MTAA WA KATI : Hapa naweka shilingi yangu kwa babu Wenger

Muktasari:

Giroud alidhani kwamba amewarudisha mchezaji The Blues, alipounganisha vyema kabisa krosi ya Mason Mount kwenye mchezo wao wa Ligi Kuu England dhidi ya Man United. Giroud akashangilia.

ARSENE Wenger ameshuhudia mabao mengi mazuri. Mengi tu. Yaliyofungwa na wachezaji wake na yale yaliyofungwa na wachezaji wa timu nyingine. Ameshuhudia mengi tu. Yaliyohusu mechi zake na hata yaliyohusu mechi za wengine.

Kwa sasa ameondoka kwenye ukocha na kufanya kazi ya kusimamia maendeleo kwenye Shirikisho la Kimataifa ya Mpira wa Miguu (Fifa).

Jumatatu iliyopita alishuhudia bao jingine zuri lililofungwa na mchezaji wake wa zamani, Olivier Giroud. Lakini, safari hii akiwa tayari bosi wa Fifa na Giroud akiwa kwenye jezi ya Chelsea, wapinzani wake wa zamani wa huko London alipokuwa na Arsenal yake.

Giroud alidhani kwamba amewarudisha mchezaji The Blues, alipounganisha vyema kabisa krosi ya Mason Mount kwenye mchezo wao wa Ligi Kuu England dhidi ya Man United. Giroud akashangilia.

Lakini, ile anamaliza kushangilia tu anaambiwa kuna mwamuzi anaitwa VAR amelikataa bao hilo. Kwamba Giroud alikuwa ameoteza. Alizidi kwa inchi tu, tena kilichozidi ni kiatu chake.

Ulikuwa ni uamuzi ambao ulisababisha machungu kwa Chelsea na hatimaye wakachapwa katika mchezo huo 2-0 wakiwa nyumbani Stamford Bridge. Frank Lampard hakuwa na namna zaidi ya kukubali tu maamuzi hayo ya teknolojia japo kishingo upande.

Lakini, bao hilo limemwibua Wenger. Akiwa sasa mkuu wa maendeleo ya soka duniani, anataka kumaliza utata huu wa uamuzi wa VAR.

Wenger anataka kuwarudishia nguvu washambuliaji. Anataka kurudisha nguvu ya mashabiki kushangilia bao linapofungwa kwa mara ya kwanza na si kusubiri VAR inasemaje.

Ukweli ni kwamba VAR imesababisha huzuni kwa waliokumbwa na jambo hilo. Ni nzuri ikienda upande wako, lakini ni mbaya ikipingana na wewe. Wenger anataka kurekebisha mambo kwenye sheria ya kuotea.

Anachokitaka Wenger ni kwamba sheria ya kuotea ibadilishwe na badala yake isiwe inahusu viungo vyote vya mchezaji aliyefunga, bali kihusike kiungo kilichofunga tu.

Kwa mfano, kama bao limefungwa kwa kichwa, basi kitazamwe kichwa kabla ya kufunga kilikuwa kimeotea na kama ni mguu, goti, kisigino, basi kitazamwe kwa muktadha huo na si vinginevyo.

Asihuhumiwe mchezaji kwamba ameotea na bao lake alilofunga kukataliwa kwa sabatu mkono ndio uliokuwa kwenye eneo la kuotea, wakati yeye amefunga kwa staili ya n’ge, mpira ukiwa nyuma yake.

Wenger anaona hiyo ndiyo njia sahihi ya kuacha kuyakataa mabao mazuri. Huo ndio mpango wake, kwamba mchezaji atahesabika ameotea kama tu bao alilofunga, kiungo cha mwili kilichotumika kufunga bao hilo kitakuwa kimeotea, vinginevyo basi haiwezi kuwa mfungaji ameotea kama kilichotumika kufunga kilikuwa sawa na beki wa mwisho au kipo nyuma ya beki wa mwisho.

Ni mpango mzuri. Walau huu utakuwa mpango wa kurudishia nguvu washambuliaji ambao wamekuwa wakishuhudia mabao yao mazuri yakiporwa na VAR.

Nakubaliana na Wenger kwenye hilo kwa sababu ukweli ni VAR imekuja kuondoa ile ladha halisi ya mchezo wa soka. Sawa dunia ya sasa ni teknolojia, lakini soka ilikuwa na utamu wake wa mambo yenye utata.

Vitu vyenye utata kwenye soka ndivyo vimekuwa vikisababisha mijadala mingi kwenye vijiwe na watu kubishana kwa aina ya mabao ambayo timu zao zimefungana.

Bao lile la kuotea, lile sio la kuotea ndicho kitu ambacho kimekuwa kikileta ladha ya kipekee kwenye soka.

Lakini, VAR imekuja kuliondoa hilo hata kwa yale mabao ya kutoa ambayo kwa macho ya kawaida tu ngumu kuyaondoa.

Sasa katika kuyafanya baadhi ya mabao matamu yanabaki ili yaendelee kuwepo kwenye kumbukumbu, mpango huo wa Wenger utanusuru mengi.

Walau sasa naweka shilingi yangu kwenye mpango huo wa babu huyu, utatufanya tuendelee kushuhudia mabao mazuri yanafungwa na kuyaweka kwenye rekodi kuliko kukataliwa na VAR kwa sababu ya kuotea kunakohitaji teknolojia kubwa sana kuona.