KIBADENI: Sio uwanjani tu, hata nje anatisha

Friday March 15 2019

 

By OLIPA ASSA

KATIKA toleo la jana Alhamisi Abdallah Kibadeni ‘King’ alifunguka mambo mengi kuhusu safari yake na soka, lakini akieleza ukweli wa majina yake na dau lililompeleka Simba.

Pia, alifafanua jina la King na Pele na tukio lililomuachia kilema cha maisha na beki aliyemnyima raha uwanjani sambamba na kukitangaza kikosi chake cha muda wote Msimbazi.

Leo anaendelea kutiririka akifichua alivyonufaika akiichezea Simba na pia, kufichua jinsi alivyoangukia mikononi mwa mtoto wa mwanasiasa mkongwe wa zamani aliye marehemu kwa sasa, Rashid Mfaume Kawawa na alivyojaaliwa kupata watoto wanaofanya atembee kifua mbele. Endelea naye!

ANACHOJIVUNIA

Kibadeni anasema soka limemjalia mambo mengi kijamii na hata kiuchumi sambamba na kupata marafiki wengi na pia kufahamika ndani na nje ya nchi.

Hata hivyo, kubwa analojivunia ni kufanikiwa kujenga nyumba Sinza kwa Remmy jijini Dar es Salaam anayoishi na mke wake mkubwa Fatuma aliyezaa naye watoto watatu, Ratifa anayefanya kazi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.

Mtoto wake wa pili ni Omary aliyemaliza Shahada ya Diplomasia na mwingine ni Assimu yupo Uingereza anasomea mambo ya michezo.

Kibadeni anasema kwa miaka tisa aliyoichezea Simba, mwaka 1978 kikosi chao kilikuwa mabingwa wa ligi, kitu kilichowapa dili wachezaji wengi kuchezea soka timu za Falme za Kiarabu, lakini yeye alikatazwa na baba yake mzazi badala yake akajikuta anatua Majimaji ya Songea ikiwa daraja la nne.

MAISHA YA MAJIMAJI

Anasema kocha aliyechukua ubingwa na Simba mwaka 1978 alikuwa Mzungu ambaye alitimuliwa kitu kilichosababisha wachezaji kusambaratika, yeye akaombwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Lawrance Gama ili akapandishe timu ya Majimaji kutoka daraja la nne mpaka Ligi Kuu.

“Nilienda Majimaji kwa heshima ya baba kwa kuwa alikuwa mwanachama wa CCM, basi akaona si mbaya nikawa mzalendo, lakini alikuwa hataki niende nje na alikataa ofa ya Yanga,” anasema.

Anasema alitua Majimaji kwa masharti makubwa, alimtaka RC Gama awasajili wachezaji ambao aliwataka yeye walikuwa ni straika Rajab Mhoza, Khamis Mulumbo (kipa), Hussein Tindwa, Idd Pazi waliomchukua kutoka Timu ya Mkoa ya Mtwara.

“Wakati Simba inajiandaa kucheza Klabu Bingwa ya Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa) ilikuja kumuomba Hussein Tindwa ambaye alifia uwanjani pale Uwanja wa Taifa, katika mechi yao dhidi ya Raccah Rovers ya Nigeria. Lilikuwa tukio la maumivu makali, aligongana na beki wa timu pinzani.

“Lakini kabla ya kuanza kwa majukumu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, alituandalia sherehe ya kututambulisha kwa wachezaji wenyeji, alitupa heshima kwa kutupatia majina ya machifu, utaratibu ulikuwa hivi.

“Aliandika vikaratasi vitano aliweka kwenye chombo, mimi nilikuwa wa kwanza kwenda kuchukua, kukifungua nikakuta jina la Mputa aliyekuwa chifu wa mkoa huo.

CHIMBUKO LA MPUTA

“Baada ya kuchukua kikaratasi kile, Mkuu wa Mkoa aliniambia hawawezi kuniita mpaka nikapate ridhaa ya watoto wake waliokuwa hai, walipigiwa simu, nikaenda mpaka Piramiho katika Kijiji cha Maposeni ambako ndiko familia hiyo ilikuwa ikiishi.

