Waletwe wengine, hawa wamechoka

Thursday March 8 2018

 

LONDON, ENGLAND. NDO kama ulivyosikia. Petr Cech nyakati zake zimeshaanza kufikia ukingoni kwenye kikosi cha Arsenal kwa sasa. Kipa huyo umri umeshaanza kumtupa mkono, miaka 35 haonekani tena kuwa na kitu cha maana cha kuisaidia timu hiyo yenye maskani yake huko Emirates zaidi ya kuishia kuwaomba radhi tu mashabiki kutokana na vichapo wanavyopokea mfululizo. Arsenal imechapwa mara nne mfululizo ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 2002.

Wakati wanachapwa na Brighton 2-1, Cech alifanya makosa ya bao la kwanza na alikuwa na nafasi ya kuokoa la pili, jambo lililomfanya kuwa gumzo kwenye Twitter mashabiki wa timu hiyo wakimwaangushia lawama kwamba amehusika kwenye kipigo walichokumbana nacho. Hata hivyo, Cech si mchezaji pekee mwenye kiwango duni kwa siku za karibuni ambapo timu anayochezea kwenye Top Six zinapaswa kutafuta wabadala wake.

Arsenal -

Petr Cech

Kipa huyo wa Jamhuari ya Czech amekubali lawama zote zilizoelekezwa kwake kutokana na kichapo cha Brighton. Kipa huyo veterani amekuwa kwenye kiwango cha chini sana msimu huu na kwamba kocha yeyote atakayekuja kuinoa Arsenal msimu ujao, basi anahitaji kutafuta kipa mpya wa kuja kuchukua nafasi hiyo. Mabadili golini yanatakiwa ili kuinusuru Arsenal kwenye kufungwa mabao ya kizembe.

Chelsea -

Cesc Fabregas

Kiungo wa Kihispaniola, Cesc Fabregas bado ni mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Chelsea, lakini ameshaanza kuonyesha uchovu unaotokana na umri. Staa huyo mwaka huu atakuwa na umri wa miaka 30 na anaonekana wazi kupata shida ndani ya uwanja. Hata Chelsea tu wanalazimika kumchezesha kwamba hawana kiungo mwingine wa kati mwenye uwezo wa kuchezesha timu. Kwa msimu ujao, Chelsea itapaswa kusajili mchezaji anayefanana na Fabregas kiuchezaji ili kuja kumbadili staa huyo aliyechoka.

Liverpool -

Dejan Lovren

Huko Liverpool nafasi ambayo ilionekana kama kuhitaji mabadiliko kwenye ajili ya msimu ujao ni kipa, lakini Loris Karius ameonekana kubadilika na kuonyesha kiwango bora kabisa kwa sasa katika kikosi hicho cha Jurgen Klopp. Kutokana na hilo, shida inahamia kwenye beki ya kati, eneo ambalo Klopp anahitaji kumtafutia Lovren mchezaji mwingine wa kuja kuchukua nafasi yake msimu ujao. Joel Matip haonekani kucheza vizuri akipangwa na Virgil van Dijk, hivyo analazimika kupangwa na Lovren, ambaye pia amekuwa akifanya makosa mengi sana. Klopp anahitaji kumtafuta mtu wa kuja kuchukua nafasi ya Lovren huko Anfield.

Man City - Fernandinho

Kiungo wa Kibrazili, Fernandinho amekuwa mmoja wa wachezaji mahiri kabisa kwenye Ligi Kuu England msimu huu, lakini umri wake kwa sasa ni miaka 32 na nguvu ni kitu cha kwisha. Ilkay Gundogan anafanya vizuri, lakini kimsingi yeye si kiungo mkabaji, hivyo jambo hilo litaifanya Manchester City kuwa na ulazima wa kusajili mchezaji mwingine wa kuja kuchukua mikoba ya Fernandinho. Ripoti zinadai kwamba Man City tayari imeshakubali kulipa Pauni 50 milioni kumnasa kiungo wa Shakhtar Donetsk, Fred kuja kuchukua mikoba ya Fernandinho huko Etihad kurekebisha mambo.

Man United - Antonio Valencia

Mtumishi halali kabisa huko Manchester United. Lakini, Valencia tayari ameanza kupata shida ndani ya uwanja kutokana na eneo analocheza la beki wa kulia kuhitajika kuwa na kasi ya kutosha kuwadhibiti washambuliaji makorofi wenye kasi ya hatari mchezoni. Nguvu na kasi zimeanza kumuisha Valencia na ndiyo maana siku za karibuni amekuwa hapigi tena krosi na muda mrefu amekuwa nyuma ili kuficha udhaifu wake kwamba miguu imeshaanza kuchoka. Ni kitu cha mzaha, Man United inataka kushinda Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya wakiwa na huduma ya Valencia, wanahitaji kumbadili beki huyo na kuchukua kijana ambaye ataweza kuja kuendana na soka la kisasa linalotumia zaidi kasi.

Tottenham -

Fernando Llorente

Hakuna udhaifu wa waziwazi kwenye kikosi cha Tottenham Hotspur, lakini kunahitajika mtu wa kuja kumsaidia Harry Kane. Vincent Janssen ameshinda na Fernando Llorente amefeli pia kwenye hilo na ndiyo maana kocha Mauricio Pochettino anahitaji kuingia sokoni mwishoni mwa msimu huu kusaka mshambuliaji mwingine atakayekuja kumbadili Llorente kwenye kikosi hicho. Shida nyingine ya Mhispaniola huyo ni kuwa majeruhi mara kwa mara, hivyo anahitaji mchezaji mwingine mwenye uhakika wa kuja kumpa msaada Kane kuisaidia timu wakati inapohitajika kufanya hivyo.