Hilo shangwe la Fiesta ni noma

Monday December 24 2018

 

By Nasra Abdallah

SHANGWE la tamasha la Fiesta ni kama ndio linaanza mwanangu kwani, usiku wa kuamkia jana mambo yalikuwa moto kwelikweli.

Kwa wale mashabiki wa burudani walioamua kulala kwa watakuwa wanajilaumu wenyewe tu, baada ya kupewa ishu nzima ya kile kilichotokea huko.

Wakati lilipopigwa zengwe kufanyika mara ya kwanza pale Viwanja vya Leaders, Novemba 24 mwaka huu, kila shabiki alidhani kwamba, ndio mwisho wa Fiesta kwani, hata lilipotangazwa kuwa shangwe zitahitimishwa tena Desemba 22, wapo waliokuwa na mtazamo kuwa haliwezi kubamba tena.

Lakini, aaaah wapi bana kuna watu wanajua kusimamia shoo na juzi usiku sasa ikadhihirika kwamba, Clouds bado ni mafaza wa game ya muziki nchini. Shoo iliyopigwa kwenye Viwanja vya Posta pale Kijitonyama haikuwa ya kitoto kabisa.

Shoo hiyo ilianza juzi saa 4:00 usiku hadi majogoo iliwabamba kinoma mashabiki na kukata kiu ya burudani waliyokuwa nayo kwani, hakukuwa na tamasha kubwa lililopigwa hivi karibuni na kuwabamba mashabiki wa Dar.

Kama kawaida mastaa kibao wa Bongo Flava walipiga shoo ya kibabe kwenye tamasha hilo huku AliKiba akalimata jukwaa vilivyo.

AliKiba akiwa na kundi lake la Kings Music lenye mastaa wanne sambamba na mdogo wake Abdul Kiba, walinukisha na kuwafanya mashabiki wengine kumwaga machozi kwa furaha huku wengine wakinyanyua mabango wakimtangazia ofa kibao.

Kiba na kundi lake walipanda jukwaa saa 10:00 alfajiri na kunogesha mzuka viwanjani hapo kana kwamba, shoo ndio ilikuwa inaanza vile.

Wale waliokuwa wakisinzia kwa kunogewa na usingizi huku wengine stimu zikiwa zimepanda kichwani kutokana na kinywaji, aah mbona waliamka na kuangusha burudani kama yote.

Kiba alipanda jukwaani akiwa amevalia mavazi kama mfalme na bakora yake ndeefu na kuangusha ngoma ya na Seduce Me kisha akashusha ngoma zake mpya za Kadogo, Mwambie Sina na Masozy ambazo kwa sasa ndio habari ya mujini.

Mbali na King Kiba, wasanii wengine waliotetemesha jukwaa ni Juma Kassim Kiroboto a.k.a Nature. Nature, ambaye kwa sasa amekuwa kimya kidogo lakini, anaposhika jukwaa mbona moto unawaka. Alianza na ngoma ya Sitaki Demu, Ugali, Stand Up na kuhitimisha na Asia.

Wakati Nature akifanya yake huko kwa mashabiki ni miguu na mikono tu ndio ilikuwa hewani. Yaani zile staili za kiumeni ndio zilikuwa zinabamba tu hapo.

Kabla jasho halijakatika unaambiwa, tayari Chid Benz alikuwa ameshafanya yake akiwarusha mashabiki na ngoma za Dar es Salam Stand Up, Raha za Dunia, Niite Chid ambazo zilibamba kinoma.

Pia, walikuwepo Vanessa Mdee, Maua Sama, Julie, Bilnas, Chegge, Rich Mavoko, Fid Q, Snura, Christian Bella, Benson Hauzimi, Dogo Janja, Weusi, Mafik na Sogy Doggy.

Makonda kama kawa

Katika shoo hiyo kama kawaida mwenye mkoa wake hakuwa nyuma. Ndio, Paul Makonda hakutaka kupitwa na Shangwe za Fiesta kwani, aliungana na wananchi wake kwenye viwanja hivyo na kufurahia burudani.

Makonda alitinga kwenye viwanja hivyo vya maraha majira ya saa 7:00 usiku na ndani ya saa moja tu alikuwa ameridhika na mzuka uliopo na kusepa zake.

Hata hivyo, hakuondoka kimya kimya unaambiwa ambapo, alitoa neno la kumtakia kheri na kupona haraka Mkurugenzi wa Vipindi wa Clouds Media, Ruge Mutahaba ambaye yuko Afrika Kusini kwa matibabu.

Makonda alishusha dua kisha akawapasha wale wanaozoza huko mitaani akiwataka kufahamu kwamba, hakuna asiyejua mchango wa Ruge katika Bongo Flava hivyo kila mmoja ana kila sababu ya kupiga goti na kumuombea mazuri kwa Mungu.

“Hakuna asiyejua mchango wa Ruge katika Sanaa, leo kuna wasanii ni mamilionea kupitia burudani. Wale wanaomsema kuwa Ruge aliwabania wanapaswa kubadilika kwani, kwa namna moja ama nyingine alikuwa anawajenga. Mnapaswa kushukuru badala ya kumlaumu kwa kuwa amekuwa moja ya mafanikio yako,” alisema.

Advertisement