CHIBU DANGOTE Kwa Tanasha sichomoki

Friday December 7 2018

 

By Mwandishi wetu

DIAMOND Platnumz! Ndio unalipotaja jina hili ni lazima uambatanishe na sifa zake ambazo zimemfanya kuishika game ya Bongo Flava barani Afrika. Ni miongoni mwa mastaa wenye mafanikio makubwa kwa sasa akicheza anga za akina Wizkid, Davido na wengine kibao wanaosumbua kwa sasa kupitia muziki.

Hapa Bongo amefanya mambo makubwa na kujikusanyia sifa kibao, ikiwemo kusaidia jamii iliyomzunguka na hili wale masela wa Tandale wanalifahamu vizuri.

Lakini, achana na sifa hizo, kuna nyingine ambayo imekuwa ikimtambulisha vyema nayo ni sukari ya warembo. Amecheza anga za madem wakali na wa kishua kuanzia Bongo, Nairobi mpaka Kampala, yaani jamaa haachi kitu unaambiwa.

Rekodi za Diamond kwa warembo sio za mchezo mchezo kabisa. Amepitia kwenye mahusiano mbalimbali ya kimapenzi, lakini kuna wanawake watatu ambao Diamond ilionekana ndio amefika mwisho.

Penzi la warembo hao na Diamond Platinumz lilikuwa gumzo huku wakiwa hawana noma kuonyesha hadharani kwamba, wanapendana hivyo wengi kuamini kuwa staa huyo wa Bongo Flava atangaza ndoa na kutuliza mizuka.

WEMA SEPETU

Penzi la Tanzania Sweetheart, Wema Sepetu na Diamond lilitikisa kila kona kuanzia Bongo hadi Nairobi, Kampala hadi DR Congo.

Ilikuwa ni couple moja matata sana, ambayo kwa namna fulani ilikuwa chachu ya mafanikio ya Diamond. Uhusiano huu ulianza wakati Diamond akianza kuishika game ya Bongo Flava na kufungua mipaka ya muziki wake kuteka mashabiki nje ya Tanzania na kupiga shoo kibao. Hapo Wema akaimbiwa ngoma kibao na kushiriki kwenye video za Diamond, ambapo hakuna jukwaa ambalo hakupandishwa kutambulishwa kwa mashabiki.

Mashabiki wengi waliamini na wengine kutamani uhusiano huu kwenda kujenga familia ya Wema na Diamond, lakini ghafla tu mambo yakabadilika na kila mmoja kushika njia yake. Team Wema na Team Diamond ambazo zilikuwa na nguvu huko kwenye mitandao ya kijamii katika kuwabeba wapenzi hao, zikaanza kuingia kwenye bifu na kutupiana kauli za shombo.

Kabla ya kuingia kwenye bifu, wakati penzi likipamba moto Wema alinukuliwa mara kadhaa akisema kwamba, Diamond ndio mumewe wa ukweli yuko tayari kuolewa naye.

Diamond mwenyewe aliwahi kukiri kwamba, penzi lake na Wema lilimemfanya kuwa mtu tofauti na kujifunza mambo mengi ya kumsaidia katika maisha ikiwemo kujifunza lugha ya Malkia (Kiingereza), ambapo kwa sasa anakigonga kiulaini kabisa.

ZARI

Baada ya penzi la Wema kufa kifo cha kawaida tu, Diamond akaibukia kwa mrembo wa Kiganda, Zarina Hassan (Zari The Boss Lady), uhusiano ambao ulianza kama utani vile.

Wawili hawa inaelezwa kuwa walikutana wakiwa safarini na kuanzisha mawasiliano ambayo yaliangukia kwenye mapenzi mazito. Safari za Diamond kwenye Jiji la Kampala, Uganda zikapamba moto na baadaye mambo yakawa hadharani.

Kama ilivyokuwa kwa Wema, Zari naye hakuwa mtu wa mchezo mchezo kabisa kwani, huko kwenye mitandao ya kijamii kulikuwa kama ndiko anakolala na kuamkia. Alikuwa na kundi kubwa la wafuasi waliokuwa wakirusha ishu zake za kibiashara na kujibu mapigo pindi anaporushiwa makombora na kambi zingine.

Hata hivyo, kwa Zari na Diamond uhusiano huo ulikwenda mbali zaidi na kupatikana watoto wawili, Tiffah na Nillan na kila kukicha ishu za ndoa zilikuwa zikizungumzwa sana.

Lakini, kama kawaida Sukari ya warembo akafanya yake na uhusiano huo ukamalizika kwa maumivu kwani, ujumbe wa kutemana ulitumwa kupitia mtandao wa Instagramu na haikuwa siri za chumbani tena.

Hapo ndipo wambeya wakafahamu kwamba, sio kila ua ridi ni nyekundu hata meusi nayo yapo.

Chanzo cha kusambaratika kwa uhusiano wa Zari na Diamond ikatajwa kuwa ni mrembo Hamisa Mobetto, ambaye ilikuja kudhihirika kuwa amezaaa na msanii huyo.

Awali, Mobetto na Diamond waliofanya ngoma ya Salome, walikuwa wakifanya siri kubwa uhusiano huo lakini, mimba ya Dylan ikaweka mambo hadharani na Zari akaamua kunyoosha mikono na kuachana na Sukari ya warembo.

Kwa sasa Mobetto hayupo tena na Diamond, lakini bifu la warembo hao halijawahi kumalizika hata kidogo na kambi zao zinaendelea kurushiana maneno ya shombo mitandaoni tu.

Tanasha Donna

Ndio habari ya mujini kwa sasa na ukiingia kwenye anga za kurasa za Diamond huwezi kukosa kukutana na neno ‘kitu ya boss’. Baada ya kutoka Uganda, kwa sasa Diamond ameweka majeshi kwa mrembo huyu wa Kenya, ambaye ni mtangazaji wa Kituo cha Luninga cha NRG.

Diamond inaelezwa kuwa amepagawa na penzi la Tanasha Donna kwa sasa anawaza ndoa tu. Wiki iliyopita Diamond alipiga shoo moja matata mjini Thika na Tanasha alikuwepo na hapo akatambulishwa rasmi kwa mashabiki kwamba, ndiye mpango mzima kwa sasa.

Pia, Chibu Dangote aliweka bayana kwamba, miongoni mwa wasichana aliowahi kuwa nao amemweleza zaidi Tanasha hivyo, anataka kufuta rekodi zote za nyuma na kutulia na mrembo huyo.

“Tanasha ndiye mwanamke aliyenionyesha kujali uzito juu ya ndoa, hivyo rasmi natangaza kumuoa huyu. Ana sifa zote za mwanamke wa kuoa,” alisema Mondi.

Advertisement