MTU WA PWANI : Tshabalala usiziache fedha hizi nje ya soka

Friday February 14 2020

 Tshabalala usiziache fedha hizi nje ya soka, Simba na Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mohamed Hussein ,mitandao ya kijamii,

 

By Charles Abel

BEKI wa kushoto wa Simba na Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ana jumla ya wafuasi 514,933 katika kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya Nairobi Sports Digital, idadi kubwa ya wafuasi wa Tshabalala wapo katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram ambao ni 427,000.

Ana wafuasi 81,705 katika Facebook wakati katika Twitter, ana wafuasi 6,228. Anashika nafasi ya tatu katika orodha ya wachezaji wa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati wanaoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wafuasi katika mitandao hiyo mitatu ya kijamii nyuma ya wakali wawili wa Tanzania na Kenya wanaokipiga katika Ligi Kuu ya England, Mbwana Samatta na Victor Wanyama.

Samatta ambaye anachezea Aston Villa ndiye anayeongoza akiwa na zaidi ya wafuasi milioni 1.6 na nafasi ya pili inashikwa na nahodha wa Timu ya Taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’, Wanyama anayeitumikia Tottenham Hotspurs ambaye ana wafuasi 933,908. Hii inamaanisha kwa wachezaji wa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati wanaocheza ndani ya Bara la Afrika, Tshabalala ndiye kinara kwa kuwa na idadi kubwa ya wafuasi katika mitandao ya kijamii kuliko mwingine yoyote.

Lakini pia ndiye mchezaji wa Kitanzania anayeshika nafasi ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya wafuasi katika mitandao ya kijamii nyuma ya Samatta lakini ukimuweka katika kundi la wale wanaocheza hapa nyumbani, yeye ndiye kinara kwa kuwa na idadi kubwa ya wafuasi katika kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Idadi hiyo kubwa ya wafuasi wa Tshabalala katika mitandao ya kijamii inapaswa kuwa fursa muhimu kwa nyota huyo kuvuna fedha kutokana na udhamini binafsi wa kampuni na taasisi mbalimbali.

Advertisement

Anapaswa kutumia namba hiyo kama mtaji wa ushawishi kibiashara kupitia matangazo ya bidhaa na huduma zao ambayo yatafanyika katika kurasa zake hizo ili aingize fedha katika akaunti zake za benki badala ya kutegemea posho na mishahara anayolipwa na Simba.

Tshabalala anaweza kuwatafuta wataalamu wabobezi wa masuala ya masoko na biashara na kuwapa jukumu la kumtafutia tenda za matangazo kisha akawalipa sehemu ya fedha atakazolipwa kupitia mikataba atakayosaini na kampuni au taasisi zitakazovutika kufanya naye kazi.

Ni akili ya kawaida ambayo itawafanya wale aliowapa jukumu hilo kuumiza vichwa na kutafuta ofa nyingi na nono za matangazo kwa vile ndizo zitakazowafanya nao wapate kitita kikubwa cha fedha kwani kinyume na hapo nao hawatanufaika.

Ni jambo ambalo linawezekana kufanyika na likaleta mafanikio kwake kwani hivi sasa dunia imehamia mitandaoni ambako kumekuwa kukilengwa zaidi na kampuni mbalimbali kwa sababu zinaamini zitafikia idadi kubwa ya wateja kirahisi.

Lakini pia zinaona matumizi ya mitandao ya kijamii katika kutangaza bidhaa hayana gharama kubwa kulinganisha na zile ambazo zinaweza kulipa katika njia nyingine kama vile vyombo vya habari au mabango yanayowekwa barabarani.

Kwa bahati nzuri mchezo wa soka ndio ambao umekuwa ukiongozwa kwa kupendwa na kufuatiliwa na idadi kubwa ya watu sio tu hapa nchini bali Afrika nzima na duniani kwa ujumla.

Ni jambo lililo wazi kwamba kutokana na mchezo huo na wanasoka kufuatiliwa kwa ukaribu, kampuni, taasisi na idadi kubwa ya wafanyabiashara wamekuwa wakipenda na kutamani kutangaza bidhaa na huduma zao tofauti na michezo mingine hasa kwa hapa nchini.

Inawezekana ikawa ni vigumu kwao kudhamini igi zetu kutokana na pengine kuhitajika kutoa fungu kubwa la fedha lakini inaweza kuwa rahisi kwao kuja kivingine kwa kutangaza kupitia wachezaji ambao wanafuatiliwa kwa ukaribu katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Tshabalala anapaswa kulitafakari hili na kuamua kulifanyia haraka ili asiendelee kuzikosa fedha ambazo alipaswa awe anazivuna hivi sasa kutokana na mtaji wa wafuasi alionao katika mitandao ya kijamii.

Katika umri wa miaka 25 alionao, akumbuke safari yake ya kimpira ni fupi ambayo imebakiza miaka isiyozidi sita ya kucheza kwa ubora wa juu na badala ya hapo atalazimika kuzipisha damu changa zitakazokuwa zinaibuka.

Angeweza kuvuna mamilioni ya fedha ikiwa angepata fursa ya kucheza soka la kulipwa kwa kiwango cha juu nje ya Tanzania lakini ameshachelewa na umri wake haumpi mwanya wa kufanya hivyo kwa sasa wala baadaye.

Advertisement