TIMUA VUMBI : Huu uchaguzi wa Yanga una nini kwani jamani?

Muktasari:

  • Uchaguzi huo unaosimamiwa na Shirikisho la soka Tanzania (TFF) kupitia kamati yake ya uchaguzi chini ya Mwenyekiti, Ally Mchungahela ulipangwa kufanyika Januari 13.

UCHAGUZI wa kujaza nafasi zilizoachwa wazi ndani ya klabu ya Yanga uliahirishwa baada ya baadhi ya wanachama kufungua kesi ya kupinga kufanyika kwa uchaguzi huo.

Uchaguzi huo unaosimamiwa na Shirikisho la soka Tanzania (TFF) kupitia kamati yake ya uchaguzi chini ya Mwenyekiti, Ally Mchungahela ulipangwa kufanyika Januari 13.

Kamati hiyo iliamua kuahirisha uchaguzi huo ili kupisha amri ya mahakama kama kesi ya msingi ingesikilizwa na wanachama waliofungua jalada hilo kutoka mikoa minne.

Kamati hiyo inayoongozwa na watu wanaofahamu sheria waliifuatilia kesi hiyo na kubaini kwamba kati ya wanachama waliofungua kesi mmoja tu ni mwanachama hai mwa maana ya kwamba ndiye hulipa ada ya kila mwezi ya uanachama wake ndani ya Yanga.

Kwa taarifa iliyotolewa ni kwamba wanachama hao walikubali kufuta madai yao ili uchaguzi uendelee kama kawaida.

Mchungahela aliwatangazia wanachama na wagombea ambao walianza mchakato wao wa kufanya kampeni kuwa ndani ya siku saba watatangaza tarehe nyingine ya uchaguzi huo na jinsi ya kumalizia kampeni zao.

Hivi sasa uchaguzi huo unategemewa kufanyika muda wowote tu mara utakapotangazwa.

Mgogoro wa uchaguzi huu umeanza tangu TFF ilipotangaza kuanza kutoa fomu za wagombea mwaka jana, wanachama walipinga kuwa uchaguzi hao hauwezi kusimamiwa na shirikisho hilo kwani Katiba yao haielekezi hivyo.

Mbali na hilo, wanachama walio wengi wanapinga kujaza nafasi ya Mwenyekiti wakidai Yusuf Manji bado wanamtambua kuwa Mwenyekiti japokuwa alitangaza kujiuzulu.

Hata hivyo, msimamo wa baadhi ya wanachama ni kwamba walipokea barua ya kujizulu kwa Manji lakini hawakukubaliana na uamuzi huo hivyo uongozi wake unatambulika ingawa kikatiba hautambuliki.

Sasa uchaguzi umerudi mikononi mwa TFF baada ya waliofungua kesi ya kupinga uchaguzi kudaiwa kufuta shitaka hilo.

Kikubwa ninachopenda kusema ni kwamba uchaguzi ndani ya Yanga ufanyike ili mambo mengine yaendelee, si kwamba mambo hayafanyiki lah hasha ila yafanyike wakati timu ya uongozi imetimia.

Walibaki wajumbe wanne wa Kamati ya Utendaji kati ya 13 lakini hivi karibuni Salum Mkemi aliyejiuzulu amerejea kwenye nafasi yake kwa maelezo ya kwamba barua yake ya kujiuzulu haikujibiwa, hivyo wamefika wajumbe watano ambao kikatiba bado hawakidhi kuiongoza Yanga.

Sinema inayoendelea juu ya uchaguzi huu imechosha kuitazama, inatakiwa imalizike ili Yanga iingie hatua nyingine ya mafanikio maana kinachoendelea sasa hakileti afya ndani ya Yanga zaidi ya kurudisha nyuma maendeleo ya klabu.

Itafika wakati haitaeleweka sasa Yanga inataka nini kati ya mambo mawili maendeleo ama kufeli kimaendeleo, kwani bila uongozi hakuna jambo la maana linaloweza kupita na kufanikiwa zaidi tu ya kufanya mambo kwa ujanja ujanja.