MTAA WA KATI : Bahati tu inamuweka Sarri Stamford Bridge

Muktasari:

  • Chelsea ilicheza hovyo na hakika Abramovich angekuwapo England na kwenda kutazama mechi hiyo, asingeweza kuvumilia. Makocha waliomtangulia waliponzwa na hilo.

MAISHA ya Stamford Bridge yamebadilika sana. Maurizio Sarri bado yupo Stamford Bridge hadi sasa akivuta tu sigara zake.

Mwaka mmoja nyuma hilo lisingekuwa rahisi kutokea. Unajua kwanini Chelsea haifanyi vizuri ndani ya uwanja na hicho si kitu alichokuwa akiweza kukivumilia Bilionea Roman Abramovich.

Sarri amekuja kwenye kipindi kizuri sana Stamford Bridge. Sasa hivi imekuwa nadra kumwona Abramovich uwanjani Chelsea inapocheza. Kukosa kibali cha kuingia Uingereza kumenusuru ajira ya Sarri na kuendelea tu kupuliza sigara zake kwenye kolido za Stamford Bridge wakati huko uwanjani timu haifanyi vizuri.

Juzi Jumapili, The Blues ilipata ushindi wa shida sana mbele ya wachovu Cardiff City.

Tena imeshinda kwa bao la mbeleko, dhahiri kabisa wachezaji wa Chelsea walikuwa wameonea wakati wanafunga bao lao la kwanza lililokuwa la kusawazisha.

Chelsea ilicheza hovyo na hakika Abramovich angekuwapo England na kwenda kutazama mechi hiyo, asingeweza kuvumilia. Makocha waliomtangulia waliponzwa na hilo.

Abramovich alikuwa hakauki viwanjani na ilikuwa shida kwao timu inapocheza hovyo.

Kwa sasa anafanya kazi kwa mbali, kuitazama timu kwenye televisheni si sawa na kwenda uwanjani. Hilo limekuwa jambo zuri kwa Sarri na walau pengine ataendelea kukusanya mishahara yake ya wiki wiki hadi mwisho wa msimu.

Kinachotajwa kwa sasa ni kwamba huenda mwisho wa msimu akabadilishwa. Lakini, kama Abramovich angekuwa ndani ya Uingereza, sidhani kama Sarri angeendelea kukalia kiti cha Stamford Bridge hadi sasa.

Hilo la Abramovich kuwa mbali na timu yake linaleta mambo mengi kwenye mjadala. Eden Hazard sasa anashawishika kuondoka kwenye timu hiyo akacheze soka lake huko Real Madrid.

Kumbuka Mbelgiji huyo wakati anatua Stamford Bridge ulikuwa usajili wa Abramovich mwenyewe. Kipindi ambacho Hazard anakwenda kujiunga na wababe hao wa London, Chelsea ilikuwa haina kocha.

Ilitoka kumfuta kazi Roberto Di Matteo na haikuwa imemtangaza kocha mpya bado. Lakini, hili la kubaki Sarri hadi sasa linasemwa kwamba ni uthibitisho wa Abramovich kuikinai timu yake. Kwamba kwa sasa hana machungu tena kama ilivyokuwa huko nyuma na ndio maana kumekuwa na maelezo mengi ya kutaka kuipiga bei. Kinachoelezwa na wengi ni kwamba Abramovich anasubiri tu ofa nzuri iwekwe mezani aipige bei klabu hiyo. Ripoti zinadai mwenyewe anataka mkwanja unaoanzia Pauni 2 bilioni kupanda juu.

Bila shaka kama Hazard ataondoka, basi Chelsea itakuwa imeanza upya. Wachezaji waliopo wengi ni wa kawaida. Sawa wanavipaji, lakini bado hawana uwezo wa kuibeba timu kwenye mazingira ya kuhitaji ushindi wa lazima.

Jambo jingine ni kwamba timu inapopoteza mchezaji wake mzuri kuna mengi yanayoweza kutokea baada ya hapo. Hazard akiondoka, basi haitashangaza ukisikia N’Golo Kante naye akiondoka.

Lakini, kumaliza nje ya Top Four kwenye Ligi Kuu England msimu huu itakuwa kosa kubwa sana kwa Chelsea. Mwonekano bado mdogo sana kuweza kufuzu kwa kuwa kuna timu mbili zinazotakiwa hadi sasa maana Liverpool na Manchester City tayari zimeshapita.

Angalia kuna Manchester United, Arsenal, Tottenham na yenyewe Chelsea nani ataenda, nani atabaki ?

Kisha kushindwa kubeba ubingwa wa Europa League ili kupata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya ni jambo litakowapa pigo kubwa wababe hao wa Stamford Bridge.

Itakuwa ngumu kwao kuvutia wachezaji wazuri kwenye kikosi chao. Shida nyingine inayowakabili ni kuhusu kuzuiwa kusajili. Hayo yote ni ya baadaye, lakini la sasa ni kuhusu Sarri na mfumo wake wa ufundishaji.

Abramovich asingemwaacha salama hadi sasa. Chini ya Sarri, viungo wa Chelsea wamekuwa nadra kupiga pasi za kwenda mbele. Jorginho anayemng’ang’ania amekuwa mtu wa kupiga pasi za pembeni tu. Anasifa ya kupiga pasi nyingi, lakini hakuna yenye maana. Jorginho hana tofauti na mtu mwenye meno mengi, lakini yote mabovu. Ni mchezaji wa Sarri na anang’ang’ania acheze. Hilo linawakera sana mashabiki wa Chelsea bila ya shaka lingemkera pia Abramovich kama angekuwa mtu wa kwenda uwanjani kuitazama Chelsea ikicheza kwa msimu huu. Sarri pia hataki kutoa nafasi kwa wachezaji makinda kuonyesha uwezo wao. Hana tofauti na Jose Mourinho na hilo ndilo lililochangia pia kiharibika kwa kibarua chake kwenye timu nyingi alizokwenda kufanya kazi. Hakuna kificho, Sarri ana bahati kuendelea kubaki Stamford Bridge hadi sasa. Ashukuru Abramovich kutokuwa na kibali cha kuingoa Uingereza, ingekula kwake kitambo sana.