“Nikapokelewa vizuri, wakachinja ng’ombe wakachukua nyongo wakaichuja damu wakaichanganya na vitu vya mila zao, tukanywa mimi na mtoto wake wa kwanza na damu wakatunyunyizia usoni, tangu hapo nikapewa uchifu, watu wakiwa na shida walikuwa wanatumwa kwangu.

“Nikapewa sharti la kuoa mke wa Kingoni, ili kujiunganisha kikamilifu na ukoo ule, waliniambia nichague ninayemtaka nikimpata niwaambie,” anasimulia.

AANGUKIA BINTI WA KAWAWA

Kibadeni anasema mwaka 1978 akiwa ametoka Simba alipewa cheo cha umeneja wa uwanja, mchezaji na chifu.

“Kuna siku kilikuja kikundi cha kinamama ofisini kwangu kutaka uwanja wautumie kwa sherehe zao, wakiwa wanajitambulisha nikasikia jina la Rehema Rashid Kawawa yaani aliyekuwa Makamu wa Rais enzi hizo, nikavuta pumzi na moyo ukatia nukta kwake.

“Walipoondoka ofisini kwangu nilienda kwenye familia ya kina Mputa kutoa taarifa ya kumhitaji binti wa Kawawa, walilifanyia kazi hilo kwenda kwenye familia yake kuwaambia wazazi wake ambao walikubali kwa moyo mmoja.

“Zilifuata taratibu za kwenda kutoa posa kisha tukafunga ndoa, hivyo Majimaji ilinipa heshima ya mke, uchifu na umeneja wa uwanja, nilipomtaarifu mke wangu alifurahi kuona nimekuwa muwazi kuliko ningekuwa nahangaika na wanawake ovyo,” anasema.

Anasema Rehema Kawawa akawa mke wake wa pili na kitaaluma alikuwa mwalimu na anaeleza amebahatika kuzaa naye watoto wawili, Sophia aliyeolewa na Bilal aliyemaliza shahada ya uhusiano wa kimataifa na sasa anafanya kazi JKT.

“Nashukuru Mungu, Wake zangu wanaelewana kwani ni wasomi wa pili Fatuma amestaafu alikuwa mhasibu, nilimuoa mwaka 1980 kutoka Zanzibar,” anasema.

“Wakati Rehema Kawawa nimemuoa mwaka 1986 kutoka Songea ambako nilipewa uchifu, naishi naye Madale ambako baba yake mzazi Kawawa alijenga kwenye kiwanja chetu hivyo siwezi kujisifu kama nyumba yangu licha ya kiwanja kilikuwa chetu na bado kuna maeneo, lakini kwa sasa amesafiri kwenda Ulaya kikazi,” anasema.

Kibadeni anasema mke wake wa kwanza alimuoa mwaka 1968 alikuwa anaitwa Sikitu Idd Mgomba na kuweka wazi kwamba alikuwa mama wa nyumbani, lakini kwa sasa wameachana.

WATOTO 14, WAJUKUU KIBAO

Kibadeni hakutisha yu ndani ya uwanja kwa kufunga mabao, hata nje ya soka alikuwa hajambo, kwani anafichua kuwa ni mmoja ya watu wanaojivunia kujaaliwa watoto wa kutosha.

“Nashukuru Mungu, nimebahatika kupata watoto wa kutosha, kitu ambacho najivunia.”

Anasema kabla ya kumuoa mkewe wa kwanza aliyezaa naye watoto sita, tayari alikuwa ana mtoto wa kwanza aliyejulikana kwa jina la Mohammed na baada ya ndoa hiyo aliwazaa Athuman, Mohamed, Habibu, Idd na Hadija.

“Tabora niliacha mtoto anaitwa Dadaa, lakini pia mwingine nimezika hivi karibuni alikuwa anaitwa Siwa, hivyo nina jumla ya watoto 14 , huku kwa idadi ya wajukuu wala hata sijui kwa kweli,” anasema.

Kibadeni amefichua siri yake ya baba yake Mbwana Samatta na pia kuanika vitega uchumi vyake anavyomiliki kwa sasa mbali na mijengo aliyoitaja hapo juu. Kadhalika amefichua utani wa jadi wa Simba na Yanga na mambo yalivyo sasa. Unajua kazungumzaje? Ungana naye kesho Jumamosi.

Advertisement