Wema: Niacheni na mifupa yangu!

Sunday September 20 2020

 

By NASRA ABDALLAH

WAKATI wanaa wakiendelea kumuandama kutokana na mwonekano wake, mrembo Wema Sepetu amevunja ukimya na kuwataka watu hao wamuache na mwili wake wa kimbaumbau kwa vile mwenyewe ameridhika nao.

Wema ana zaidi ya mwaka sasa tangu awe katika mwonekano mpya wa mwili wake huo, ambapo kila leo amekuwa akiambulia vijembe kutoka kwa watu wa mitandaoni kuhusu kujibadilisha kwake huko.

Moja ya sababu ya msanii huyo kujikondesha alieleza ni kutokana na tatizo lake la kutoshika ujauzito na kubainisha kuwa wataalam wa afya walimshauri apunguze mwili ambao ulikuwa umeshafika kilo 109.

Akihojiwa na mtandao wa Dizzimonline, uliotaka kujua namna anavyochukulia watu wanavyosema kuhusu mwili wake alisema: “Hao wanaozungumzia vibaya mwonekano wangu wa sasa hawanisumbui, ilimradi nilichokifanya nimeridhika nacho na inatosha, waniache tu na mifupa yangu.” Kisha supastaa huyo anayeigiza pia filamu aliongeza kwa kusema: “Hivi huoni namna ninavyonoga hata kwenye tamthiliya ya Karma kutokana na mwili wangu huu wa sasa.”

 

Advertisement