TIMUA VUMBI : Kamati ya Nidhamu TFF imewasahau kina Morrison,Mkude

Muktasari:

Tangu wachezaji hao wapelekwe kwenye kamati hiyo inakaribia mwezi mmoja pasipo kamati kutoa tamko lolote endapo walikutana ama la. Lakini imedaiwa kuwepo na ugumu wa kukutana kwa wajumbe wa kamati hiyo kutokana na majukumu yao binafsi hivyo kila wanapopanga kukutana kolamu yao haitimii na kushindwa kufanya maamuzi yoyote.

SHIRIKISHO la Soka la Tanzania (TFF) lina kamati zake mbalimbali ambapo baadhi ya kamati zipo huru kwa maana ya kwamba haziingiliwi na taasisi hiyo.

Kamati hizo huundwa na Kamati ya Utendaji ya TFF chini ya Rais Wallace Karia na moja ya Kamati huru ni Kamati ya Nidhamu iliyo chini ya Mwenyekiti, Wakili Kiomoni Kibamba.

Februari 22, 2020, mshambuliaji wa Yanga, Bernard Morrison alipelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya shirikisho hilo kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa Tanzania Prisons baada ya Kamati ya Saa 72 kuamua kumpeleka huko.

Siku nne baadaye yaani Februari 26, 2020, kiungo wa Simba Jonas Mkude naye alitupwa kwenye kamati hiyo kwa kosa kama la Morrison, kumpiga kiwiko mchezaji wa Biashara United.

Tangu wachezaji hao wapelekwe kwenye kamati hiyo inakaribia mwezi mmoja pasipo kamati kutoa tamko lolote endapo walikutana ama la. Lakini imedaiwa kuwepo na ugumu wa kukutana kwa wajumbe wa kamati hiyo kutokana na majukumu yao binafsi hivyo kila wanapopanga kukutana kolamu yao haitimii na kushindwa kufanya maamuzi yoyote.

Kutokana na hilo, wachezaji pia wapo njia panda juu ya hatima yao huku wadau wa soka wakibaki na maswali juu ya kamati hiyo inavyofanyakazi zake kwa wakati.

Moja ya maswali yanayoumiza vichwa wadau wa soka nchini ni kwanini wajumbe wa Kamati nyeti kama hiyo wasiwe wale wa kuajiriwa moja kwa moja na taasisi hiyo ili kila muda wapatikane ofisini?

Kwamba endapo Karia akaamua kuteua watu ambao watakuwa na jukumu la kushughulikia majukumu ya mpira pekee itaondoa sintofahamu kwa watu na pia itarahisisha kutokuwa na mlundamano wa kesi kukaa muda mrefu kwasababu tu wajumbe wamebanwa na majukumu mengine binafsi. Inaonyesha wajumbe wote wa kamati hiyo ni waajiriwa sehemu nyingine, hivyo si rahisi kwa wajumbe hao kuacha majukumu ya waajiri wao kuliko kazi ya ‘udeiwaka’.

Tuhuma za wachezaji hao ambao wakibainika kwamba wametenda makosa hayo kanuni ipo wazi kuwa wanafungiwa mechi tatu, lakini hadi sasa muda unazidi kwenda na haitakuwa ajabu hata ligi ikimalizika kesi hizo zisijaridiwe. Je, uamuzi huo unachelewa kwasababu ni wachezaji wa Simba na Yanga au?

Inanikumbusha miaka ya nyuma aliyekuwa mchezaji wa Azam FC, Kipre Tchetche alipatwa na kosa lakini halikujadiliwa hadi ligi ilimalizika na mchezaji huyo akatimka nchini.

Karia kama kuna uwezekano hizi kamati nyeti wateuliwe watu ambao hawana majukumu mengi ya waajili wao ili wawe wanakutana kwa wakati na kutatua matatizo ya kimpira kwa muda mwafaka. Ni wazi watakuwa wanalipwa posho wanapokaa kwenye vikao hivyo, basi hizo posho Rais Karia azihamishie kwa wale ambao hawajabanwa sana, wachezaji wahukumiwe kulingana na makosa yao ili watumikie adhabu zao maisha yaendelee.

Siamini sana kama hakuna watu wengine wasiokuwa na majukumu wakapewa kazi hiyo kuliko hawa ambao wanaonekana wamebanwa na majukumu na waajiri wao.

Mkude na Morrison nadhani kila wanaposhtuka kuwa kuna kesi Kamati ya Nidhamu basi mioyo yao inaripuka kama wamebeba matanki ya mafuta ya petroli kuwa wataambiwa nini siku kamati ikikutana.

Rais Karia anatakiwa kufanya maamuzi mengine yatakayofanyakazi kwa haraka au kama si rahisi basi awaeleze ukweli kuwa kesi zisikilizwe kwa haraka kuepusha mlundamano wa kesi kwenye kamati yao.

Waamue kufanya kama walivyoamua Kamati ya Saa 72 kwamba wanakutana tu kila wanapopata taarifa kutoka kwa kamisaa wa mechi husika ingawa nayo awali ilikuwa ni kichomi.