MTAA WA KATI : Pep Guardiola bahati nayo imemtupa mkono

Muktasari:

Man City iliingia msimu huu ikiwa na kazi mbili. Kwanza kutetea ubingwa, lakini pili ni kulifukuzia taji hilo ilibebe kwa mara ya tatu mfululizo kufikia rekodi iliyowahi kuwekwa na Sir Alex Ferguson kubeba ubingwa mara wa ligi mara tatu mfululizo akiwa na Man United.

SIO safari hii. Pep Guardiola hana ujanja tena wa kumzuia Jurgen Klopp asifanye yake kama alivyofanya msimu uliopita.

Wakati Liverpool ilipoonekana inakwenda kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu England msimu uliopita, Guardiola na Manchester City yake wakacharuka, wakamweka chini Klopp wakabeba ubingwa kibabe.

Lakini, msimu huu bahati mbaya zimeamkia huko Man City. Wanafungwa kwenye mechi ambazo kimsingi walipaswa kushinda.

Juzi Jumapili, dhidi ya Tottenham mechi iliyoishia Man City kuchapwa 2-0, wenyewe ndio waliopiga mashuti mengi, waliotengeneza nafasi nyingi, waliomiliki mpira kwa muda mwingi na wamepiga kona nyingi. Lakini, filimbi ya mwisho ilipopulizwa, Guardiola alikumbana na kipigo cha sita msimu huu na kuonekana kama ni kawaida yake kuchapwa.

Man City iliingia msimu huu ikiwa na kazi mbili. Kwanza kutetea ubingwa, lakini pili ni kulifukuzia taji hilo ilibebe kwa mara ya tatu mfululizo kufikia rekodi iliyowahi kuwekwa na Sir Alex Ferguson kubeba ubingwa mara wa ligi mara tatu mfululizo akiwa na Man United.

Lakini, Man City ya msimu huu imekuwa na beki dhaifu haijawahi kutokea. Vichapo vimeifanya kuachwa pointi 22 na Liverpool na stori za sasa huko kijiweni si ushindani tena kwenye mbio za ubingwa, bali ni lini Klopp atabeba taji lake la kwanza la Ligi Kuu England.

Kitu kibaya kitakachomuuma zaidi Guardiola, timu yake inaweza kuwa ndio itakayokuwa ikiwapongeza Liverpool kwa kuchukua ubingwa kwa maana ya kujipanga mistari miwili mabingwa wapya wapite wakati watakapokutana nao Etihad wikiendi ya kwanza ya Aprili.

Bila ya shaka hilo litamuumiza sana Guardiola. Na sasa mjadala umerudi upya, kwamba atabaki Etihad au ataondoka? Kama atabaki, basi hakuna ubishi, atafanya usajili wa fujo kwenye dirisha lijalo kuziba mapengo yote yaliyoonekana kuwa na shida msimu huu.

Man City haina zali msimu huu. Mchezo wa juzi huwezi kumwaga sifa kwa Jose Mourinho kwamba amefanya maajabu kushinda. Man City ilikosa bahati. Imepoteza nafasi nyingi na imekosa penalti pia. Unaweza kuona jinsi mambo yanavyokuwa magumu kwa Guardiola.

Ushindi umempa nguvu Mourinho, ambapo Spurs yake sasa imepanda hadi kwenye nafasi ya tano, pointi nne tu nyuma ya kuifikia nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya. Sasa Mourinho anawasaka wajiri wake wa zamani, Chelsea ili kuwaengua kwenye nafasi hiyo ya nne.

Hayo yanatokeo huko kwa makocha wengine, lakini kwa Guardiola amekuwa na bahati mbaya. Alihitaji kusajili beki mwingine kwenye majira ya baridi baada ya kushindwa kufanya hivyo kwenye majira yake ya kiangazi.

Jambo hilo linamgharimu sasa na watu wanajipigia tu kikosi chake. Kwa msimu huu timu pekee ambayo ingeweza kuichelewesha Liverpool kwenye mbio za ubingwa ni Man City, lakini sasa wakali hao wanaweza kutangaza ubingwa mapema zaidi na kuvunja rekodi ya Man United, ambapo walitangaza ubingwa Aprili 14, 2001.

Hakuna namna kitu pekee kwa Guardiola kwa sasa ni kukubali tu, hakuna ubingwa na pengine kitu cha kufanya ni kulinda nafasi ya tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya. Wiki chache zilizopita, mwenyewe alikiri kwamba kwa Liverpool hii hata ingecheza kwenye ligi nyingine za La Liga, Serie A, Bundesliga bado ingechukua ubingwa.

Kwenye ligi hizo hakuna timu iliyocheza mechi 25 na kushinda 24, huku ikiwa haijapoteza mechi.

Liverpool imekifanya hicho kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Sasa inasubiri siku tu ya kujibebea taji lake la kwanza ililolisubiri kwa karibu miaka 30.