MTU WA PWANI : Azam Sports imefichua tunachokikwepa kule FDL

Muktasari:

Sahare All Stars inaweza kuwa ndio timu iliyoshangaza zaidi katika mashindano hayo kwa kutinga hatua ya robo fainali kwani ndio pekee kutoka Ligi Daraja la Kwanza iliyoweza kutinga katika hatua hiyo.

HATUA ya 16 Bora ya Mashindano ya Kombe la Azam Sports Federation, imemalizika Jumatano wiki hii ambapo timu nane (8) zimetinga hatua ya robo fainali.

Timu hizo ni mabingwa watetezi Azam, Simba, Yanga, Alliance, Kagera Sugar, Namungo, Ndanda na Sahare All Stars.

Haikuwa kazi rahisi kwa timu hizo kupenya na kuingia katika hatua hiyo ya robo fainali kwani zilikutana na ushindani wa hali ya juu katika hatua iliyomalizika.

Ushahidi wa hilo ni matokeo ambayo timu hizo ziliyapata kwani kati ya mechi nane zilizochezwa, ni mbili tu ambazo zilimalizika katika muda wa kawaida na mechi sita zililazimika kusubiria mikwaju ya penalti ili kumpata ushindi.

Sahare All Stars inaweza kuwa ndio timu iliyoshangaza zaidi katika mashindano hayo kwa kutinga hatua ya robo fainali kwani ndio pekee kutoka Ligi Daraja la Kwanza iliyoweza kutinga katika hatua hiyo.

Jambo la kuvutia na kushangaza zaidi, Sahare wameingia katika hatua hiyo baada ya kuichapa Panama kwa mabao 5-2, ambao ndio ushindi mnono zaidi katika hatua ya 16 Bora tofauti na mechi nyingine saba ambazo hazikuzalisha idadi kubwa ya mabao.

Kabla ya kutinga hatua ya 16 Bora, waliitoa Mtibwa Sugar ugenini kwa mikwaju ya penalti na jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba katika mechi zao zote wamekuwa wakionyesha kiwango bora na cha kuvutia ndani ya uwanja.

Katika hali ya kushangaza, hawa Sahare All Stars wamekuwa hawafanyi vizuri katika Ligi Daraja la Kwanza na ni miongoni mwa timu ambazo zimekuwa zikipigania kusalia katika ligi hiyo.

Pamoja na kiwango bora ambacho wamekuwa wakikionyesha, juhudi zao zimekuwa zikikwama kwa kile kinachotajwa kukosa mipango ya nje ya uwanja na fedha tofauti na timu baadhi ya timu zinazofanya vizuri.

Fitna hizi zinazotajwa ni uhongaji wa waamuzi na makamishna wa mechi ili timu ipate upendeleo, kuwahonga wachezaji wa timu pinzani lakini pia masuala ya ushirikina.

Kutokana na hilo wanajikuta wakipata wakati mgumu katika mechi zao dhidi ya timu ambazo zimekuwa zikijihusisha na vitendo hivyo hivyo juhudi zao zinakuwa kama kilio cha samaki ambacho machozi huenda na maji.

Kwa bahati mbaya Ligi Daraja la Kwanza, haionyeshwi katika luninga hivyo inakuwa ni jambo gumu kwa jamii na mamlaka za soka kupata nafasi ya kuona hujuma na udhalimu ambao umekuwa ukifanywa na timu ambazo zimekuwa zikitumia nguvu ya fedha, fitna na wanasiasa ili zitimize lengo la kupanda Ligi Kuu.

Matokeo yake timu kama Sahare zinajikuta zikiumizwa na uamuzi mbovu wa waamuzi ambao wamekuwa wakizibeba waziwazi baadhi ya timu na malalamiko yao yanakuwa kazi bure.

Ni jambo ambalo limekuwa likipigiwa kelele kila uchao na kila wakati kumekuwa na vilio kutoka kwa timu, mashabiki na wadau wa soka lakini mwisho wa siku mamlaka husika zinaonekana ziko kimya kuchukua hatua ya kukomesha changamoto hizo.

Kwa vile baadhi ya marefa na makamishna wamekuwa wakihusika katika ukandamizaji wa timu, inakuwa ni vigumu kupatikana ushahidi wa kushughulikia matatizo yanayopelekea timu kama Sahare kushindwa kuchomoza na kupanda Ligi Kuu.

Hatupaswi kushangaa na kujiuliza kwa nini timu nyingi zinazotamba katika Ligi Daraja la Kwanza zimeondolewa mapema katika Kombe la Azam Sports Federation halafu zile zinazofanya vibaya zikifika mbali na kutamba.

Ni vigumu kwa waamuzi kuchezesha vibaya ili kuzibeba timu fulani kwa sababu mashindano ya Azam Sports Federation yanaonyeshwa katika luninga na uovu wao utaonekana hadharani.

Ni kama ilivyo katika Ligi Kuu ambapo kwa sasa inakuwa ni rahisi kuwahukumu waamuzi na makamishna kwa sababu kila yanayofanyika yanaonekana.

Kufuzu kwa Sahare All Stars na kiwango bora kilichoonyeshwa na Stand United na Ihefu FC dhidi ya vigogo vya soka nchini Simba na Azam FC hadi kufikia kutolewa kwa mikwaju ya penalti ni jambo ambalo halijatokea kwa bahati mbaya.

Ni ushahidi tosha kuwa kuna matatizo mengi katika Ligi Daraja la Kwanza ambayo yanakwamisha timu bora kufanikiwa na kujikuta zikiwa wasindikizaji.

Wengi wetu tunayafahamu lakini tunajikausha bila kuyashughulikia huku tukijifanya kushangazwa na ushindani wa kina Stand United, Ihefu na Sahare All Stars.