Tunahitaji nini kwa Amunike?

Emannuel Amunike amewekwa kikaangoni na kundi kubwa la wadau na mashabiki wa soka nchini ambao wamekuwa wakikosoa uteuzi alioufanya wa kikosi cha nyota 25 wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.

Kuna wanamhoji kwa nini amemuacha beki wa kimataifa wa Tanzania anayecheza soka la kulipwa Afrika Kusini kwenye klabu ya Baroka inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo.

Kuna wanaomshangaa na kumlaumu kwa nini hakulijumuisha jina la kiungo mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu wakitumia kigezo kuwa ndiye mchezaji aliyepiga idadi kubwa ya pasi za mabao msimu huu na hadi sasa amefanya hivyo mara 15.

Wengine wameshangazwa na kitendo cha kumwacha kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ wakidai Stars itakosa ubunifu katika safu yake ya ushambuliaji kisa haitokuwa na mpishi wa kutengeneza nafasi kwa washambuliaji wake.

Kila mtu amekuwa akisema lake juu ya uteuzi huo lakini kimsingi maoni ya wengi yamekuwa yakikosoa uamuzi wa Amunike kuwaita au kuwaacha baadhi ya wachezaji katika kikosi cha Stars kitakachocheza mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), baadaye mwezi Juni huko Misri. Hata hivyo, ukitazama maoni na maswali ya wengi juu ya kile ambacho Amunike amekifanya kisha ukatafakari kwa umakini, utabaini yanatolewa kwa mtazamo usio wa kiufundi yakichagizwa na ushabiki wa mtu kwa mchezaji husika ambaye hajapewa nafasi ya kuwemo kikosini.

Wanaomkosoa Amunike wanashindwa kufahamu kwamba kuna sababu mbalimbali zinazopelekea mchezaji kupata nafasi kwenye kikosi cha timu ya taifa na haimaanishi kwamba ukiwa unatimiza kigezo kimoja basi ni lazima uitwe hata kama hutimizi vingine.

Mchezaji anaweza kuwa ni mzuri lakini akawa hana nidhamu au namna ya uchezaji wake haiendani na mbinu ambazo kocha anataka kuzitumia kwenye mchezo husika au staili yake haiwezi kusaidia timu kuwakabili wapinzani kwenye mechi iliyo mbele.

Mechi dhidi ya Uganda inahitaji zaidi wachezaji ambao wana nidhamu ya mbinu, wanaoweza kufanyia kazi vyema kile watakachoelekezwa na benchi la ufundi badala ya wale ambao watacheza ili kufurahisha majukwaa.

Ni mechi ambayo haiitaji wachezaji wanaoonekana kuwa wazuri pindi timu inapokuwa na mpira lakini pale inapoupoteza wanageuka mzigo kwa wenzao jambo linaloweza kuigharimu timu.

Pia wanaokosoa kitendo cha kuitwa kwa baadhi ya wachezaji wa kigeni wakidai hawakupaswa kuwemo kwenye uteuzi kwa madai hawapati nafasi ya kucheza kwenye klabu zao na bora waitwe wachezaji wanaofanya vizuri kwenye ligi ya nyumbani, wanasahau bado ligi yetu haijawa na ubora kiasi hicho cha kuweza kulinganisha na ligi pamoja na mazingira ambayo hao wanaocheza soka la kulipwa wanatoka.

Pamoja na hilo, inavyoonekana hao wanaokosoa hawajawafuatilia kwa umakini nyota hao wanaocheza soka la kulipwa ili kujiridhisha madai yao wanaitwa huku wakiwa hawachezi ni sahihi au sio sahihi. Mfano wengi wamekuwa wakidanganya Farid Musa na Shaban Chilunda hawapati nafasi ya kucheza kwenye klabu zao ambazo ni Mezalla pamoja na CD Tenerife B.

Lakini katika hali ya kushangaza, kwenye mechi saba za mwisho kabla ya kuitwa Stars, Chilunda ameichezea Mezalla katika mechi nne wakati katika mechi tano za mwisho za CD Tenerife B, Farid Musa amecheza mechi nne na kati ya hizo, tatu alianza kwenye kikosi cha kwanza. Nguvu kubwa tunayotumia kukosoa na kupinga uteuzi wa kikosi cha Stars uliofanywa na Amunike, inatufanya tusahau nini ambacho Tanzania inakitaka kwake yeye akiwa Kocha Mkuu wa Taifa Stars katika kipindi hiki.

Kiu ya kufuzu AFCON kwa mara ya kwanza baada ya miaka takribani 39, inaonekana inaanza kufunikwa na tamaa yetu ya kutaka kuona mchezaji fulani anakuwepo kikosini au hatokuwepo pasipo kumpa nafasi na uhuru kocha kutumia wale wachezaji anaowahitaji.

Ni vyema tumwache Amunike afanye kile anachoona ni sahihi kwa sasa kwa sababu mwishowe hakuajiriwa awe kocha wa timu ya taifa ili awafurahishe mashabiki na wadau wa soka kwa kuita wachezaji wanaowapenda. Tunachotakiwa kufanya ni kumdai Amunike nafasi ya kushiriki AFCON mwaka huu pasipo kuangalia amemwita nani au nani hajamjumuisha kikosini kwani sio lengo letu kuu kwa sasa.

Inavyoonekana wengi wetu hadi sasa hatujui nini tunachokihitaji kati ya kufuzu AFCON au Amunike kuwaita wachezaji tunaowataka.

Inanikumbusha hadithi ya mapinduzi ya viwanda kule Uingereza. Hasira za vibarua zilipelekea waharibu mashine viwandani wakiamini ni chanzo cha wao kupoteza ajira wakati adui yao halisi alikuwa ni binadamu aliyezitengeneza na kuamuru zitumike.