STRAIKA WA MWANASPOTI : Kwani Simba, Leopards na Yanga kuna nini?

Muktasari:

  • Yalikuwa mashindano mazuri ambayo yalihusisha klabu zetu kongwe za Afrika Mashariki za AFC Leopards, Gor Mahia (Kenya) na Simba na Yanga zaTanzania.

NACHUKUA fursa hii kuzipongeza Klabu za Bandari, Kariobangi Shark na Mbao FC kwa kazi nzuri sana ambayo ziliifanya juzi tu katika Mashindano ya SportPesa Super Cup yaliyoandaliwa jijini Dar es Salaam.

Yalikuwa mashindano mazuri ambayo yalihusisha klabu zetu kongwe za Afrika Mashariki za AFC Leopards, Gor Mahia (Kenya) na Simba na Yanga zaTanzania.

Klabu za Yanga, Leopards na Gor Mahia ziliondolewa katika raundi ya kwanza, Simba ikimfunga AFC Leopards, Yanga ikipigwa na Kariabangi Sharks, Gor Mahia ilibanduliwa na Mbao FC katika hatua ya matuta.

Ni mara ya tatu sasa haya mashindano yanaandaliwa na mshindi wa mashindano ya kwanza na ya pili alikuwa Gor Mahia ya Kenya.

Mshindi wa kwanza kwa mara ya tatu sasa ni Kariobangi Sharks kutoka Kenya pia. Swali langu kwa Watanzania kwenu mnaona sawa tu kila wakati kombe linaondoka Dar es Salaam likielekea Nairobi?

Shida yenu kubwa na yafaa mbadilishe fikra hizi, ni kwamba Simba na Yanga macho yao yote yanaangaliana tu. Simba kufungwa ni sherehe kwa Yanga na Yanga kufungwa ni sherehe kwa Simba.

Nadhani bado tunaishi katika maisha ya kale. Timu lazima zibadilike na kuwa na maisha ya kisasa. Ukiona maandalizi ambayo viongozi wa Yanga wanafanya wakati wanataka kucheza na Simba ni makubwa sana, utadhani timu inataka kucheza fainali ya Kombe la Dunia.

Wachezaji watapelekwa kwa hoteli za kifahari, watalala New Afrika, Kempinski na kadhalika. Au timu itapelekwa Visiwa vya Zanzibar, Unguja au Pemba. Itafanya mazoezi kwa viwanja vizuri. Kila kitu wanachohitaji wachezaji wanapewa lakini ukiangalia maandalizi wakati wanapocheza na klabu nyingine inatia aibu sana.

Mechi ni mechi, zote zina alama tatu tu. Lipi kubwa Afrika ambalo Simba na Yanga zinaweza kujivunia? Yanga kumfunga Simba ama Yanga kumfunga Al Ahly ya Misri, Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, Asante Kotoko ya Ghana, Etoile Du Sahel ya Tunisia lipi jambo kubwa?

Ukitaka kujitangaza ubabe katika bara hili la Afrika lazima uwe mstari wa mbele. Lazima utikise Afrika. Maandalizi ya hizi klabu mbili kwa ukweli ni duni wakati zinakutana klabu nyingine za Afrika.

Wakati Yanga inacheza na Simba hapo ndipo sasa viongozi wote wa Yanga wataenda kambini na kutoa ahadi kibao kwa wachezaji ‘wafungeni Simba tutawafanyia hivi na vile.’

Mambo hayo yanayofanyika Yanga na kwa upande wa watani zao, Simba ni vivyo hivyo.

Watapewa ahadi nzuri wakikalibia kucheza na Yanga, wachezaji watakula vizuri kwa hoteli ya kifahari na kupelekwa Zanzibar.

Hivi mambo haya yataendelea hadi lini? Mara ya mwisho Yanga kushinda mashindano ya kanda hii ni msimu wa 2009/2010 iliponyakua Tusker Cup pale Tanzania.

Fainali ikiwa Sofapaka na Yanga. Hapo nikiwa mchezaji nikitokea katika benchi dakika 10 za mwisho na niliweza kuichinja Sofapaka na kombe likabaki Dar es Salaam. Watanzania hasa viongozi wa Simba na Yanga, hamuoni aibu kila kukicha Kombe la SportPesa Super Cup linapanda ndege na mihela ikirudi Kenya?
Nyie kwenu ni jambo la kawaida tu. Bahati mbaya, hata ukitaka kumuoa Binti Bahati lazima umpambie kila kukicha. Tanzania imebaki na vijembe vya Simba na Yanga kuanzia asubuhi usiku hata hakuna kulala. Maisha ya soka yatakuwa hivyo hadi lini? Inafaa muamke.

Kitu cha pili tunafaa tujiamini na makocha wetu wazawa. Tazama Kocha Ben Mwalala, tazama kocha wa Sharks, tazama kocha wa Mbao FC. Nilifurahishwa sana na hizo klabu na zote zilikuwa na wachezaji kutoka kanda yetu.

Kama Mbao FC ikizidi kupiga lile soka ililolionyesha kwenye michuano hiyo itafika mbali. Ilionyesha uchu wa kushinda kombe. Ilipigana kwa udi na uvumba, kumaliza namba nne sio mchezo na ni mara yake ya kwanza kushiriki mashindano haya makubwa Afrika Mshariki.

Wakati umewadia kwa viongozi wa Simba, Yanga, Gor Mahia na AFC Leopards wajifikirie, angalau Mahia haipo vibaya vile. Nikiangalia katika soka letu inawakiIisha Kenya katika Mashindano ya Afrika na imekuwa ikifanya vizuri tu. Imeshinda taji la SportPesa Super Cup mara mbili.

Simba nayo iko kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, ilianza vizuri mchezo wa kwanza kabla ya kuharibu dhidi ya AS Vita pale DR Congo. Lakini vipi kwa Afrika Mashariki? Simba, Yanga na AFC Leopards kulikoni?

Kazi nu kutamba mitandaoni lakini la msingi hatulioni. Tubadilike, ubabe ni kushinda mataji ya Afrika. Maandalizi ya kila mechi lazima yawe ya kweli. Usajili uwe wa juu. Bila hivyo miaka nenda miaka rudi nyimbo zitakuwa zilezile. Acha tujaribu mwakani. Mwakani hadi lini? Hongera Kariobangi Sharks kwa kutwaa ubingwa mwakani itakipiga na Everton jijini Nairobi. Ben Mwalala na kikosi chake cha Bandari hongera. Mbao FC endeleeni vivyo hivyo.