JAMVI LA KISPOTI : Hili la Lukumay, Nyika ni la kuijenga Yanga mpya

Thursday March 28 2019

 

By Khatimu Naheka

NI wazi sasa zama za Yanga chini ya uongozi Yusuf Manji zimehitimishwa rasmi baada ya wajumbe wawili waliosalia madarani kujiuzulu jana.

Waliomalizikia kujiuzulu jana ni Kaimu Mwenyekiti Samuel Lukumay na Hussein Nyika ambaye alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano na Usajili na wote wakiwa wajumbe wa kamati ya utendaji wa kuchaguliwa.

Sababu yao ni moja tu, kupisha mchakato kamili wa uchaguzi na sio ule wa kujaza nafasi ambao ulikuwa ukienda na kukwama pale Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Yanga haikuwa sawa. Yanga ilikuwa na makundi yaliyokuwa yanasigana juu ya uimara wa uongozi wa klabu hiyo.

Yapo makundi ambayo yalikuwa hayakubaliani na mambo ya viongozi waliosalia madarakani.

Wapo pia wengine waliokuwa wanawakubali viongozi waliobaki na kila mmoja alikuwa akipambana na vita yake kwa nafasi yake na eneo lake.

Suala hili halikuwa linaipa TFF na hata serikali nafasi nzuri ya kuchagua wapi ni sahihi na wapi siyo sahihi.

Katika hali ya namna hiyo wale wasuluhishi nao walijikuta wanachagua timu mbili za kuchezea katika msigano huo na kuzidi kukoleza moto mbaya ndani ya klabu hiyo.

Kibaya zaidi wapo ambao wanaamini kwamba hakuna cha serikali (kwa maana ya Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo) wala TFF wanaoweza kutenda haki katika mgogoro huo. Na hapo ndipo ishu ya kuangaliana rangi (U-Simba na U-Yanga) likaanza.

Salama kwa Yanga ni kwamba wakati wote wa msigano huu, timu yao ilibaki salama ikiendelea kuongoza Ligi Kuu ya Tanzania Bara ikinusurika kuyumba vibaya kupitia migogoro hiyo ya kiungozi.

Hayo yote sasa yanaweza kufikia mwisho kupitia fursa hii iliyopatikana jana baada ya viongozi hawa kujitambua na kuamua kuikoa klabu yao.

Serikali sasa na hata TFF wanatakiwa kutulia na kuwaunganisha Wanayanga, kwanza kwa kuwarudishia mchakato wao wa uchaguzi usimamiwe na Wanayanga wenyewe wakishirikiana na Baraza la Wadhamini.

Chombo pekee ambacho sasa kina usafi ya kuisimamia Yanga ni Baraza la Wadhamini chini ya mwenyekiti wake George Mkuchika.

Kitakuwa kichekesho endapo atatoka mtu sasa na kuanza kusema hata baraza hilo hawalikubali. Huyo atakuwa haitakii mema klabu yake na hatakiwi kuendekezwa.

Wakati mwingine migogoro ya namna hii inachangia kwa kiasi kikubwa kukwamisha maendeleo ya taasisi lakini pia wapo ambao siku zote wamekuwa wakiishi kutokana na migogoro na wanajulikana.

Itashangaza kuona watu hawa sasa badala ya kuungana na wenzao kuhakikisha wanatapata uongozi kamili, wao wanapita huku na kule kupandikiza chuki. Hili halitakiwi kupewa nafasi.

Fursa iliyopo sasa imekuja wakati muafaka kwa serikali na hata TFF kuwa na uhuru wa kushirikiana na baraza la wadhamini wa Yanga kusuka mambo ya mchakato safi wa uchaguzi wa klabu hiyo.

Wanayanga sasa wanatakiwa kuwa na utulivu na kushirikiana katika mchakato uliopo ili kuunda uongozi mpya utakaomfukuzia mbali bundi pale Jangwani.

Advertisement