JAMVI LA KISPOTI : Heritier Makambo anapowasafisha kina Nyika

Thursday May 23 2019

 

By Khatimu Naheka

Yanga sasa habari njema kwao ni kukaribia kuuza mastaa wake akiwemo mshambuliaji Heritier Makambo anayetakiwa na klabu zisizopungua tatu.

Makambo ghafla anageuka almasi katika msitu wa Yanga ambao haukujua kama neema kubwa inaweza kushuka kwao katika mazingira ya namna hiyo.

Taarifa za kuuzwa kwa kina Makambo zikanifanya ghafla kukumbuka kelele za wakati fulani pale Yanga kuna watu wanaiba fedha tu kinyemele kupitia usajili.

Nikaanza kuwatafuta wale jamaa wanaojua kupiga makelele ya kuwachafua watu ili nijue Yanga ilikuwa inaibiwaje mbona mambo kama yanaenda mswano kwao.

Nilishtuka zaidi baada ya kiongozi mmoja wa sasa katika utawala wa Mwenyekiti Dk Mshindo Msola kuniambia katika uchunguzi wake kumbe Yanga ilitumia kiasi cha Dola 15000 (Sh34.2 milioni) tu kumsajili Makambo akiwa mchezaji huru.

Ghafla nikashika kichwa zaidi, kichwa kiliniuma nikichukua kiasi hicho kisha nikalinganisha na kiasi kidogo cha Dola 100000 (Sh230 milioni) ambacho ni ofa ya chini kabisa ambayo Makambo anahitajika na klabu ya Horoya AC ya Guinea na wanataka kuipa Yanga.

Advertisement

Akili ya haraka haraka hapo ni kwamba Yanga itapata faida ya kiasi cha Sh196 milioni katika uhamisho huo wa Makambo ambaye amebakiza mkataba wa mwaka mmoja na Yanga mpaka sasa.

Utagundua jambo moja, Makambo na makali yake yote ya ufungaji aliyoyafanya msimu mmoja, kumbe Yanga ilikuwa makini katika kusajili kwa bei rahisi na umasikini wao.

Hapa maana halisi ni kwamba Yanga ilitumia kiasi kidogo kumsajili Makambo ambaye amewafungia mabao 20 msimu huu kabla ya mechi ya jana ya Mbeya City ukilinganisha na sajili zingine za klabu nyingine kama ule wa Adam Salamba anayetajwa kuigharimu Simba Sh30 milioni na hata Obrey Chirwa wa Azam aliyesajiliwa kwa kiasi kinachotajwa Sh40 milioni akitokea Uarabuni.

Nilichogundua ni badala ya matusi viongozi wa Yanga waliosimamia usajili wa Makambo tu wakiongozwa na mwenyekiti Hussein Nyika walipaswa kupongezwa na sio kutukanwa.

Naungana na Kocha Mwinyi Zahera ambaye wikiendi iliyopita alilazimika kutamka mbele ya Wanayanga viongozi waliopita hawakuwa wabaya lakini walikutana na mambo magumu ya kuhusu ukata mkali wa klabu yao.

Kamati ya usajili ilikuwa kwa kiasi kikubwa ikitumia fedha za mifukoni kusajili na sio nguvu ya fedha za klabu huu ni ugumu mkubwa hasa kupata timu yenye ushindani na bado ikabaki kupambana kupigania ubingwa mbele ya klabu kama Simba ambayo haikuwa inajua maisha mabovu ndani ya msimu mzima.

Waliokuwa wanatukana uongozi wao hapo nyuma sasa ndiyo wanaotamba mtaani kuwa Yanga inauza wachezaji Ulaya hii ni elimu tosha ya kubadilisha akili ya wadau wa soka hapa kwetu hususan mashabiki.

Kuna uwezekano mkubwa bado Yanga ikapata fedha nyingi kupitia wachezaji wake kama Feisal Salum na wengine ambao inaelezwa wana ofa mbalimbali.

Hii ni fursa nyingine kwa klabu kama Yanga yenye halio ngumu kiuchumi kuelewa faoda ya utulivu wa usajili na kusajili vyema unaweza ukatumia nafasi hiyo kupata wachezaji bora ambao badaye wanaweza kuja kuwa chanzo kizuri cha mapato.

Soka sasa ni biasahara kubwa kama ukitulia na kujua kuchukua wachezaji bora na kuwafungulia milango ya kibiashara kwa klabu nyingine.

Yanga sasa inakaribia kuoga fedha kupitia mchezaji ambaye hawakuamini kama atakuja kuwa dhahabu akiletwa kwa majaribio na baadaye kuwa nguzo muhimu.

Sijafunga mjadala wale jamaa zangu tuwasiliane kuelezana ni jinsi gani Yanga ilikuwa inapigwa msimu unaomalizika pengine nitawaelewa njooni na hoja tuzungumze.

Advertisement