Ilikuwa ni Bocco ama Chilunda

Muktasari:

  • Matokeo hayo yaliwanyong’onyesha mashabiki wa soka nchini na wachezaji kwani matarajio yao yalikuwa ni makubwa na ushindi huo wangeupata basi uhakika wa kwenda Cameroon mwakani haukuwa na shaka.

TAIFA Stars juzi Jumapili ilipoteza mechi yake na Lesotho ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0, mechi iliyochezwa jijini Maseru, Lesotho.

Matokeo hayo yaliwanyong’onyesha mashabiki wa soka nchini na wachezaji kwani matarajio yao yalikuwa ni makubwa na ushindi huo wangeupata basi uhakika wa kwenda Cameroon mwakani haukuwa na shaka.

Hivi sasa Stars ina kibarua kigumu cha kuhakikisha wanaifunga Uganda huku wakiomba kila dua wapinzani wao Lesotho ambao pia wana pointi tano wapoteze dhidi ya Cape Verde katika mechi yao ya marudiano.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wataalamu wa soka, walisema Kocha wa Stars Emmanuel Amunike alikuwa na mipango yake ambayo haistahili kuingiliwa lakini wamedai safu ya mbele alistahili kupangwa John Bocco pamoja na Shaban Chilunda.

Aliyewahi Kocha wa Taifa Stars, Dk Mshindo Msolla alisema hivi sasa sio wakati wa kutupiana lawama ama kumlaumu kocha huyo kwani ni wazi mipango yale imefeli, kinachotakiwa sasa ni kujipanga upya kwa ajili ya kuwadhibiti Uganda na kufuzu kwa Stars kupo mikononi mwa wachezaji wenyewe.

“Nafasi ipo kama nilivyosema kwa kuangalia mabao kama yatakuwa sawa, pointi sawa na nani alimfunga mwenzake, kikubwa tuwafunge Uganda na wanafungika tu,” alisema.

Naya mchambuzi Joseph Kanakamfumo mawazo yake yaliendana na mtazamo wa Dk Msolla, Amunike alipaswa kumwanzisha Bocco na Chilunda huku Msuva akianzia pembeni pamoja na Kichuya.

“Kwenye viungo unawaachana viungo kama Jonas Mkude, Fei anaanzia benchi pia kiufundi haikukaa vizuri pengine Amunike alikuwa na mipango yake ya ushindi. Ili tusonge mbele tunapaswa tushinde mechi ya mwisho kwani timu zote tatu, Stars, Lesotho na Cape Verde zina nafasi ya kufuzu mmoja,” alisema Kanakamfumu.

FATIKI

Imeelezwa kikosi cha Stars kilipoweka kambi yake Afrika Kusini kilifanyishwa mazoezi mara mbili kwa siku, jambo lililoelezwa kiufundi linaathiri miili ya wachezaji kwani wanachoka. Wote wanacheza mechi za ligi kuu hivyo walipaswa kufanya mazoezi mara moja kwa siku.

Kanakamfumu anaeleza kiufundi; “Hilo pia nimelisikia, sio zuri kwa afya za wachezaji, miili yao inachoka, mazoezi kama hayo yanatakiwa kufanywa wakati wa maandalizi ya muda mrefu kuelekea msimu mpya wa ligi, ligi ikianza wachezaji wanapaswa kufanya mazoezi mara moja kwa siku.”