Amkeni amkeniii... Enzi za Ngwasuma zarudishwa

Tuesday December 24 2019

 

By Rhobi Chacha

AMKENI amkeniii... Bila ya shaka unazikumbuka zile enzi za ngoma kali kali za FM Academia Wazee wa Ngwasuma. Na hakika utakuwa umezimisi zile tungo tamu kama Prison, Dunia Kigeugeu na Hadija,Heshima kwa wanawake.

Basi unaambiwa Wazee wa Pamba, Wazee wa Mjini, Wazee wa Ngwasuma watakutana katika jukwaa moja kwa ajili ya onyesho moja ya Funga Mwaka siku ya Boxing Day Desemba 26, 2019 kwenye Ukumbi wa Escape One jijini Dar es Salaam.

Wale mastaa wote uliokuwa ukiwashabikia wakati ule wanakutana kwenye jukwaa moja. Moto utawaka wakati 'Wazee wa Bling Bling', kina Patcho Mwamba
, Liva Sultan
, Papii Kocha,
Toskani Nzimbu, Totoo Zebingwa, Jose Mara
, Kardinal Gento
, Malou Stonch
, Jesus Katumbi
 'Jesus', rapa G-Seven, Pablo Masai, King Blaize, Papii Kocha, Elombee Kichinja, Balotelli na wengineo watakapokiwasha pale.

"Tingisha kama imeisha... weka nyingine', 'Samaki ana vipande vingapi... vitatu.. hebu vitaje... kichwaa, tumbo na mkia.... tingisha mkiaaa," ni kati ya raha zile watakazokumbushwa mashabiki pale.
 
Akizungumza na Mwanaspoti mmoja wa waandaaji wa tamasha hilo, Anania Junior amesema ni tamasha mahususi kwa ajili ya kukuza muziki wa dansi pamoja na kuimarisha umoja na ushirikiano kati ya wanamuziki wa dansi.

“Lengo kuimarisha ushirikiano katika wanamuziki wa dansi pamoja na kukuza muziki wa dansi kuhakikisha wapenzi wa muziki huu wanapata burudani," alisema Anania Junior.

Tamasha hilo lenye kiingilio kuanzia Sh. 10,000 na V.I.P ni Sh.50,000 hadi Sh.100,000  zitaporomoshwa nyimbo zote zilizowahi kutamba kama katika bendi ya FM Academia kama Heshima kwa Wanawake, Shida, Hadija, Freedom, Prison, Dunia Kigeugeu, Neema,Dotnata na nyingine nyingi.

Anania amesema tamasha hilo lililoratibiwa na Clouds Plus Production & Classic FM, linakwenda kwa jina la 'Ngwasuma Reunion Day'.

Amesema wanamuziki hao wamejichimbia kambini na wameahidi kufanya balaa katika usiku huo.

"Ukweli hili tamasha la Ngwasuma Reunion ambalo ni muunganiko wa wanamuziki tuliowahi fanya kazi katika bendi ya FM Academia,tumejiandaa vya kutosha kuwapa burudani wapenzi wa muziki wa dansi,na nikwambie tu sauti bado zipo na mashairi hakuna hata mtu mmoja aliyeyasahau, watu waje tu kwa wingi"alisema Jose Mara


Naye Rapa Kitokololo amesema haya "mambo yatakuwa balaa tarehe 26 siku ya Boxing Day,nitaimba Rapu zangu zote nilizowahi imba pindi niko FM academia,na najua watu wananifahamu vizuri mimi Kitokololo Kuku mambo yangu huwa sinaga shoo mbovu" alisema Kitokololo
 


Advertisement