Diamond aibukia kwa Alicia Keys

Tuesday September 15 2020
alicia keys pic

Licha ya kwamba tayari ameshafanya mambo mengi makubwa ya kuvunja rekodi, mwanamuziki wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz ameendeleza desturi yake hiyo baada ya jana jina lake kutajwa kwenye albamu ya mwanamuziki wa Marekani, Alicia Keys.

Kupitia kwenye moja ya akaunti za mtandao wa kijamii wa Twitter zilizojikita kwenye kutoa habari za msanii Alicia Keys, liliwekwa tangazo la albamu yake anayotarajia kuiachia Septemba 18 mwaka huu na wakatajwa miongoni mwa wasanii alioshirikiana nao na hapo ndipo jina la Diamond lilipochomoza.

“Albamu ijayo ya Alicia Keys ambayo inaitwa Alicia itakuwa na nyimbo 15 na atakuwa ameshirikiana na wasanii kama vile Miguel, Khalid, Sampha, Diamond Platnumz, Snoh Aalegra na Jil Scott!” imeandikwa katika ukurasa huo.

Lakini pia baada ya post hiyo, post nyingine iliwekwa ikionesha nyimbo zote 15 katika Albamu hiyo ambapo wimbo wa Alicia Keys na Diamond ni wimbo namba nne unaoitwa Wasted Energy.

Mbali na kuwemo kwenye albamu, pia jina la Diamond limejitokeza kwenye Playlist ya Alicia Keys ya mtandao wa kusikiliza muziki wa Spotify, ambapo aliweka nyimbo 15 anazosikiliza sana, na mbili kati ya hizo ni za Diamond.

Ngoma hizo ni African Beauty ya Diamond ft Omarion (msanii wa Marekani), na Nana ya Diamond ft Mr. Flavour (msanii wa Nigeria)

Advertisement

Diamond ambaye pia ni bosi wa lebo ya muziki ya Wasafi Classic Baby (WCB), yenye wasanii kama Zuchu, Mbosso na Rayvann hakuwa nyuma, kwani kupitia akaunti yake ya Instagram alipost picha ya Playlist ya Alicia Keys kama ishara ya kuheshimu kilichofanywa na Alicia.

 

Mahaba ya Familia ya Alicia kwa muziki wa Tanzania

Mwanzoni mwa mwaka huu mume wa Alicia Keys ambaye pia ni prodyuza mkubwa wa muziki nchini Marekani, Swizz Beatz aliweka video kupitia ukurasa wake wa Instagram akisikiliza wimbo wa singeli wa wasanii Lava Lava na Meja Kunta unaoitwa Wanga.

Kama hiyo haitoshi, Februari mwaka huu Swizz Beatz aliweka video nyingine tena akisikiliza wimbo huo huo lakini safari hii akiwa ameufanyia remix, yaani marudio kwa kuuongezea vionjo kwa kuuchangana na muziki wenye asili ya kimarekani, Hip Hop.

Katika post hizo, Swizz Beatz ameeleza wazi mahaba yake juu ya muziki huo mpya masikioni mwake huku akiweka wazi kwamba anajikita katika kujifunza na kuelewa ili siku moja zijazo atengeneze muziki wa singeli pia.

Hii ni dalili nzuri kwa sababu kama itafikia hatua hiyo, jina la Tanzania litazungumzwa zaidi nje ya mipaka kwa sababu muziki wa singeli hapa ndo nyumbani kwake.

Advertisement