NO AGENDA: Maisha ya Ngwair alijiona New York akiwa Bongoland

NAKUPA homework; nitajie wimbo wa Ngwair akilia kuteswa na mapenzi. Nioneshe ngoma ya Albert Mangweha, akilalamika maisha yamempiga mpaka akakata tamaa. Ukipata, nitakwenda Kihonda, Morogoro, nikalale mwezi mzima juu ya kaburi lake.

Ngwair alifanya muziki wa maono yake. Alijiona katika jukwaa la kidunia, akiishi maisha ya kisupastaa. Pesa haikuwepo mfukoni lakini aliziona zikiingia kwenye akaunti zake halafu angezitumia bila uangalifu wala tahadhari, maana ni nyingi.

Hata alipousema ugumu wa maisha, aliujadili kama hali ya mpito, kwamba angebadili na kunyoosha mambo. Msikilize katika “Msela”, ambao aliupiga shambulizi la pamoja na wana TMK, Sir Nature na KR Mullah, anayasema maisha ya ghetto katika sura chanya. Kwamba anatafuta kesho iwe poa.

Mpate kwenye “Dakika Moja”, humo ndani anamlilia demu, si kwamba katendwa au kapigwa kibuti, la! Ngwair anatongoza. Tena mtoto anamtongozea kiwanja. Anamuuliza mtoto jina lake, kinywaji anachotumie ili wapate muda wa japo dakika moja amweleze anavyompenda.

Ni ile kiume. Mwanaume akimtaka mwanamke na akili ikimtuma kuwa akijinyenyekeza ndio atampata, anaweza kujishusha utadhani Petro mbele ya Yesu. Akimpa kisogo anabadilika mpaka jogoo awike mara tatu ndipo atakumbuka. Hivyo, Dakika Moja Ngwair alilia kutongoza, sio mateso ya mapenzi.

Mcheki Ngwair original; picha linaanza na “Ghetto Langu”, mkwaju wa mwaka 2003 uliofanzwa kiufundi na Mdachi genius wa Bongo Records, P Funk. Humo ndani Ngwair anajikuta yupo Harlem, New York kwenye ghetto la brotherman Mase.

Ngwair anarap kuwa ghetto lake linanukia airfresh utadhani nyumbani kwa Mase. Msikilize pia Ngwair anavyofloo, utamuona Mase akiwa Bad Boy Records kwenye mitambo ya tajiri P Diddy, ghorofa ya 16 ya mjengo wa 1440 Broadway, New York.

Ngoma ya pili “Napokea Simu”, unamsikia Ngwair akitamba jinsi simu yake ilivyo busy, akipigiwa sana simu na mademu, mapromota na prodyuza wake P Funk. Unayaona yaleyale maisha ya kisupastaa. Ngwair aliota maisha makubwa.

Tuuendee mzigo wa mizigo katika mizigo yote ya Bongo Fleva, “Mikasi”. Ngwair anayazungumza maisha yake ya kuanzia asubuhi mpaka alfajiri inayofuata. Ni raha tu. Misosi, mitungi, sigara, kisha makaburini kula kuku moshi (kijiti), kisha viwanja kusaka wanawake.

Shida haukuwa msamiati ndani ya kichwa cha Ngwair. Asubuhi aamke, apige mswaki, aoge, atupie viwalo mwilini, ajipulizie manukato anukie vizuri, halafu apitie wahuni wenzake wakakae baa. Wapige supu na chapati, wavute sigara, wanywe pombe, mchana wale ugali mkubwa na samaki, baada ya hapo wakavute bangi. Kisha maneno viwanja kukamilisha siku na watoto wa kike.

Ikae Mikasi, isogelee “CNN”, utaipata ladha ya Ngwair akijiona 50 Cent, tena maskani yake South Jamaica, Queens, New York. Floo kama Curtis Jackson, vile sauti yake inayotokea kwenye mdundo, vinanda na mixing za Dr Dre, katika studio za Aftermath, Colorado Avenue, Santa Monica, California.

Ngwair wa CNN, anatamba ana pesa zimejaa mfukoni kuliko ATM, yupo juu zaidi ya KLM na anakesha akila bata kama televisheni ya CNN inavyokesha ikirusha matangazo. Anawaza shida zenu za Kibongo huyo?

