STRAIKA WA MWANASPOTI : Kongole Afrika Mashariki kwa kufuzu AFCON 2019

Muktasari:

  • Mabao mawili yaliyotiwa kimiani na beki, Aggrey Moris, mshambuliaji, Saimon Msuva na Erasto Nyoni aliyefunga kwa penalti yalitosha kuiwezesha Tanzania kufuzu.

KWA mara ya kwanza kabisa Kanda hii ya Afrika Mashariki litawakilishwa katika fainali za mataifa ya Afrika na timu nne. Hii ni mara ya kwanza katika historia ya kanda hii kuwakilishwa na idadi kubwa ya timu.

Haijawahi kutokea. Imekuwa furaha tupu na Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) na linajivunia kwelikweli mafanikio haya.

Timu za Taifa ya Kenya, Harambee Stars, Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Uganda ‘The Cranes’ na Burundi ‘Intamba m’Urugamba’ zimefuzu zote kuwakilisha nchii zao katika mashindano ya kimataifa barani Afrika.

Juzi Jumapili kulikuwa na vifijo na nderemo jijini Dar es Salaam baada ya Taifa Stars kuinyuka Uganda kwa mabao 3-0 ndani ya Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mabao mawili yaliyotiwa kimiani na beki, Aggrey Moris, mshambuliaji, Saimon Msuva na Erasto Nyoni aliyefunga kwa penalti yalitosha kuiwezesha Tanzania kufuzu.

Ilikuwa ni mshikemshike na kushikilia roho kwa pande ile nyingine Lesotho ilikuwa katika uwanja wa ugenini ilipokuwa ikicheza dhidi ya Cape Verde.

Hata hivyo, mechi hiyo iliishia kwa sare tasa. Iwapo Lesotho ingeshinda basi ingekuwa kizungumkuti kwa Tanzania kufuzu hatua ya fainali ambayo itachezwa kule Misri.

Timu zote zingekuwa na pointi nane, lakini uwiano wa mechi za kufunga na kufungwa ungeangaliwa kwa kuwa kila kitu kingekuwa kinafanana.

Lakini Maulana, Mwenyezi Mungu alilishikilia Taifa la Tanzania likafuzu kwa mara ya kwanza katika fainali hizo baada ya miaka 39 kwani muda mrefu ilikuwa ikijaribu lakini bila ya mafanikio.

Wakati huo huo ikumbukwe Uganda Cranes ilikuwa tayari imeshafuzu kama mshindi wa kwanza kwenye kundi hilo la L.

Harambee Stars nayo ilikuwa katika kundi moja na Ethiopia, Sierra Leone na Ghana. Baada ya kubanduliwa kwa Sierra Leone kundi hilo lilibaki na timu tatu tu.

Kenya, Ghana na Ethiopia. Hatimaye Kenya ilimaliza katika nafasi ya pili nyuma ya washindi wa kundi hilo Ghana. Katika mchezo wa mwisho jijini Accra Ghana, Black Stars ilishinda mechi hiyo kwa bao 1-0. Hata hivyo, tayari Kenya ilikuwa ishafuzu.

Burundi vilevile ilifuzu kwa mara ya kwanza kabisa kutoka kwa kundi lao la C baada ya kumaliza ya pili nyuma ya washindi wa kundi hilo Mali. Kundi hilo lilijumuisha Gabon na South Sudan.

Ni jambo la muhimu kuona timu zetu za taifa zikifuzu katika mashindano hayo. Kanda hili likuwa limelala kabisa.

Angalau Sasa tunajivunia kuona timu zetu katika mashindano hayo yatakayoandaliwa jijini Cairo, Misri.

Mafanikio ya kanda hii ya Afrika Mashariki yalianza kutengenezwa na klabu za Gor Mahia ya Kenya na Simba ya Tanzania.

Gor Mahia ilifuzu kwa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Confederation Cup), wakati Simba Sports Club ikifuzu robo fainali katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika.

Hii inakuonyesha Nini?

Inatuonyesha iwapo tutaendelea kuendesha soka letu vizuri na kuzingatia umuhimu wa ukuzaji wa talanta kuanzia utotoni, basi si ajabu ndani ya miaka mingine mitano haya mataji tutayaleta kanda hii.

Uganda kumbuka inaenda kushiriki fainali hizi za AFCON kwa mara ya pili mfululizo.

Walikuwepo katika fainali zilizopita wakaona utamu wa kushiriki mashindano hayo na waliweka mikakati za kufuzu mapema. Kweli wakafuzu.

Kenya nayo mara ya mwisho kuwepo katika mashindano hayo ilikuwa miaka 15. Raundi hii imefuzu. Kwa hivyo, viongozi lazima waamke. Timu zetu hizo zimeshafuzu. Hakuna sherehe za kufuzu. Maandalizi yawe sambamba ili kwenda kutoa ushindan mkali kule Misri.

Maandalizi yanafaa kuanza sasa. Wasingojee hadi dakika za mwisho ndipo waanze kurukaruka.

Viongozi wetu waweke mikakati kabambe za kuziwezesha klabu zetu na timu zetu za kimataifa ziweze kunawiri katika mashindano hayo.

Haitapendeza timu hizo zikifika kwenye fainali kule Misri zikaanza kuchapwa mabao ya kutia aibu. Haitakuwa sawa hata kidogo.

Hatutapenda kusikia visingizio vingi kutoka kwa benchi la ufundi na wachezaji baada ya kufungwa na kutolewa mapema.

Ni afadhali kuchukua tahadhari mapema kabla ya hatari tunayoenda kupambana nayo kule Misri.

Wadau wa soka na serikali wasiziache timu hiz bila ya kuzipa msaada wa maandalizi ya mapema. Lazima mzipe ushauri na msaada wa hali na mali. Ushauri ambao utawezesha kujipanga vyema.

Hatutaki kufika Misri na kubanduliwa raundi ya kwanza. Angalau timu mbili tatu zifuzu katika robo fainali.

Ikumbukwe katika kanda hii ya Cecafa ni Rwanda na Sudan Kusini tu ndio zilizokosa kufika katika fainali za mashindano hayo. Rwanda ilimaliza ya mwisho katika kundi lake la H.

Hata hivyo, sio neno sana, jambo la umuhimu kwa Rwanda na Sudan Kusini ni kujipanga. Wajiulize walikosea wapi? Wakati watakapojua watajipanga ili kuweza kushiriki fainali hizo zitakapoandaliwa tena. Lakini kwa sasa mashabiki wa soka wa nchi hizo wanapaswa kutoa sapoti nzuri kwa timu za Kanda ya Afrika Mashariki zilizofuzu kwa fainali za mwaka huu.