MTAA WA KATI : Ukweli mchungu wababe Arsenal, Man United

Tuesday December 17 2019

Ukweli mchungu -wababe Arsenal- Man United-Man City - Liverpool-Spurs - Man City-Man United-

 

By Said Pendeza

WAKATI mwingine unahitaji kukubaliana na ukweli hata kama unaumiza, kwa sababu hivyo ndivyo ukweli ulivyo.

Ukweli ni kwamba mashabiki wa Manchester United na Arsenal ifike mwisho kujigamba na kuziweka timu zao kwenye orodha ya timu vigogo kwa sasa. Timu hizo zimebaki majina tu kwa sasa.

Tazama Man United inavyocheza kwa sasa. Wamejiondoa kwenye kundi la timu kubwa bila ya kujitambua. Ona wanapocheza dhidi ya Man City, Chelsea, Liverpool, Tottenham na timu nyingine zinazofahamika kuwa ni kubwa, inagangamala na kucheza kwa kiwango kikubwa sana. Man United inayocheza na Man City au Liverpool unaweza kuthubutu kuitabiria ubingwa. Lakini, sasa isubiri kwenye mchezo dhidi ya Aston Villa au Everton. Utashangaa ni kuwasahau kama ni walewale Man United waliocheza na Spurs na Man City.

Hilo linaonyesha kwamba wanapocheza mechi kubwa wanacheza kwa kupania. Wanataka kuwadanganya watu kwamba nao bado wamo kwenye kundi la wababe. Lakini, kupania au kukamia kitu ni kawaida ya timu ndogo inapocheza dhidi ya timu kubwa. Man United ya sasa imejiweka kwenye kundi hilo. Mashabiki wa Man United wakubaliane na ukweli huo.

Watazame Arsenal. Namna walivyofungwa kwenye mchezo wao dhidi ya Man City wameonyesha kwamba wamerudi nyuma kilomita nyingi sana kutoka kule walikokuwa na wanakotaka kwenda. Ukweli ni kwamba timu hizo mbili zinahitaji muda mrefu kwelikweli kurudi kwenye ubora wao. Sambamba na hilo wanahitaji uwekezaji mkubwa pia kuwa timu za kiushindani muda wote, wiki kwa wiki. Hiyo ina maana zinahitaji kufanya matumizi makubwa ya pesa. Lakini, si matumizi tu, bali matumizi sahihi. Arsenal na Man United zinahitaji kufanya matumizi ya pesa mfululizo kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu kurudi kwenye ubora wao. Hakuna ubishi ndizo timu zilizojikusanyia mashabiki wengi ndani ya miaka ya karibuni, hivyo kuboronga kwao kumekuwa kukiwagusa watu wengi.

Ndani ya miaka michache iliyopita, timu hizo zimeonekana kuwa na tatizo kwenye aina ya usajili wake. Aina ya wachezaji ambao imekuwa ikiwachukua. Zinatumia pesa nyingi, lakini hazisajili wachezaji sahihi.

Advertisement

Watazame Arsenal wanao Pierre-Emerick Aubameyang na Alexandre Lacazette kwenye fowadi yao. Walikuwa pia na Henrikh Mkhitaryan na wanaye Ozil. Nini kilichowafanya watumie Pauni 72 milioni kumsajili Nicolas Pepe?

Kulikuwa na ulazima huo wakati timu tatizo lake kubwa lilionekana kuwa ni beki na mbaya zaidi Laurent Koscielny naye aliondoka? Pauni 72 milioni hizo ingekuwaje zingetumika kwenye usajili wa beki wa kati? Matumizi mabaya ya pesa. Sasa watahitaji kuendelea kutumia pesa kufanya usajili ambao pengine isingekuwa hivyo kama wangefanya mambo yao kwa akili huko nyuma.

Kwa sasa, timu hizi hazistahili tena ya kuitwa timu kubwa. Huo ndo ukweli.

Advertisement