NINAVYOJUA : Itachukua muda kupata wawakilishi bora wa nchi

Thursday February 7 2019Joseph Kanakamfumu

Joseph Kanakamfumu 

By Joseph Kanakamfumu

Unaweza kujiuliza ni lini Tanzania itapata timu ambayo itakwenda kutuwakilisha vyema kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, achilia mbali kufika fainali, bali kwenda kubeba ubingwa.

Wakati ukiendelea kujiuliza hivyo, wenzetu wanabadilika msimu hadi msimu na kuendeleza matumaini ya kufikia mafanikio makubwa Afrika.

Nadhani majibu yapo mbali sana, wakati bado tunaamini ligi yetu ni bora, huku ikiwa na klabu zinazolipa wachezaji pesa nyingi, hata hivyo hicho sio kigezo.

Swali hilo hapo juu linaweza kuwa linaulizwa sana kutoka vichwani mwetu hasa kutokana na jinsi wawakilishi wetu wanavyoendelea kuleta matokeo mabovu kuliko mategemeo yalivyokuwa mwanzo.

Ni kweli watu wengi tulikuwa na mategemeo makubwa Simba ambayo ndiyo timu pekee iliyoingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, tuliamini ni moja ya vikosi bora ambavyo Simba imewahi kuwa navyo huku tukiamini kwenye uwekezaji mkubwa kiasi uliofanywa na Mdhamini Mkuu wa klabu hiyo Mohamed Dewji utaleta tija kubwa na kutoa matokeo chanya kwenye michuano hii mikubwa.

Simba msimu huu baada ya kufanikiwa kuchukua ubingwa wa nchi iliendelea kujiimarisha sana kwa kuajiri kocha mwenye uelewa mkubwa wa soka, Patrick Aussems, kisha ikaongeza wachezaji bora wa ndani na nje ya nchi kina Meddie Kagere, Clotus Chama na Pascal Wawa.

Pia ilichukua vijana wa ndani ambao kwetu tunawaona ni bora kina Hassan Dilunga, Salamba na wengineo kisha ikajiandaa vizuri kwa kuweka kambi nje ya nchi huku ikicheza michezo mizuri ya kirafiki, hakuna shaka wengi tulitulia tukiamini mazuri yanakuja.

Pamoja na kuwa michuano hii Simba bado inaendelea na kimahesabu hakuna timu iliyojihakikishia kuingia hatua inayofuata na angalau timu zote bado zina nafasi ya kufanya vizuri, lakini matokeo haya ya awali waliyoyapata Simba yamerudisha nyuma mno mategemeo tuliyokuwa nayo wengi juu ya Simba kufanya vizuri,

Tumebaki tunajiuliza tunakwama wapi kuweza kufanya vizuri kwenye uwakilishi wa kimataifa kama inavyoelekea kwa Simba?

Najaribu kuingia kwenye mjadala wa kitaifa kuhusu sisi kutofanya vizuri na sijui kama kwa siku za karibuni tutafanikiwa kufanya vizuri.

Moja na ambayo ndiyo sababu kubwa ni nchi kuwa na ligi bora.

Kwangu ligi bora haiishi tu kwenye eneo la waamuzi bora, uendeshaji ulio bora, udhamini mzuri kwenye ligi na kadhalika.

Mimi naizungumzia ligi bora kwa upande wa mafanikio au matokeo chanya ya uchezaji ‘Performance’ ambayo inatakiwa kufikiwa na timu kadhaa kupitia kwa wachezaji wao.

Naizungumzia Performance ya juu inayotakiwa kufikiwa na klabu kiuchezaji ndani ya uwanja, hiki ndicho kitakacholeta ushindani mkubwa kwenye ligi yetu.

Mafanikio haya yanatokana na usawa wa ufundishaji, upatikanaji wa wachezaji walio bora wa ndani na wa nje ya nchi.

Hapa namaanisha ili Simba au Yanga bora iliyo na wachezaji bora wa ndani na nje ya nchi iwe kimatokeo inatakiwa kukutana na Ndanda, Kagera Sugar, Lipuli na nyinginezo zenye wachezaji bora wa ndani na hata nje hata kwa asilimia fulani kwa kuwa si rahisi kila timu kusajili wachezaji wa aina moja lakini angalau wawe na ubora kiasi, bila shaka kwa utaratibu huu tunaweza kuzitengeneza timu wawakilishi kwenye ubora fulani.

Hii inaonyesha ni jinsi gani timu zenye wachezaji tunaowaona bora mfano Simba, msimu huu kutopata ushindani mkubwa ndani ya ligi yetu kitu ambacho kingeweza kuwanoa wachezaji wa Simba kwa kuwaongezea ubora miguuni mwao lakini kwa jinsi ilivyo ni kazi sana kwa mchezaji bora kuupata ubora zaidi anapocheza ndani ya ligi yetu.

Pia kutengeneza Performance hakutengenezwi na klabu pekee kupitia kwa benchi za ufundi.

Pia ratiba yetu inawafanya wachezaji wasiweze kufikia utimamu wa mafanikio ya utendaji wa kazi ndani ya uwanja, ratiba ya michezo mingi ndani ya ligi yetu ukilinganisha na miundo mbinu ya nchi yetu na hasa uwezo wa klabu zetu.

Hata hivyo, pia kusajili wachezaji waliomaliza mikataba yao huku klabu zao zikishindwa kuendelea nao. Wengi wa wachezaji wetu ni wale wenye viwango vya kawaida, ndiyo maana nasema itatuchukua muda mrefu kuja kupata wachezaji bora watakaoweza kutuwakilisha na kufanya vizuri kwenye michuano hii mikubwa barani Afrika.

Advertisement