Lulu Diva : Diamond? subirini ndoa

Friday December 20 2019

Lulu Diva - Diamond- subirini ndoa-Bongofleva-Lulu ‘Diva’ Abbas-supastaa wa muziki-Diamond Platnumz -

 

By Rhobi Chacha

UKARIBU wa nyota wa Bongofleva, Lulu ‘Diva’ Abbas na supastaa wa muziki huo, Diamond Platnumz hauwezi kumuacha salama kimwana huyo mrembo.

‘Lulu Diva’ katika siku za karibuni ameonekana kuwa na ukaribu wa hadharani na Diamondi ambao haukuwapo siku za nyuma na maswali kibao yakafuata nyuma ya wawili hao.

Katika dunia ya Insta ambayo kila mtu anasema lake, wawili hao wamehusishwa kimapenzi .

Jambo hilo limemfanya Lulu Diva kufunguka: “Subirini ndoa yangu” huku akisema siku akiolewa watu hawatajua kwani amegundua watu wengi wana husda.

Lulu Diva alisema anaamini kuwa si kila mtu ana mapenzi ya dhati kwake hivyo atafunga ndoa ya kimyakimya kwanza na sherehe itafuata baadaye.
“Siku hizi wanga wengi watu watashtukia nimeshafunga ndoa sherehe baadaye kwa wale ndugu na marafiki maana najua siyo wote wanaopenda jambo hili litimie,” alisema Lulu Diva 

Hata hivyo, Lulu Diva ambaye kwa sasa anatamba na wimbo unaoitwa ‘Mapopo’, alikataa kumtaja mwanaume aliye naye sasa.

Advertisement

Kimwana huyo ambaye pia alivuma na nyimbo kama ‘Utamu’, ‘Ona’, ‘Amezoea’, ‘Nilegeze’ na nyingine nyingi, ameiambia Mwanaspoti kuwa licha ya kuiwaza siku yake ya ndoa lakini haitakuja mapema sana.

“Sifikirii ndoa kwa sasa, bado nakula ujana kwanza na mpenzi wangu, hivyo mashabiki wanaosubiri ndoa yangu wanipe nafasi kidogo, acha nijiachie kidogo,” alisema Lulu Diva huku akiacha tabasamu zuri katika uso wake uliojaa urembo wa asili. 

Lulu Diva aliendelea kulitonya Mwanaspoti kuwa licha ya watu kumuunganishia matukio na kumpa skendo za kujihusisha na baadhi ya wanaume maarufu lakini mwanaume halisi ambaye atamuoa hawatamjua kirahisi.

“Unajua  kwanini nasema ndoa yangu itakuwa siri? Au kutomuanika mwanaume atakayenioa?  Sababu hadi sasa nishapewa wanaume feki na watu mitandaoni, we mwenyewe umeona na kuniuliza hapa, mara Diamond, mara Jaguar (Kenya), mara Rich Mavoko yaani walifika mbali hadi kunihusisha kimapenzi na kaka yangu Idrissa Sultan. 

“Sasa watashangazwa sana na mimi kwa sababu mengi yanayosemwa si ya kweli lakini siku watasikia tu nishaingia kwenye ndoa na ni mke wa mtu, mume wangu hawawezi kumjua kirahisi, kama wanavyofikiria,” alisema Lulu Diva.

Mbali na hiyo, Lulu Diva ambaye kwasasa amejikita katika tamthilia, amesema hajaupa kusogo muziki bali ameamua kuonyesha Watanzania kuwa ana kipaji kingine mbali na muziki.

Lulu Diva kwa sasa anafanya mambo makubwa tamthilia ya ‘Rebeca’ inayorushwa kupitia DStv, na amesema ameona muda mwingi auweke kwenye kuigiza.

Alisema amepumzika muziki kwa muda, lakini atarejea kwa kishindo kama cha radi.

Advertisement