Achana na topic ya “She Got a Gwan”, ni kawaida mwanamuziki wa kiume kumsifia mwanamke. Ipotezee “Mademu Wangu”, maana humo ndani Ngwair alitaka tu kutuonesha umahiri wake wa kujua sifa za warembo wa Kitanzania kutokana na makabila yao. Ikamate “Nipe Dili”, uone vile mwana Chemba Squad, alivyowaza kupiga dili apate mkwanja, awe tajiri, aponde raha.

Kwenye mawazo, Ngwair hakuwa mvivu. Ndio sababu aliandika nyimbo nyingi na kurekodi kwa imani kuwa muziki ungempa pesa nyingi za kumuwezesha kuishi maisha aliyoyataka. Bahati mbaya biashara ya muziki Bongo si kama Marekani. Wala soko la Dar si la New York.

Muziki haukumpa Ngwair maisha aliyoyatamani. Wakati Ngwair alipofariki dunia Mei 28, 2013, ilikuwa miaka 10 tangu alipotoa Ghetto Langu. Hakuwa na ghetto kama la Mase. Hakuna madili aliyofanya kumuingizia pesa za kutosha. Alipigika na kuishi kwa kuungaunga.

Kama swali ni kwa nini Ngwair alikufa mapema? Jibu ni Watanzania. Aliwahudumia muziki mzuri lakini wao hawakumlipa malipo mazuri. Akaangaika huku na huko kutafuta pesa. Kifo kikamkuta ugenini, Afrika Kusini.

Ngwair, alifanya muziki na kuwasilisha hisia halisi za kigangster. Kumiliki pesa. Kutumia wanawake. Kufanya starehe zenye tambo nyingi kwa jeuri ya pesa, kampani, ulinzi wa watu na bunduki. Hayo ndio maisha ya gangsters, wajukuu wa babu George Washington.

Pamoja na hivyo, Ngwair alikuwa mtetezi na mwenye kuwahamasisha wanawake kujikubali, kujiamini na kuamka kujitetea. Ngwair hakutaka mwanamke awe mnyonge. Aishi kwa kutegemea wanaume. Ipate “Sikiliza” ambayo aliwaalika FA na Lady Jaydee.

Ngwair alitaka mwanamke ajitambue kuwa anaweza kufanya chochote na kuwa yeyote. Hata rais akitaka. Akauliza, kama ni vigezo, wanaume wanavipata wapi mpaka wanawake wavikose? Ngwair hakuamini kama kuna ambacho mwanaume anaweza halafu mwanamke asiweze.

Ngwair alikuwa mkweli sana; kwa vile yeye aliimba sana starehe na kutumia wanawake, hakuacha kuwazindua wanawake kwamba alipokwenda viwanja, japo awe na pesa, vinywaji, muziki mzuri na lundo la marafiki, lakini kama hakuna wanawake hilo eneo huona halilipi.

Ni ujumbe kuwa wanawake ndio hukamilisha furaha na starehe za wanaume. Wanawake huifanya dunia iwe tamu kama ilivyo. Ngwair aliamini kuwa wanawake wakitambua thamani na umuhimu wao, halafu wakaishi kulingana na umuhimu na thamani yao, wanaume wangewanyekea sana.

Tuinenee pia “Mapenzi Gani”, Ngwair akisaidiwa na Jaydee kwenye chorus, aliongea na binti mrembo anayefujwa na kugeuka hazina iliyofichwa. Ameolewa na mwanaume mwenye pesa, lakini anateseka. Mwanaume ana wanawake wengi, anampiga kila mara.

Ngwair anamtaka huyo binti mrembo kutambua kuwa hayo sio mapenzi. Bora ajiamini, afanye uamuzi, ikibidi awe binti komando, kwani mapenzi sio pesa wala nyumba nzuri. Ngwair alitaka wanawake wawe huru katika kuchagua maisha yao yenye furaha bila kuwa tegemezi.

Huyo ndiye Ngwair. Alitekwa na fikra za kigangster, akataka aishi kama New York akiwa ndani ya ardhi ya Bongo. Mpenda starehe, mtetezi wa usawa na haki za wanawake. Alhamisi iliyopita alitimiza miaka saba kaburini.

Endelea kupumzika The Freestyle King.