Kwa Kagame hii afadhali hata Ndondo Cup

Muktasari:

  • Wawakilishi hao ni mabingwa watetezi Azam FC, mabingwa wa Ligi Kuu (VPL) Simba, JKU na Singida United.

MICHUANO ya Kombe la Afrika Mashariki na Kati maarufu kama Kombe la Kagame inaendelea jijini Dar es Salaam huku Tanzania ikiwa na wawakilishi wanne.

Wawakilishi hao ni mabingwa watetezi Azam FC, mabingwa wa Ligi Kuu (VPL) Simba, JKU na Singida United.

Timu zote nne zimefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo. Hii ni hatua nzuri kwa wawakilishi wa nchi ingawa mashindano yenyewe yanaonekana kutokuwa na mvuto.

Mashindano ya sasa hivi hayasisimui kabisa wala hayana mvuto hata ushindani wake ni mdogo ukilinganisha na miaka kadhaa iliyopita.

Kumbuka mashindano hayo kwa mara ya mwisho yalifanyika nchini mwaka 2005 na Azam kubeba taji kwa rekodi tamu ya kutofungwa hata mechi moja.

Kama haitoshi Azam iliyocheza fainali na Gor Mahia, ilimaliza michuano hiyo bila hata safu yake ya ulinzi kuruhusu bao hata moja!

Pamoja na kwamba mashindano hayo yalianza kupoteza mwelekeo wake siku nyingi lakini michuano ya mwaka 2005 ilikuwa na msisimko kulinganisgha na mwaka huu.

Naamini mashabiki wengi wa soka wanatamani kuona mashindano hayo yanakuwa na msisimko wake kama miaka iliyopita.

Mashindano ya Kagame yalijaza watu uwanjani kushuhudia timu zao tofauti na sasa unaweza kuchukua dakika zako kadhaa kuwahesabu mashabiki waliofika uwanjani.

Ni wazi kwamba hata waandaaji wa mashindano hayo ukiachana na timu shiriki wameona jinsi mwenendo ulivyo na kama ni hasara, basi mwisho wa mashindano faida itakuwa ndogo kama lengo lao ni kuingiza pesa.

Tatizo lipo wapi? Haya mashindano yamekuwa yakilegalega kadiri siku zinavyosonga mbele na pengine mwaka huu usingekuwa udhamini wa Azam huenda yangepigwa kalenda tena kama miaka miwili iliyopita tangu Azam FC ilipotwaa ubingwa huo.

Katika mashindano hayo mechi ambayo ingekuwa na mvuto kwa mashabiki wa soka ingekuwa ni ile ya Simba dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga.

Yanga ilijitoa siku chache kabla ya mashindano hayo kwa sababu ya kuwa na muda mfupi wa maandalizi yao ya mechi yao ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Gor Mahia ambayo nayo inashiriki Kombe la Kagame .

Viongozi wa Shirikiso la Vyama vya Soka vya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) waliona njia mwafaka ya kurudisha msisimko wao kwenye michuano hiyo ni kuzipanga tSimba na Yanga katika kundi moja.

Mpango huo ulifeli na kuwafanya mashabiki kukata tamaa japokuwa siyo sababu kubwa ya kudorora kwa mashindano haya makubwa ya Afrika Mashariki.

Kingine ni kuyaleta mashindano hayo kipindi ambacho kuna Kombe la Dunia. Sijui viongozi wa Cecafa walishindwaje kuangalia kwa jicho la tatu kuhusu suala hili.

Labda kwa kuwa hayajafanyika kwa muda mrefu ndio maana wakaona ni bora liende tu.

Viongozi wa Cecafa ambao wanasimamia mashindano hayo chini ya Katibu Mkuu Nicholous Musonye wanatakiwa kuliangalia hili kwa mapana zaidi na wasichukulie kwamba ni kitu cha kawaida. Ni lazima hapo kuna jambo la kufanyiwa kazi.

Mara kadhaa Musonye amekuwa akilalamika kuna viongozi wa Cecafa wanahujumu michuano hiyo.

Ingekuwa jambo la busara sana kama kiongozi huyo angeweka bayana hilo ili kuwafanya wananchi kujua ni nani mchawi wa Kombe la Kagame. Haitoshi tu kulalamika bila ya kuwa na ushihidi wa kutosha juu ya hambo hilo. Lakini Musonye akaumbuke baadhi ya nchi zilijiondoa katika Cecafa ya mwanzo kutoakana na ubabaishaji. Musonye amesahau kuwa nchi za Zimbabwe, Zambia, Malawi na nyingine zikuwa chini ya umoja huo. Anayalinganishaje mashindano haya na yakle ya kipindi kile?

Inawezekana miaka mingine ambayo michuano hi haikufanyika ni kutokana na kukosa udhamini lakini je, Cecafa ina njia gani mbadala wa kurudisha mvuto wa Kagame Cup.

Timu shiriki huenda zinayatumia mashindano hayo kama ni maandalizi tu ya mashindano yao yajayo ama kwa timu za hapa Tanzania huenda yanatumia kuangalia vikosi vyao.

Hii ni mbaya maana akili yao haipo kwenye ushindani bali ipo kutengeneza vikosi.

Musonye na viongozi wenzake kwa miaka miwili ambayo walishindwa kufanya mashindano hayo watakuwa wamejifunza kitu na kupata majibu kwanini wamefikia hatua hii ambayo hata mechi za Ndondo zinakuwa na mshabiki wengi. Kuna mashabiki wengine wanaweza kuona ni bora wakaangalie Ndondo kuliko Kombe la Kagame sasa.