MTAA WA KATI : Mwacheni Sarri atuletee Kante mwingine tusiyemjua

Muktasari:

  • Sarri mwenyewe alikaa kimya. Alipotoa kauli, basi ilikuwa na utata Chelsea ndio wataamua kumfuta kazi kama wakiona hafai.
  • Jambo hilo lilikuja baada ya Chelsea kufungwa na Wolves katikati ya juma lililopita.

MAURIZIO Sarri anajibu kwa vitendo. Kabla ya Jumamosi, madai yaliyotawala anamharibu Kante. Kwa nini amchezesha kwenye kiungo ya kushambulia, wakati anafanya vizuri zaidi kwenye kiungo ya kukaba.

Hayo yalikuwa maoni ya watazama mpira tu. Lakini, hatakuwa akizingatia mfumo wa kocha huyo.

Sarri mwenyewe alikaa kimya. Alipotoa kauli, basi ilikuwa na utata Chelsea ndio wataamua kumfuta kazi kama wakiona hafai.

Jambo hilo lilikuja baada ya Chelsea kufungwa na Wolves katikati ya juma lililopita.

Wengi waliamini asingefanya kitu mbele ya Man City ya Guardiola. Ndio mchezo uliokuwa ukifuatia.

Lakini, Sarri mpango wake ulikuwa palepale, Kante kucheza kwenye kiungo ya kushambulia.

Hakubadilishwa na maoni ya watu. Alimwacha Jorginho kwenye eneo la kukaba. Mwenyewe ameweka wazi akisema Kante ni mchezaji mahiri, mwenye uwezo wa kukaba na kupora mipira, lakini linapokuja suala la kucheza kwa maelekezo, Kante hana huo ujuzi ukilingana na ule wa Jorginho.

Kwa maana fupi, Jorginho anakupa kile unachokitaka. Kwenye mechi dhidi ya Man City lilionekana hilo.

Kante alifanya kazi yake na kitu cha ziada alifunga pia bao. Kumbuka wakati Sarri anatua Stamford Bridge kitu kimoja kikubwa alichokuwa akikitaka kutoka kwa Kante kuwa kiungo anayefunga mabao pia.

Kante alifanya kila kitu, lakini hakuwa akifunga mabao. Alibeba ubingwa Leicester City na Chelsea, lakini ukihesababu mabao yake hayakuwa yakizidi matatu.

Sasa Sarri anataka kumfanya kuwa kiungo aliyetimia kila idara. Anakaba na anafunga. Pia Sarri anamtumia Kante kwenye kiungo ya kushambulia akiwa na madhumuni ya kuanza kumnyang’anya mpinzani mpira akiwa bado kwenye nusu yake.

Jambo hilo limewasaidia Chelsea na ndio maana Ligi Kuu England msimu huu, wanashika namba tatu kwa kufungwa mabao machache licha ya Jorginho ndiye kiungo wao mkabaji na si mzuri kwenye jambo hilo.

Chelsea wamefungwa mabao 13 na wanazidiwa na Liverpool waliofungwa mabao tisa na Man City mabao tisa. Ni wazi, Sarri atakuwa amewajibu waliokuwa wakihoji uwezo kwa vitendo. Kumdhibiti Guardiola na Man City yake.

Tena kwa kumfunga mara mbili bila ya kuruhusu bao, hilo halikuwa jambo rahisi. Lakini, hilo lilitokana na ufundi wake, ikiwamo wa kumtumia Eden Hazard kama mshambuliaji wa kati bandia.

Hivi ndivyo Sarri alivyoonyesha yeye si mtu wa kukariri. Anafanya kitu kulingana na mipango yake anavyotaka iwe kwa siku husika na kwa wakati mwafaka.

Kitu kingine hakuna mahali ambako Kante amelalamika kucheza kwenye nafasi anayocheza kwa sasa. Zaidi ya hilo ni kufurahia tu kuona jina lake linakuwa kwenye orodha ya wafungaji na kuisaidia timu yake.

Tumwaache Sarri atuletee Kante mwingine, yule anayekaba na kupora mipira tushamfahamu tayari.

Kwani kuna asiyefahamu umahiri wa Kante upo kwenye nini? Hakuna asiyejua. Kwenye nafasi anayocheza hatamfanyi ashindwe kutimiza majukumu yake ndani ya uwanja na kilichobadilika ni eneo lake tu la utendaji kazi.

Kocha Sarri mfumo wake anataka mashambulizi yanatengenezwa kwenye sehemu ya kiungo na hapo anamwona Sarri, ambaye kimsingi sio kiungo wa kubaka bali ni kiungo mwenye uwezo wa kukaa na mipira na kuamrisha mechi ichezwe anavyotaka yeye.

Jorginho ni aina ya viungo kama alivyokuwa Michael Carrick wa Man United. Anachezeshwa mbele ya mabeki wa kati, lakini wala hajui kukaba.

Ukabaji wake yeye ulikuwa kuufanya mpira ulipofika kwake, basi uwe umetulia na kupelekwa pale panapohitajika tu.

Ndio maana ilikuwa ngumu kumwona kiungo Carrick akichafuka uwanjani kwa sababu ya kukaba au kuonyeshwa kadi za njano hovyo hovyo.

Yeye alichokuwa akifanya ni kuukaba tu mpira na si kumkaba mtu. Huo ndio ulikuwa umuhimu wake na hakika Man United ilikuwa ikipwaya pale ilipokosa huduma yake. Kwenye kikosi cha Barcelona kuna mtu wa aina hiyo. Sergio Busquets. Kimsingi, Busquets si kiungo wa kukaba, kwa sababu hiyo kazi haifahamu vyema.

Mhispaniola huyo hakukabi, anachofanya ni kuukaba mpira kwenye njia zake na kisha unapokuwa kwenye himaya yake anahakikisha unakwenda kwa mtu mwafaka na kwa wakati sahihi.

Hilo ndilo analolifanya Jorginho huko kwenye kikosi cha Sarri. Sarri anafahamu umuhimu wa Kante, lakini kimsingi kwenye mfumo wake hataki tu mchezaji ambaye atakuwa amejitengenezea majukumu ya aina moja tu, kunyang’anya mipira na kuwapa wenzake waucheze.

Sarri amembadilisha Kante na kumpa majukumu mengine, pengine hayo yanamfanya apevuke zaidi na kuwa mchezaji tofauti. Hilo ndilo tunalohitaji kuliona kutoka kwa Kante. Lucas Torreira ni kiungo mkabaji, lakini ameonyesha kwamba amekuwa na uwezo tofauti kwenye kufunga.

Hivyo ndivyo anavyopaswa kuwa mchezaji wa kisasa kwa sababu mfumo unaotamba kwenye soka katika kizazi hiki, kukaba ni kazi ya kila mchezaji na si ya mtu mmoja tu. Zile zama za kina Claude Makelele, Patrick Vieira, Roy Keane, Gennaro Gattuso zimeshakwisha na ndio Man City wanamtumia Fernandinho kwenye kiungo ya kukaba wakati si mahiri sana kwenye suala hilo.

Anachokifanya Fernandinho ni kuhakikisha tu mpira unakuwa salama unapokuwa kwenye miguu yake huo ndio ukabaji wa kisasa kumdhibiti mpinzani.