THE TRENDSETTER : Nikisema Diamond sio tena mwanamuziki utanielewa?

Wednesday November 13 2019

DIAMOND-MANAMUZIKI-WASAFI-WASAFI FESTIVAL-TAMASHA-WASANII-BURUDANI-KIJITONYAMA-

 

By Luqman Maloto

MBILI sifuri sifuri kenda (2009), aliamua kutugeuza njiwa. Bi mkubwa Patricia Hillary, yeye alimtuma njiwa” apeleke salamu, ila yeye akatutuma sisi, eti tukamwambie jinsi ambavyo bado anampenda. Huko sio kutugeuza njiwa?

Wabongo wakaona kijana analeta dharau. Anatokaje Tandale kwao huko halafu anaibuka bila hata salamu na kuwatuma wakubwa zake? Hakuna aliyekwenda kumwambia.

Kikafuata kilio. Bwa’mdogo akatupeleka Mbagala na machozi. Eti kisa tuligoma kwenda kumwambia kipenda roho wake, ndio akapigwa kibuti kwa sababu kwao Mbagala.

Hili tusiliache likapita. Kwani wanaoishi Mbagala hawana wapenzi? Mbona Mbagala majanki wanang’oa kiurahisi na maisha ni poa? Wanapendwa na wanaoa. Wapo wanagonga ‘mathna’, mtaala. Wake wawili na kuendelea.

Dogo alizingua kwa vitabia vyake, alipopigwa chini akasingizia Mbagala. Aache zake! Hatuishii hapo, baada ya kujiliza sana, mrembo Hawa akamhurumia. Wakazaa mpaka watoto. Unadhani alitulia? Akaondoka zake akimzuga Hawa kuwa angerejea!

Kwani alirejea? Si mpaka Hawa akaumwa, ndio akampeleka India kutibiwa? Maskini Hawa, kumbe kipindi chote alipokuwa anangoja marejeo ya baba watoto wake, alipitia madhila mengi hadi “Akamiss Kucheka”.

Advertisement

Mpaka hapo kuna usichojua mwana? Tupo mezani na Nasibu Abdul Juma ‘Diamond Platnumz’. Safari yake ya dude kwa dude, back to back, ina simulizi yenye vionjo vyenye kuhamasisha mno kujituma kusaka mafanikio.

Kujiliza mapenzi ndio zake, lakini ndivyo huzidi kutoboa. Mara ajifanye ana “Mawazo”, halafu akatutishia “anataka kulewa.” Kadiri anavyojiliza, na milango ya Benjamins inazidi kufunguka.

Ni safari baada ya safari, akachora ramani kimataifa. Akaongeza thamani ya Kiswahili. Akawafanya Wanigeria waimbe Kiswahili, Davido akatuletea njaa zake za kutamani ugali wa muhogo, baada ya kupata ubaridi kidogo. Sijui huo ugali anakula na mboga gani? Au alidhani ubaridi kidogo ni aina ya mboga? Ni wimbo “Number One”.

Kama kauli mbiu ya ile kitu ambayo asili yake ni Tanzania, kwamba moja huanzisha nyingine, Diamond akakifanya Kiswahili kizungumzwe Marekani. Mshindi wa Tuzo za Grammy, Ne’Yo akalia mahaba: “Nipo mzima kwa sababu ya wewe tu”.

Kiswahili ‘mbofuu’, ila hatukumcheka, sanasana tumempenda mno kwa kusaidia kukuza Kiswahili chetu. Ingekuwa Mbongo ametobanga Kiingereza, mbona angekoma? Anyways, Ne’Yo alikipa hadhi Kiswahili alipokuwa anamsaidia Diamond kuoa, wimbo “Marry You”.

Diamond hashindwi aisee! Akamfanya brotherman kutoka Inglewood, California, Omarion aimbe Kiswazi: “Penzi twalipamba ngonjera, huba kama Tanga Segera, kwa viuno vya baikoko kutoka Manzabay. Picha twazitwanga kisela, post Insta wanga kuwakera, baada ya chali kimoko.”

Diamond anakuza Kiswahili na sanaa yake imewezesha kina Ne’Yo, Omarion, Davido, Iyanya na wengine kuongea Kiswazi japo cha kutandika kwenye nyimbo.

KILICHOTULETA SASA

Safari ya Diamond kwenye muziki imekuwa peeevu sana. Lini Tanzania iliwahi kuwa tishio Afrika? Mtoto wa Mama Nasibu na vimilonjo vyake, ameweza kuiweka nchi kwenye ramani ya dunia kimuziki.

