EXTRA SPESHO: Nandy ukijilaumu, mlaumu na Mondi

BAADA ya tamasha lile kubwa la hisani lililopewa jina la Siku ya Afrika (#Kutokea Nyumbani) lililofanyika Mei 25 na kurushwa na MTV Base Afrika, Nandy alijikuta kitanzini.

Nyota huyo wa Bongofleva alikosolewa sana na kushambuliwa kutokea kila kona ikiwamo kwenye mitandao ya kijamii kutokana na shoo aliyoifanya katika tamasha hilo.

Binti wa watu masikini hakuweza kuvumilia. Akaomba radhi. Ameomba radhi kwa mashabiki wake akisisitiza kwamba wanamfahamu na hajawahi kuwaangusha, ila hili limetokana na kupotoshwa na menejimenti yake.

Nandy amesema menejimenti yake ilimfikishia vibaya taarifa. Ikamueleza atume video akiwa nyumbani kwake wakati huu wa kukaa nyumbani kutokana na corona, awe anaimba. Ndio wakaja na kamera zao akakaa tu kwenye kochi lake sebuleni akaimba hadi shoo yake imeisha. Ndio, amekaa tu kwenye kochi.

Wengi wakaitaja ‘perfomance’ yake katika onyesho hilo kuwa ndiyo mbovu zaidi ukilinganisha na wasanii wote walioshiriki.

Na kwamba amejiangusha mwenyewe kwa kushindwa kuitumia fursa nzuri ya kutazamwa na hadi kina Ludacris, Fat Joe, French Montana au Sean Paul, ambao inatarajiwa watakuwa wameitazama shoo hiyo kwa vile wameshiriki japo kwa kutoa ujumbe wao kwa jamii kuhusu kuchangia wenye uhitaji.

Watu wanajua kwamba hiyo ilikuwa ni ‘platform’ adimu sana ambayo msanii alipaswa kufanya kitu ambacho kingebaki akilini mwa mastaa hao wakubwa wa muziki duniani. Na ukiwakaa kichwani huwezi kujua nini kitatokea baadaye. Kiufupi lile lilikuwa ni ‘jukwaa’ la kujikubalisha kwa watu wa maana sana Afrika na duniani kwa ujumla.

Kwa sababu orodha tu ya mastaa walioshiriki kutumbuiza au angalau kutoa ujumbe, ilikuwa si ya kitoto. Kwa waliolishuhudia wanatambua. Kila msanii alirekodi video yake akiwa nyumbani kwake katika kipindi hiki cha janga la corona na kuwatumia DSTV ambao waliziweka pamoja na kuzirusha siku hiyo kupitia chanel MTV Base Africa. Supastaa wa filamu wa Uingereza, Idris Elba, ambaye asili yake ni Afrika kwa baba mwenye asili ya Sierra Leone na mama Mghana, alikuwa muongozaji wa shoo hiyo.

Orodha ya waliotumbuiza shoo hiyo ni ‘hataree’. Alikuwapo mwanadada raia wa Afrika Kusini aliyekulia na kusoma shule za Dar es Salaam, Sho Madjozi, ambaye amepata kutamba na ngoma ile kali ya ‘John Cena’, alikuwapo Davido, kundi la Sauti Sol, Fally Ipupa, Bebe Cool, Angelique Kidjo, AKA, Burna Boy, DJ Maphorisa, Salif Keita, Tiwa Savage, Toofan, Yemi Alade na wengineo wengi.

Mastaa waliotokea na kutoa tu salamu za hamasa kwa jamii kusaidia wenye uhitaji ni pamoja na Mcongo anayecheza kikapu NBA, Serge Ibaka, ambaye alimtambulisha Fally Ipupa kutumbuiza, mwanariadha anayeshikilia rekodi ya dunia ya marathon, Eliud Kipchoge aliyelitambulisha kundi la kwao Kenya la Sauti Sol, marapa wa Marekani Ludacris, Fat Joe, French Montana, mwanamuziki wa Jamaica, Sean Paul, muigizaji wa Nigeria Omotola Jalade, mwanamuziki Jidenna, Yvonne Chakachaka, Kirk Franklin na kundi la Lady Smith Black Mambazo.

Waliongea pia mastaa wa tamthilia maarufu ya ‘Power’ inayoandaliwa na rapa 50 Cent huko Marekani, Naturi Naughton (Tasha St. Patrick), Omari Hardwick (Ghost) na Rotimi (Andre ‘Dre’ Coleman) akiwa sambamba na rafikiye wa kike staa wa Bongofleva, Vanessa Mdee. Nyota mwingine wa Bongofleva, Ommy Dimpoz pia aliachia ujumbe wake wa hamasa katika onyesho hilo la kutokea majumbani kwa mastaa.

Rais wa Rwanda, Paul Kagame na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, wote walitoa ujumbe muhimu katika tukio hilo la hisani ambalo mapato yote yalipangwa kwenda katika Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto (Unicef).

Pengine Nandy hapaswi kujilaumu sana kwa kutumbuiza akiwa amekaa tu kwenye kochi sebuleni, kwa sababu hata Sauti Sol walitumbuiza kwa wimbo wao wa ‘Insecure’ wakiwa wamekaa tu sebuleni kwa wimbo mzima. Hata Fally Ipupa alitumbuiza wimbo mzima peke yake akiwa amekaa tu kwenye chumba na hata Davido alikuwa studio tu wimbo mzima mbele ya mic.

Tofauti yao na Nandy ni kwamba Sauti Sol na Fally Ipupa walikuwa na magitaa.

Pengine mtu aliyemchongea Nandy hasa ni Mtanzania mwenzake, Diamond Platnumz. Huyu kijana kutoka Tandale siyo mtu mzuri kabisa linapokuja suala la ‘perfomance’. Daima hachukulii poa shoo yake yoyote na aliua sana katika onyesho lile.

Akitumbuiza kwa wimbo wake wa ‘Jeje’, Mondi alitengeneza kama muvi flani hivi inayoanza akiwa amelala chumbani, kisha binti anamletea chai ya asubuhi, ile wazungu wanaita ‘Breakfast In Bed’. Halafu mnyama ananyanyuka kitandani na kumuimbia ‘Jeje’ binti huyo huku akimfuata.