Diamond afichua ukweli kuhusu Tanasha, Hamisa, Wema

Monday April 27 2020

 

By RHOBI CHACHA

NYOTA wa muziki wa kizazi kipya nchini, Naseeb Abdul 'Diamond Platnumz' amezungumza habari za kuachana na mzazi mwenzake Tanasha Dona, na ushiriki wa Hamisa Mobetto kwenye video ya Alikiba pamoja na kurudiana na Wema Sepetu.
Diamond amezungumza hayo leo Jumatatu kupitia mtandao wa YouTube wa Wasafi Media ambapo alianza kwa kusema kuwa wameachana na Tanasha ambaye alikuwa na matarajio ya kumuoa kwa asilimia 100.
"Unajua kuhusu Tanasha kwakuwa hajaweka wazi kilichotokea sasa sio vizuri kuongelea suala hilo, ila kiufupi hatuko pamoja na Tanasha kulikuwa na sababu ziko nje ya uwezo wake na mimi nje ya uwezo wangu hivyo tulipeana muda, niliongea nae tu vizuri utengano wetu hauhusishwi kunifumania kama baadhi ya watu wanavyosema
"Nilishangaa habari za mimi kufumaniwa na Tanasha nchini Kenya kitu ambacho hakijawahi kutokea, huwezi amini katika mahusiano yangu ya kimapenzi kwa Tanasha niliamua kutulia kabisa mambo mengi ya ujana niliweka pembeni toka nilivyokuwa naye.
"Kuna mambo tu ya kifamilia kama familia tunaitengenezaje kesho yetu hapo ndio kuna vitu vilikuwa vinapingana kati yetu,  ndio tukasema pengine kila mtu anatakiwa kutafakari kwanza kwa upande wake ndio ikawa mtengano mliouona,  kwahiyo Mungu kama akipanga tuwe wote tutakuwa wote tu asipopanga basi" amesema Diamond.
Daimond amefafanua madai ya Tanasha kumbadirisha dini hapa; "Ni kweli tulipokuwa Kigoma, Tanasha alibadiri dini akawa Muislamu, hakulazimishwa kubadiri dini kama inavyosemekana kwa watu.
"Ila alipenda mwenendo wa kutokana na ndugu yangu Ricardo Momo kuzungumzia mawaidha ya dini kila wakati ndipo mimi nikamwambia ndugu yangu ukifanikisha Tanasha abadiri dini nakununulia kiwanja.
"Basi siku ya siku Tanasha mwenyewe akanitamkia anataka kubadiri dini ameupenda Uislamu, nilimuuliza unamaanisha? akajibu ndio, nikamwambia katafakari urudi tena kuniambia, akarudi tena kuniambia ndio anataka kubadiri dini ndio akabadiri
Diamond aliendelea kusema; "Mimi ukweli nilitaka kumuoa Tanasha, nilipanga kabisa asilimia 100, sasa sijui imekuwaje labda Mungu hakupanga na huenda ana makusudi yake huko mbele, ila kama nilivyosema mwanzo kuna vitu vimeingilia ambavyo havikuwa sawa upande wake na wangu ndio maana tumepeana muda wa kutafakari kila mmoja"
Kwa upande wa Hamisa Mobetto kuhusu ushiriki wa video ya wimbo Dodo wa msanii Alikiba, Diamond amesema alitoa  baraka zote kwani kabla ya kwenda Hamisa alimtaarifu ushiriki wa video hiyo.
"Ukweli ni kwamba Alikiba ana haki ya kumtumia mtu yeyote kwenye video na hata Hamisa ana haki ya kushiriki kwenye video yeyote ya msanii, niwajuze  tu watu kitu ambacho hawakijui Hamisa kabla ya kwenda kushiriki aliniambia kuwa Alikiba amemcheki kutaka kushiriki kwenye wimbo wake mpya.
"Hivyo ananipa taarifa isije nikaja kuona wimbo ushatoka na watu wakaongea tofauti  nikamwambia nenda nakupa baraka zote" amesema Diamond.
Hivi karibuni mitandao ya kijamii imekuwa ikisimulia sana habari za Diamond na Wema Sepetu kurudiana kimapenzi hapa anafafanua;
"Hizi habari zipo naziona kwenye mitandao, ila watu hawajui kwasasa naheshimiana vipi  na Wema, nilichoamua ni kuwa karibu na wanawake wote niliowahi kuwa nao kwenye mahusiano, sitaki bifu liendelee nao ndio maana nimejirudi kwa Wema sio kwa mapenzi narudia tena namuheshimu sana" amesema Diamond

Advertisement