P Funk: Singeli inakuja inakataa, ile kasi mh!

PRODYUZA mkongwe wa muziki wa kizazi kipya, Paul Matthysse a.k.a P-Funk Majani amesema muziki wa singeli una nafasi ya kuwa nembo ya muziki wa Tanzania kama tu itawezekana kuimbwa taratibu.

Majani alisema hayo kupitia mahojiano na Mwanaspoti na kufafanua kitu pekee kinachounyima nguvu muziki huo ni hali ya kwamba hauimbiki taratibu, kwa sababu kitaalamu ili muziki uweze kuwa nembo ni lazima uweze kuimbwa kwa namna mbili tofauti, kwa haraka au kwa kubembeleza.

“Sikiliza miziki mingine yote, inaweza kuimbwa kwa aina mbili. Kwa mfano, kuna taarab zinazoimbwa kwa kasi na zipo zinazoimbwa taratibu, Hip Hop hivyo hivyo, lakini singeli ni mbio tu mwanzo mwisho, inaunyima sifa kuwa muziki wa kutubeba,” alisema.

Aliongeza kwamba kama vijana wanaofanya muziki huo wataongeza ubunifu na kutengeneza singeli ya taratibu muziki huo unaweza kuvuka boda kwa urahisi kwa sababu ndiyo muziki ambao umechota vitu vingi kutoka ndani ya nchi kuliko miziki mingine.

Kwa sasa P Funk amejikita zaidi kwenye usimamizi wa lebo yake ya Bongo Records ambayo ina jumla ya wasanii wawili wa kurap, Rapcha na Lil Dwin.