Martha : Hiki ndicho Tinoco ninachomfanyia

Saturday November 30 2019

Martha-Tinoco -ninachomfanyia-Kagera Sugar- Benedict -Tinoco-mrembo-nidhamu-mwanaspotiSoka-burudani-

 

By Olipa Assa

HAWAKUKOSEA waliosema nyuma ya mafanikio ya mwanaume kuna nguvu ya mwanamke hawakukosea. Ile nidhamu, heshima na kujituma kwa kipa wa Kagera Sugar, Benedict Tinoco kuna mrembo anayefanya mambo yaende. Huyu si mwingine, bali ni Matha Robert.

Matha ndiye mke wa Tinoco ambaye ametoka kujifungua hivi karibuni mtoto wa kike. Mwanamama huyo anafichua namna anavyomuweka sawa mumewe kumtofautisha na wachezaji wengine.

Jambo kubwa analomjenga ni kuwa na nidhamu anayoamini kuwa chanzo cha mafanikio ya kuwa kipa bora.

Katika mahojiano na Mwanaspoti, Matha anasema: “Kuna umri unafikia lazima baadhi ya mambo aachane nayo kabisa, anatazamwa kwa upana, mfano wazazi wangu lazima waone nidhamu yake iwe uwanjani ama nyumbani.”

“Kati ya vitu ambavyo sivipendi ni kumuona anafanya fujo za kupigana uwanjani, hivyo nakuwa namsisitiza kuhakikisha anakuwa mfano wa kuigwa kwani kwa sasa ana wakwe na tayari tuna mtoto ambaye akija kukua atahitaji kuona mfano mwema wa wazazi wake.”

WALIKUTANA DUKANI

Advertisement

Safari yao ilianza mwaka 2017, Matha alipokuwa anauza duka la vifaa vya umeme na Tinoco alikuwa mteja wake.

Tinoco alivutiwa na mrembo huyo, akamwaga sera zilizoeleweka masikioni mwa Matha, kisha wakaanza mahusiano mpaka kufikia kuishi pamoja.

“Alikuwa mteja wangu mkubwa, akaamua kuua ndege wawili kwa jiwe moja, baada ya kununua kwa muda mrefu vifaa akaamua kunifungukia na mimi nilimpenda, tukaanza safari ya mapenzi hapo.”

SAPOTI YAKE

Anasema anamkosoa pindi anapoona anafanya hovyo uwanjani na kumsimamia kufanya mazoezi ya kumuweka fiti hasa anapokuwa mapumziko. “Nahakikisha naisimamia ratiba yake ya mazoezi vyema anapokuwa nyumbani, naangalia ni vyakula gani vya kumjenga kama mchezaji, najua soka ndio kazi inayofanya anitunze na itasomesha watoto wetu.”

KIWANGO CHA CASSILLAS

Martha anatamani kuona mume wake anafikia kiwango cha ubora wa kipa wa zamani wa Real Madrid, Iker Cassillas na humwambia kijanja ili asijisikie vibaya.

“Tukikaa pamoja kuboresha kazi yake maana anakuwa ananiuliza mke wangu unadhani kitu gani niongeze ili niwe bora, huwa natumia hekima na upendo kumwambia nataka afike wapi,” anasema.

“Kuna wakati namfungulia video za Cassillas kisha namwambia mume wangu natamani siku moja nikuone kwenye kiwango hiki, huwa ananisikiliza na kuyafanyia kazi.”

ANAMTULIZA HIVI

Anasema anatambua kwamba changamoto za mpira zipo nyingi, ikitokea mumewe amevurugwa jambo la kwanza anapiga goti kumuombea ili Mungu ampe amani ya moyo kisha anamshauri kwa busara kuchukulia kama mapito ya muda mfupi. “Silaha kubwa huwa namuombea sana kwa Mungu kwa sababu nampenda sana mume wangu, iwe anaingia kucheza nasali afanikiwe, akivurugwa nasali ili Mungu ampe amani, akifanya vyema huwa namshukuru Mungu pia,” anasema.

MUME WA AINA

GANI KWAKE

Martha annamshukuru Mungu kumpa mume anayemtengenezea furaha, huku akimuona kama aliyeletewa kwa muujiza kutokana na ucheshi na anavyojali na kumthamini. “Mungu kanipendelea kwa hili eneo, sijawahi kujuta wala kumchoka, mcheshi, tunataniana kuna wakati natamani dunia iwe yetu peke yetu, ana upendo wa ajabu kiukweli najisikia fahari kuwa mke wa Tinoco,” anasema.

Advertisement