Leo hii ukitafuta chaneli ya YouTube ya mwanamuziki Afrika yenye wateja (subscribers) wengi zaidi, unamkuta Diamond Platnumz. Watu zaidi ya milioni 2.6 wame-subscribe kwa Underground King wa Tandale.

Davido anafuata akiwa na subscribers milioni 1.9. Miaka mitano iliyopita, nani angedhani Diamond angefika katika ukubwa alionao? Miaka 10 iliyopita, mtabiri gani angetabiri kuwa msanii wa Bongo angewafungisha tela wengine wote Afrika?

Diamond ana subscribers wengi YouTube kuliko Koffi Olomide, Fally Ipupa, P Square na wengine wote Afrika. Nani angeufikiria msuli huo wa Diamond kipindi akiwa mchovu, akichukua tuzo tatu kwa mkupuo, Diamond Jubelee Hall mwaka 2010? Hakuna na hakuwepo. Tusitaniane!

Ni uchawi kufikiri subscribers milioni 2.6 wa Diamond wote ni Watanzania. Ni ushirikina kudhani Tanzania inaweza kuizidi Nigeria kwa mtaji wa watu.

Tanzania haiingii kwa Nigeria hata mara tatu. Kwa watu milioni 52 wanaokadiriwa kuwepo Tanzania, utalinganishaje na Nigeria yenye watu zaidi ya milioni 190 na inaitafuta milioni 200?

Ni hekima kama sio thawabu kukubali kuwa Diamond amefanikiwa kujitangaza vizuri kimataifa na mafanikio hayo yanamfanya ajimwambafai YouTube. Mafanikio hayo yanamfanya Diamond kuwa mwanamuziki mwenye mtaji mkubwa wa watazamaji wa video zake YouTube kuliko mwingine yeyote. Kila anapotoa video, ana uhakika wa watazamaji milioni 2.6. Fikiria kati ya hao kila mmoja akitazama mara tatu.

Waza katika hao subscribers kila mmoja akawapa ujumbe wenzake watatu, kisha nao wakatazama mara tatu-tatu. Ongeza na mtandao mkubwa wa masoko ya muziki wake, alioueneza kote Afrika na duniani.

Matunda hayo ndio yanamfanya Diamond leo kila video yake inapotoka, ndani ya chini ya saa 24 iwe imetazamwa zaidi ya mara milioni moja. Au milioni mbili chini ya saa 48.

Na kwa mwendo huo, nini cha kushangaza kuona leo wastani wa video zake kutazamwa YouTube ni mara milioni 40? Yupo vizuri, japo alitupiga ‘saundi’ kuwa alitemwa na demu wake kisa alikuwa anaishi Mbagala. Ukizingua lazima uachie bomba, uwe wa Masaki hata Oysterbaby. Asiichafue Mbagala yetu!

TUMPE TUZO YAKE

Ladies and gentlemen, hakuna wakati mwingine mzuri kuliko huu, kutambua athari kubwa ya kimuziki ambayo Diamond ameileta na kusababisha yeye ndiye awe mwamuzi wa fasheni za nyimbo zenye kutamba Tanzania.

Akitaka nchi iimbe Jibebe inakuwa, akiamua ikanyage basi kinachofuata ni Kanyaga. Alivyo hana adabu, anawafanya mpaka mashabiki wa Yanga waimbe Simba Baba Lao. Sikumpenda alipoimba Nyegezi na Rayvanny, alitumia vibaya msuli wake kimuziki, kuifanya nchi iimbe wimbo usio na maadili.

Diamond sio tena aina ya mwananuziki ambaye anaweza kupotezwa kwa kubaniwa redioni na runingani. Ana nguvu kubwa kwenye mitandao ya kijamii. Followers milioni 8.2 Instagram. Facebook ina watu zaidi ya milioni 2.8. Twitter anao 738 elfu. Usisahau subscribers milioni 2.6 YouTube. Kwa mtaji huo mkubwa wa watu, unaweza vipi kumfanya Diamond aachie bomba kwenye muziki? Labda aamue mwenyewe. Tena awe mjinga kweli. Ni kwa msuli huo, ndio maana Diamond amekuwa akizifanya ngoma zibambe, hata zile ambazo zingefanywa na wengine zingebaki kichekesho. Ni kwa sababu Diamond sio tena mwanamuziki, bali mwamua uelekeo wa muziki (musical trendsetter) Tanzania. Mabibi na mabwana, tuzo ninayompa Diamond ni The Trendsetter of Music Tanzania. Anawaimbisha na kuwachezesha atakavyo!

Advertisement