Unahitajika utulivu mechi ya Simba na Al Ahly

Thursday January 31 2019

 

By Joseph Kanakamfumu

Simba tayari wameshaondoka kwenda Misri kwenye Jiji la Alexandria kucheza dhidi ya mabingwa wa kihistoria barani Afrika, Al Ahly kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Timu hizi zote ziko kundi D pamoja na timu za AS Vita na JS Saoura, huku Al Ahly wakiongoza kundi hilo wakifuatiwa na AS Vita , huku Simba na JS Saoura zikitofautiana kwa pointi moja hadi mbili tu.

Kwenye mchezo unaotarajiwa kupigwa Jumamosi usiku kwa saa za Afrika Mashariki, kumbukumbu yangu inanionyesha ni muda sasa Simba hawajacheza na Wamisri hawa, huku wapinzani wao Yanga wamekutana na Al Ahly mara mbili.

Mechi ya kwanza Yanga walitolewa kwa penalti baada ya kila timu kushinda bao moja nyumbani Yanga ikishinda Dar es Salaam kwa bao 1-0 , lililofungwa na nahodha wa kipindi hicho, Nadir Haroub Cannavaro, kisha Yanga kufungwa bao 1-0 ugenini.

Kwenye mechi ya pili, Yanga ilifungwa mabao 2-1 Misri kwenye baada ya awali kufungana bao 1-1 kwenye mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam .

Kwa vipindi vyote hivyo, Yanga ilionekana imara kuliko Wamisri, lakini kilichowasaidia Wamisri hao ni uzoefu tu.

Al Ahly hawakuwa imara sana hasa kutokana na Misri kukumbwa na machafuko yaliyosababisha Misri kutocheza ligi ya ndani ni kipindi kirefu, huku Yanga nayo ilikuwa kwenye wakati mzuri sana kiuchumi na hivyo ilipata utulivu mkubwa na maandalizi mazuri.

Kumbukumbu yangu inanikumbusha kuwa kipindi Simba wanafanya vizuri na kufanikiwa kuingia Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003, baada ya kuwatoa waliokuwa Mabingwa watetezi wa kombe hilo, Zamalek kwa mikwaju ya penati, kulikuwa na utulivu mkubwa sana kwa upande wa Simba kwenye mchezo wao huo wa mwisho.

Simba ilikuwa na utulivu ndani na nje ya uwanja huku ikipata sapoti ya nguvu kutoka shirikisho kwa kupata ratiba iliyowapa nafasi ya kukaa nje ya nchi kwa wiki mbili na zaidi wakijiandaa na mchezo huo.

Bado kikosi cha Simba kwa mchezaji mmoja mmoja kilikuwa kimeenea vizuri sana, wengi wakiwa na uzoefu wa michezo mikubwa Afrika na hata mwonekano na miili ya wachezaji wengi kipindi hicho ilikuwa bora zaidi.

Iliondoka nchini katika hali ya utulivu sana na kutoa matumaini makubwa ya kwenda kutoa upinzani wa dhati kwa Waarabu hao.

Huo ndio utulivu ninaosemea hasa ukilinganisha na jinsi Simba hii inavyoondoka kwenda kucheza na Al Ahly ambayo kimsingi imejiimarisha sana, Al Ahly hii ina hamu kubwa ya kuchukua kombe hili ililolizoea kulichukua likiwa pia na thamani kubwa.

Al Ahly hawajataka kulala mwaka huu, wamejiimarisha sana kwa kusajili wachezaji walio bora wa ndani ya nchi yao na wageni kutoka nje, wanakumbuka jinsi walivyolikosa msimu uliopita kwa kufungwa mabao 3-0 na Experance ya Tunisia.

Wanavyocheza nyumbani ni hatari zaidi kwa sababu wanaonekana kujiachia sana kimbinu huku pia wakilindwa zaidi na waamuzi ambao huwa upande wao kwa namna yoyote ile.

Hivyo utulivu na umakini kwa Simba unatakiwa wa hali ya juu. Ni timu yenye wachezaji wenye nguvu na kasi ndani ya uwanja, hii ndio silaha yao kubwa.

Ukiwaangalia Simba unaiona jinsi ilivyoondoka ikiwa haina utulivu ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo, hadi nje ya uwanja kwa mashabiki wake, Simba imeondoka ikiwa imetoka kushiriki michuano ya SportPesa, iliyotakiwa kuwaweka kwenye kiwango kizuri cha uchezaji, saikolojia na utulivu mkubwa.

Haijafanya vizuri kwenye michuano hii kinyume na inavyosemwa kuchukua ubingwa wa SportPesa haikuwa lengo lao.

Hata hivyo, matokeo hayo yatakuwa yameivuruga kiaina na mbaya zaidi ili kwenda hadi kwa wachezaji ambao walisakamwa sana kutokana na matokeo ya mechi ya nusu fainali dhidi ya Bandari ya Kenya.

Hakuna utulivu ule uliokuwapo mwanzo huku mabadiliko yakifanyika kwa kumwondoa meneja aliyekuwapo haya yote yanaondoa ule utulivu ninao usemea.

Ndipo hapa ninapowasihi Simba kuwa na utulivu mkubwa na umakini kwenye mchezo huu unaokuja hasa wakijiangalia jinsi walivyojiandaa jinsi walivyovurugana na mashabiki wao jinsi msemaji wao alivyowajia juu mashabiki wake kutokana na jinsi wanavyomchukulia tofauti.

Ni wazi Simba wanahitaji kucheza kwa uangalifu sana, Kocha Patrick Aussems hatakiwi kujificha kwenye kichaka cha timu kucheza vizuri tu, huku ikiwa haitoi matokeo mazuri ugenini.

Aussems lazima acheze kutokana na kuheshimu ubora wa wenzake Al Ahly na akubali tu kuwa wapinzani wake wako kwenye ubora mkubwa huku timu ikicheza soka la kushambulia zaidi.

Advertisement