Wema: Nilifikisha kilo 109

Friday February 21 2020

 Wema: Nilifikisha kilo 109,MREMBO Wema Sepetu,Miss Tanzania 2006,

 

By Nasra Abdallah

MREMBO Wema Sepetu, amesema wakati akiwa na mwili mnene alifikisha kilo 109, jambo ambalo halikuwa zuri kiafya kwake.
Wema ameyasema hayo leo Ijumaa katika hafla ya utiaji saini kati yake na kiwanda cha rasta cha Angel kuwa balozi wa bidhaa zao.
Wema alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa na Waandishi wa Habari waliotaka kufahamu jinsi anavyojisikia baada ya kupungua mwili na namna ambavyo anazungumziwa na watu.
Wema amesema anajisikia furaha kwani mwili wake ulifika hatua mbaya hadi kilo 109 na hii ilitokana na kujiachia kwa kula kila kitu vikiwemo vyakula vya kuongeza uzito.
Amesema kutokana na kula vyakula maalum, mazoezi na kunywa dawa mbalimbali amepungua hado kufika kilo 65 kwa sasa.
"Huu mwili ndio niliokuwa nauhitaji, nilipokuwa Miss Tanzania 2006 nilikuwa na kilo 55, lakini nilijiachia hadi  kufika kilo 109 kwa kweli nilikuwa naelekea kubaya, nashukuru Mungu kufika hapa.
"Hata siku nikijaaliwa kupata mtoto nitajitahidi nibaki mwembamba kwa kuwa unanipa amani, wembamba raha jamani asikuambie mtu,"amesema Wema.
Kuhusu watu wanavyomzungumzia ikiwemo kusema anaumwa, Wema ambaye pia ni msanii wa filamu amesema hajali kwani hata alivyokuwa mnene walimsema na kumpa maneno mengi ikiwemo nyumbu, tembo na mengineyo.
Kuhusu ubalozi wa rasta aliopewa, amesema hii ni mara yake ya kwanza kupata ubalozi na inaonyesha mwaka wake utakuwa mzuri kutokana na mitihani aliyopitia miaka miwili iliyopita.

Advertisement