MTU WA PWANI : Sio dhambi kujadili kipato cha Samatta na Diamond

Friday January 24 2020

 Sio dhambi kujadili kipato cha Samatta na Diamond-Ligi Kuu ya England- klabu ya Aston Villa-KRC Genk-

 

By Charles Abel

KUNA mijadala mingi imeibuka mara baada ya mshambuliaji na nahodha wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta kujiunga na klabu ya Aston Villa inayoshiriki Ligi Kuu ya England.

Ile ambayo inaonekana kushika chati ni inayohusu upande wa maslahi ambayo mchezaji huyo atayapata mara baada ya kuhama katika timu ya KRC Genk na kutua nchini England ambako anaenda kutimiza rasmi ndoto yake ya muda mrefu kucheza katika ligi yao.

Kuna ambao wanajadili kiwango cha fedha ambacho Samatta atalipwa cha Pauni 50,000 (Shilingi 151 milioni) ambacho atakuwa anapokea kila wiki kikiwa ni mshahara wake ndani ya klabu hiyo.

Wanaona kwa maisha ya Kitanzania ni kiasi kikubwa cha fedha ambacho kwa muda wa miaka minne na nusu ya mkataba wake na Villa, kitamfanya mchezaji huyo kuwa bilionea mkubwa nchini na pengine akawa ndiye mwanamichezo tajiri kuliko wote hapa Tanzania.

Na hili ni jambo ambalo liko wazi na kwa sasa halina kipingamizi kwa sababu malipo kwa wanamichezo wetu kama vile wanasoka yamekuwa ni kiduchu.

Ukiondoa wale wanaojadili kiwango cha mshahara wa Samatta, kuna ambao wamekuwa wakibishana juu ya nani zaidi kwa nguvu ya kiuchumi baina ya mwanasoka huyo na mwanamuziki anayefanya vizuri hapa nchini na Afrika kwa ujumla, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’.

Advertisement

Kuna wanaoamini kuwa shughuli za kimuziki zimemfanya Diamond kumiliki kiasi kikubwa cha fedha kuliko mwanasoka huyo lakini pia kuna ambao wanadhani kuwa Samatta ana fedha nyingi kuliko mwanamuziki huyo ambaye ni kiongozi wa lebo maarufu ya WCB hapa nchini.

Kwa bahati mbaya wale ambao wanasimamia upande wa Diamond wamekuwa hawana ushahidi unaojitosheleza kwa sababu hakuna data zinazoonyesha kiwango cha fedha ambacho mwanamuziki huyo anapata kwa, wiki, mwezi, mwaka au katika kila shoo ya muziki ambayo anafanya iwe ndani au nje ya nchi.

Lakini wakati mijadala hiyo ikizidi kupamba moto, kuna ambao wamekuwa wakiitafsiri tofauti na kuona kuwa wale ambao wanajadiliana kuhusu fedha na utajiri wa Samatta na Diamond wanafanya makosa kwa kufuatilia vipato visivyowahusu.

Kwa mtazamo wao wanaamini kuwa jamii haifanyi kitu sahihi kuendeleza mijadala kuhusu mastaa hao wawili nchini kwa sababu walipambana wenyewe hadi kufika hapo walipo na hakuna mantiki ya kujua nini wanachoingiza kupitia shughuli zao.

Hata hivyo kiuhalisia, uwepo wa mijadala ya namna hiyo una faida na umuhimu mkubwa katika maendeleo ya sekta ya michezo na nyinginezo nchini kuliko hasara kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakitafsiri.

Mojawapo ya faida hizo ni kuwapa hamasa watu wa kada mbalimbali kuwa katika juhudi na utayari, wana nafasi ya kufanya vizuri na kupiga hatua zaidi katika shughuli wazifanyazo za kutafuta mkate wao wa kila siku.

Hapana shaka kwamba kwa kiasi kikubwa, mafanikio ya Samatta na hata ya Diamond yametokana na juhudi zao binafsi ingawa wapo watu ambao kwa namna moja au nyingine waliwapa sapoti.

Wote wawili wametokea katika familia za watu wa hali ya chini hivyo ni wazi kwamba mijadala ya sasa inaweza kuwafanya watoto na vijana waliopo katika familia za hali ya kawaida na zenye vipato vya wastani au vidogo kiuchumi, wataanza kuamini kuwa wakipambana wanaweza kubadilisha hali zao za kimaisha miaka ya usoni.

Lakini faida nyingine ya mijadala ya namna hiyo ni kujenga taswira nzuri ya shughuli ambazo Samatta na Diamond kwa jamii ya Kitanzania.

Kwa muda mrefu, muziki na michezo hasa mpira wa miguu zimekuwa hazionekani kama ni sekta zenye maana na faida kubwa kiuchumi na badala yake zimekuwa zikionekana kama shughuli za watu waliokosa dira kimaisha.

Ni wazi kwamba sasa nchi inaona inaweza kuona faida ya uwekezaji katika maeneo hayo mawili ili tupate kundi kubwa la wanasoka na wanamuziki ambao watakuja kuwa chanzo cha mapato ya serikali kupitia kodi na uwekezaji ambao wataufanya hapa nchini.

Kwa sasa, michezo na burudani havitazamwi kama sekta zinazoweza kubadilisha uchumi wa nchi na ndio maana hata bajeti ambayo imekuwa ikipangwa kwa ajili ya wizara husika huwa ni kiduchu na haionekani kama inakidhi mahitaji ya wizara hiyo.

Pia inaweza kuwafanya wazazi wakabadili mitazamo na kuanza kuwekeza katika vipaji vya watoto wao ili waweze kunufaika navyo siku za usoni badala ya kuamini kwamba uwekezaji kwa watoto unafanyika katika elimu tu.

Uthubutu wa Samatta na Diamond, umewafanya wafanikiwe kuziishi ndoto zao, unapaswa kutumika kama darasa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.


Advertisement