Saa 24 ngumu kwa Ngoma Jangwani

Muktasari:

  • Bosi huyo aliyekuwa katika meza iliyotumika kumsainisha Ngoma,  alisema wameona ni bora kuchana na straika huyo.

MASHABIKI wa Yanga wameanza kuhesabu saa tu kabla ya kujua hatma ya straika wao wa kimataifa kutoka Zimbabwe, Donald Ngoma, kwani mabosi wa klabu hiyo wanapiga hesabu kumsitishia mkataba, lakini wakipiga hesabu za maana.

Taarifa ambazo Mwanaspoti limezipata kutoka ndani ya Yanga ni kwamba ndani ya saa 24 kuanzia unapolisoma gazeti hili kuna kikao kizito kitafanyika kumaliza uhai wa Ngoma ndani ya timu hiyo na kinachomuondoa ni kubainika si wa kupona leo wala kesho.

Mmoja wa mabosi wa Yanga ameliambia Mwanaspoti uongozi umepata ripoti iliyoshiba kutoka kwa mmoja wa madaktari wao kuwa  wachague moja kumvumilia au kuachana naye na wao kuamua kumpiga chini.

Bosi huyo aliyekuwa katika meza iliyotumika kumsainisha Ngoma,  alisema wameona ni bora kuchana na straika huyo.

Inaelezwa huo ndio msimamo utakaopelekwa katika kikao hicho cha mwisho, kubwa likiwa ni kuokoa gharama katika kuendelea kumlipa mshambuliaji huyo.

Ngoma ambaye anachukua kiasi kisichopungua Dola 3,500 (kama Sh8 milioni) kwa mwezi, uongozi umeona ni bora kumlipa mishahara ya miezi miwili kuokoa hasara zaidi ambapo sasa atachukua kiasi cha Sh15 milioni ikiwa ni gharama ya kuvunja mkataba.

Hata hivyo, Yanga imekubalia kuingia hasara hiyo kufuatia straika huyo kuchukua kiasi cha Sh89.6 milioni walipomsainisha mkataba wa miaka miwili katikati ya mwaka jana.

Mbali ya ripoti hiyo ya Daktari, Mwanaspoti linajua mmoja wa mastraika wa timu hiyo pia amehusika kukatwa kwa Ngoma baada ya kuwaambia mabosi wa klabu hiyo uwezekano wa kurudi kwa Mzimbabwe huyo ni mdogo kauli iliyowashtua.

SIMBA WACHEKELEA

Wakati Yanga wakipambana kukata jina la Ngoma, mtaa wa pili kwa watani wao Simba kumekuwa na kicheko cha kujipongeza baada ya kumkosa straika huyo.

Bosi mmoja wa Simba amefichua kwamba ndani ya klabu yao Ngoma alibakiza hatua chache kutua kwa kishindo akimfuata kiungo Haruna Niyonzima, lakini mgawanyiko ulioibuka ndiyo uliochelewesha dili hilo.

“Tulishakubaliana karibu kila kitu na Ngoma sasa kilichotokea kuna makundi mawili yaliibuka moja likigomea usajili huo wakidai ulikaa kisiasa zaidi wengine wakisema asajiliwe atasaidia.” chanzo kilisema.

“Waliokataa walikuja na hoja ya majeraha yake lakini pia waliona Bocco (John) anatosha.

“Wale waliokuwa wanakataa sasa wanatusumbua sana wakitamba walikuwa sahihi kutokana na hiki kinachoendelea kwa wenzetu.”