Dada Mkuu Jide naye aitwa Basata

BARAZA la Sanaa la Taifa(Basata), limeendelea kuonyesha makucha yake kwa kushughulikia mmomonyoko wa wa maadili katika sanaa.

Hii ni baada ya hivi karibuni kumuita msanii wa siku nyingi katika muziki wa Bongo Fleva, Judith Wambura ’Jay Dee’ kwa ajili ya mahojiano.

Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza, alisema wiki moja iliyopita walikutana na msanii huyo mwenye majina mengi, ikiwamo Dada Mkuu, Binti Machozi na Komando kwa ajili ya mahojiano.

Hatua hiyo ya kumuita na kumuhoji, Mngereza alisema imetokana na wimbo wake wa ‘One Time’ aliouchia mwezi mmoja uliopita.

“Ni kweli tumemuita Jay Dee kama wazazi na walezi wake katika sanaa kuzungumza naye, kubwa likiwa ni wimbo wake wa One Time, ambapo kuna kitu kama bangi anaone-kana kukivuta katika video ya wimbo ule.

“Kama mnavyojua matumizi ya bangi ambayo ipo katika kundi la dawa za kulevya hayaruhusiwi katika nchi yetu, hivyo tumemuita kuhojiana naye suala hilo kama walezi wake, mambo ambayo tumekuwa tukiyafanya kwa wasanii mbalimbali,” alisema.

Hata hivyo, Katibu huyo alikataa kueleza kiundani ni hatua gani wameamua kumchulia Jide kuhusiana na suala hilo kwa kile alichoeleza kuwa ni mambo ya kiofisi zaidi na itakapofika hatua ya kuwekwa wazi watalisema.

Wakati kuhusu kama kuna hatihati ya kuuufungia wimbo huo au kuurudia, Mngereza alisema yote yanawezekana na kumtaka mwandishi wa habari hii kuwa na subra.

Kwa upande wake Jide alipotafutwa kuhusu sakata hilo, alisema waulizwe Basata.

Jide hivi karibuni amesherehekea miaka 20 ya kufanya muziki.