Kilichotokea kwa makocha waliorudi kuinoa real Madrid

Friday March 15 2019

 

MADRID, HISPANIA,

WIKI chache zilizopita, kulikuwa na stori za kuwahusisha makocha wawili Jose Mourinho na Zinedine Zidane kurudi kwenye timu waliowahi kuinoa ya Real Madrid.

Huko na huko, hatimaye Real Madrid imetangaza kumrudisha Zidane kwenye benchi la ufundi la timu hiyo baada ya kuona mambo yao yanakwenda kombo chini ya Kocha Santiago Solari.

Zidane amerudi Real Madrid ikiwa haizidi hata miezi 10 tangu alipoachia ngazi mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kuwapa mataji matatu mfululizo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hata hivyo, Zidane hatakuwa kocha wa kwanza kuinoa Real Madrid katika awamu zaidi ya moja baada ya kuwapo na makocha wengine kibao wakiwamo hawa watano maarufu kabisa.

Cheki walichofanya matokeo hao baada ya kurudi kuifundisha Real Madrid kama alivyofanya Zidane hivi karibuni.

Alfredo Di Stefano

Awamu ya kwanza: 1982-1984

Amerudi: 1990-91

Gwiji wa Real Madrid, Alfredo Di Stefano alianza kukinoa kikosi hicho cha Los Blancos kati ya mwaka 1982 na 1984, akishinda mechi 63 kati ya 108, huku akishuhudia vichapo katika mechi kadhaa za makombe na timu ikimaliza nafasi ya tatu katika msimu wa La Liga katika msimu wa 1982/83.

Di Stefano alirejea Real Madrid mwishoni mwa mwaka 1990, kwa kipindi kifupi na kusaidia timu hiyo kubeba ubingwa wa SuperCopa de Espana, ikiichapa Barcelona katika mechi zote mbili kabla ya kuachana na wababe hao wa Bernabeu Machi 1991.

John Toshack

Awamu ya kwanza:

1989-90

Amerudi: 1999

Baada ya miaka minne ya kuwa kocha huko Real Sociedad, John Toshack alibamba kibarua cha kwenda kuinoa Real Madrid, ambao walikuwa wakiingia kwenye msimu wa 1989/90 walipotokea kubeba ubingwa wao wanne wa La Liga . Katika msimu wake wa kwanza Los Blancos, Toshack akaongeza taji la tano mfululizo, lakini mambo yalikuwa mazito kwenye msimu wake wa pili ambapo na hapo ndio ukawa mwisho wake. Kocha huyo raia wa Wales alirudi huko Madrid mwaka 1999 baada ya kufutwa kazi kwa Guus Hiddink, akitokea Besiktas. Lakini, mambo hayakuwa mazuri kabisa kwa Toshack katika awamu yake ya pili kwenye kikosi hicho na hata mwaka hajamaliza alifutwa kazi kutokana na kuwakosoa wachezaji wake hadharani huku akiwa ametibuana na Bodi ya Real Madrid.

Vicente del Bosque

Awamu ya kwanza: 1994

Amerudi: 1996, 1999-2003

Kocha Vicente del Bosque awamu zake mbili za kwanza alizokwenda kuinoa Real Madrid alikuwa kocha wa muda. Kipindi cha kwanza ilikuwa mwaka 1994, kisha alirudi tena Santiago Bernabeu mwaka 1996.

Kikafika kipindi cha Mhispaniola huyo kuingia kwenye timu hiyo akiwa kocha wa kudumu, ambapo aliisimamia timu hiyo kati ya mwaka 1999 na 2003, alipokuja kuchukua mikoba ya kumrithi John Toshack. Katika kipindi hicho, Del Bosque alipata mafanikio makubwa akibeba mataji mawili ya ligi, Spanish Super Cup mara moja, Ligi ya Mabingwa Ulaya mara mbili, Super Cup na Intercontinental Cup, akiwa nna kikosi matata kabisa cha Galacticos.

Jose Antonio Camacho

Awamu ya kwanza: 1998

Amerudi: 2004

Jose Antonio Camacho hakika atakuwa mmoja wa makocha ambao hawatahitaji kuwa na kumbukumbu nzuri katika yake huko kwenye kikosi cha Real Madrid, ambapo nyakati zake kwenye timu hizo zilikomea ndani ya miezi tu, hata mwaka hajamaliza akiondolewa kwa kutibuana na uongozi akiwa hajafundisha hata mechi moja. Hata aliporudi tena klabuni hapo mwaka 2004, mambo hayakuwa mazuri pia. Katika awamu yake ya pili aliporudi kwenye kikosi hicho, alichukua mikoba ya Carlos Queiroz. Camacho aliisimamia timu hiyo kwenye mechi sita tu, akaachia ngazi baada ya timu kuanza vibaya msimu wa 2004/05.

Fabio Capello

Awamu ya kwanza: 1996-1997

Amerudi: 2006-2007

Kabla ya Zidane, huyu ndiye kocha wa miaka ya karibuni kurudi kuinoa Real Madrid. Fabio Capello, alianza kuinoa Los Blancos mwaka 1996 na kukaa kwa msimu mmoja tu, ambapo alishinda taji la La Liga. Mambo yake yalitibuka baada ya kutibuana na aliyekuwa mwenyekiti wa kipindi hicho, Lorenzo Sanz pamoja na mashabiki kutokana na alivyokuwa akimtumia straika Raul. Capello alirudi Madrid miaka 10 baadaye akiwa na malengo ya kumaliza ukame wa mataji kwenye kikosi hicho. Alianza msimu kwa kasi hafifu sana kabla ya mambo kuchanganya na kubeba taji jingine la La Liga. Hata hivyo, alifutwa tena kazi baada ya mwaka mmoja tu kutokana na kutibuana na bodi ambao hawakuwa wakipendezwa na soka lake la kujilinda alilokuwa akifundisha kwenye timu hiyo.

Advertisement