STRAIKA WA MWANASPOTI : Ligi Kuu England ndio kwanza kama inaanza vile!

Tuesday April 2 2019

 

By Boniface Ambani

BAADA ya mapumziko kidogo ya mechi za kimataifa, mashindano ya kuwania nafasi za Euro, Ligi Kuu ya England imerejea wikendi iliyopita kwa kushindo. Ligi hiyo ambayo ni kipenzi cha Wana wa Afrika Mashariki imerudi kwa moto kwelikweli.

Najua Ligi Kuu ya England ina wafuasi wengi sana katika kanda yetu hii. Kuna mashabiki wengi wa Manchester United, Arsenal, Liverpool, Manchester City, Chelsea, Tottenham na timu nyingine.

Wengi tunaipenda ligi hiyo kutokana na ushindani mkali iliyonayo tofauti na nyingine barani Ulaya ambazo zinakuwa na ligi ya timu moja ama mbili tu kila mwaka.

Ligi Kuu England huwezi kutabiri mechi zake kama timu hizi kubwa nilizozitaja hapo juu ambazo zinaunda Big Six zinapocheza na timu nyingine zisizokuwa na majina wala wafuasi wengi.

Pamoja na vita ya kuwania taji la ligi hiyo kubaki farasi wawili tu, Liverpool ambayo imebakisha mechi sita kumaliza msimu ikiongoza ikiwa imecheza mechi 32 na kuzoa alama 79.

Liverpool iko mbele kwa alama mbili tu juu ya mpinzani wake wa karibu sana Manchester City ambayo iko katika nafasi ya pili ikiwa na alama 77.

Ushindi mgumu wa Liverpool juzi Jumapili wa mabao 2-1 dhidi ya Tottenham uliipa timu hiyo alama tatu muhimu sana katika harakati zake za kunyakua taji hilo kwa mara ya kwanza tangu 1990.

Hiyo ni zaidi ya miaka 29 tangu inyakue taji hilo. Mohamed Salah, Sadio Mane, Roberto Firminho, Van Dijk, James Milner ni baadhi tu ya wachezaji tajika kwenye kikosi hicho ambacho kimesukuma gurudumu hilo la Liverpool tangu msimu uliopita.

Aliyekuwa mshambuliaji wa kikosi hicho enzi zake, Ian Rush ambaye alikuwa katika kikosi kilichoshinda taji mwaka 1990 amewapa changamoto kubwa wachezaji wa Liverpool hasa Salah.

Ian Rush amemhimiza jambo Salah ili aweze kuhakikisha taji hilo amelishinda msimu huu na kuiondolea nuksi ya mataji timu hiyo. Msimu uliopita Salah alikuwa mfungaji bora. Sawa, lakini Rush anasema tuzo za kipekee huwa hazisaidii klabu sana.

Rush anamwambia Salah kama akitaka kuacha sifa tele pale Anfield ni lazima ashinde hilo taji msimu huu. Anachokisema Ian Rush kwa Salah ni kitu cha maana sana, kwani siku zote mchezaji bila mataji sio mchezaji tena.

Wachezaji wanaotamba duniani wanatambulika kwa mataji ambayo wameyashinda hasa ya Ligi Kuu ama Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.

Liverpool ingali ipo kwenye mbio za kunyakua taji la Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kufuzu kwa hatua ya robo fainali ambapo sasa itacheza dhidi ya Porto ya Ureno.

Klabu hiyo ilifika hatua hiyo baada ya kuitoa timu ngumu ya Ujerumani, Bayern Munich.

Shida kubwa kwa Liverpool iko kwenye Ligi Kuu England ambako taji lake linawaniwa na Manchester City inayonolewa na Kocha Pep Guardiola.

Guardiola anamnyima sana raha Jurgen Klopp. Jamaa halali kwani Man City iko katika nafasi ya pili na alama 77 baada ya kuizamisha Fulham kwa mabao 2-0. Kumbuka ina kiporo kimoja mkononi.

Kama Maaachester City ikishinda kiporo hicho itakuwa inarejea kileleni mwa jedwali hilo. Hapa patachikimbika. Kazi ipo na kulingana jinsi ligi ilivyo hadi sasa, tunatazamia kuona mbio hizi hadi mwisho wake.

Mtu alisema ligi hii ni kama mbio za nyika, huwezi kumbishia, atakayechoka shauri yake. Mpaka sasa Liverpool imebakisha mechi sita dhidi ya Southampton, Chlesea, Cardiff, Huddersfield, Newcastle na Wolverhampton.

Kwa upande wa Manchester City ina mechi saba ambazo ni dhidi ya Cardiff, Tottenham, Crystal Palace, Manchester United, Burnley, Leicester City na Brghton.

Tukiachana na vita hiyo ya ubingwa kuna nyingine ya kutafuta nafasi ya kuingia nne bora. Hapo kuna nafasi mbili tu ukiziondoa Liverpool na Manchester City kuiwakilisha nchi katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Vita ya kuwania nafasi hizo mbili iko kwa Tottenham, Manchester United, Arsenal na Chelsea. Jiulize nani ataenda na nani atabaki?

Ni kivumbi kwelikweli. Tottenham haikujitendea haki baada ya kukubali kufungwa na Liverpool juzi Jumapili.

Manchester United ilijitendea haki baada ya kuifunga Watford mabao 2-1 uwanajani Old Trafford.

Kocha Ole Gunnar Solskjaer alipata ushindi wake wa kwanza baada ya kukabidhiwa mikoba rasmi ya kukinoa kikosi hicho kwa kupewa kandarasi ya miaka mitatu.

Chelsea nayo pia ilijiweka pazuri baada ya kushinda mabao 2-1 dhidi ya Cardiff. Jana Jumatatu ilikuwa zamu ya Arsenal kumenyana na Newcastle United.

Kama imeshinda ( nadhani unayajua matokeo) itaaruka hadi nafasi ya tatu. Vita hii inakuwa tamu zaidi kwa sababhu timu hizo zote zimeachana alama moja tu. Tottenham imebaki na alama zake 61, Man United pia ina 61, Arsenal ina alama 60 kama Chelsea.

Nani atamwachia nani aingie kwenye nafasi hiyo? Kumbuka Liverpool imebakisha mechi kubwa moja dhidi ya Chelsea wakati Man City imebakisha na wakubwa wawili, Manchester United na Tottenham ambao wote wanataka kuingia Top Four. Kazi bado mbichi Ligi Kuu England ndio kwanza kama inaanza.

Advertisement