochezwa jioni dhidi ya Mwadui basi Simba ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara wamecheza mechi 14 wanashika nafasi ya nne wakiwa na pointi 33.
Yanga ambao jana Jumatano walicheza na Singida United wao wapo kileleni mwa msimamo wakiwa na pointi 54 wamecheza mechi 22.
Timu inayoshika mkia ni African Lyon imecheza mechi 24 na kukusanya pointi 19 pekee ambazo zinawaweka katika mazingira magumu ya kujinasua kushuka daraja.
Kuna tofauti kubwa ya mechi ambazo Simba wamecheza na zilizobaki ambazo ni viporo, ukilinganisha na waliopo kileleni basi ni mechi nane kuwafikia Yanga wakati Lyon ni mechi 10.
Simba hawajamaliza mechi za mzunguko wa kwanza wakati timu zingine zote zimeingia mzunguko wa pili wa ligi huku baadhi zitalazimika kucheza na Simba mechi zao za mzunguko wa kwanza, hivyo zitapiga mechi mbili za mizunguko miwili kwenye kipindi cha lala salama.
Simba inaeleweka kwamba wanashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi na tayari wamecheza mechi tatu na kukusanya pointi tatu pekee ambazo walizipata kwenye mechi ya kwanza iliyochezwa nyumbani dhidi ya JS Saoura ya Algeria.
Walisafiri kwenda DR Congo walipigwa bao 5-0 dhidi ya AS Vita na baadaye kufungwa bao kama hizo Misri walipocheza na Al Ahly. Simba itakuwa na wakati mgumu pale itakapoanza kucheza viporo vyao mfululizo ambavyo waliomba wenyewe kupangiwa tarehe nyingine kupisha maandalizi yao ya mechi za kimataifa ingawa wapinzani wao wote kwenye kundi lao wanaendelea na mechi za ligi zao huku wakicheza na Simba.
Bodi ya Ligi kupitia Mwenyekiti wao, Steven Mnguto aliweka wazi kwamba mabadiliko ya ratiba hasa mechi za Simba ni kutokana na viongozi wa klabu hiyo kuomba mechi hizo zisichezwe kwa wakati huo hata pale ambapo nafasi ya kucheza ilikuwepo.
Viongozi wa Simba ndiyo walikuwa wakiomba mechi zao zisichezwe kwasababu ya michuano ya kimataifa bila kuangalia athari za huko mbele na zaidi watawachosha wachezaji wao kucheza mfululizo.
Bodi ya Ligi ambayo pia ilikuwa inakubali maombi ya Simba yenyewe haitaathirika na athari zozote, ila wanapaswa kujua kwamba kuikubalia klabu moja tu kuomba kila wakati huo ni udhaifu mkubwa, yaani wameonyesha udhaifu wa wazi kwa Simba kwamba wanaweza kuamua lolote na likatekelezwa bila kupingwa.
Ligi ni moja, kanuni ni zile zile hata sheria zake, vipi pale ambapo timu nyingine ikaomba mechi zake kubadilishiwa tarehe Bodi watakubaliana na hilo? Maana tatizo hapo ni uzito wa sababu tu kupeleka maombi.
Bodi ya Ligi udhaifu huu unadhoofisha ligi, ratiba zipo wazi ambazo wanacheza mechi za kimataifa na ligi ya ndani, mambo mengine si ya kukubali tu kisa Simba ama timu yenye uwezo imepeleka maombi yake kuhusu kutochezwa mechi zake, hawa wengine watoto wa masikini mnawaweka kwenye wakati gani.
Sasa hivi zile timu ambazo zilipaswa kucheza na Simba mzunguko wa kwanza zitalazimika kujiandaa mara mbili kwa wakati mmoja, kama mechi zitachezwa Dar es Salaam na wakati huo pengine zitakuwa zimetoka jijini hapa hapa kucheza pengine na Yanga ama Azam hizo gharama za wakati mmoja nani atazisaidia.
Simba ifike mahala uoga uwekwe kando maana inaonekana kabisa hofu yao ndiyo iliyopelekea kuomba mechi zao zisogezwe mbele, kwenye vita hampaswi kuhofia kupigwa mnapaswa kuingia kupigana bila kujali itakuwaje.
Inasikitisha pia kama kikosi ni kipana inakuwaje kuwepo na hofu ya kucheza mechi za ligi na kukimbilia kuwekewa viporo.
Wachezaji wa Simba wajiandae kisaikolojia kucheza mfululizo, kuchoka na kupambana kupigania kombe kubaki Msimbazi, vinginevyo  hakutakuwa na maelewano mazuri.

Advertisement