WAMEJISHTUKIA

Thursday July 27 2017

 

By Rhobi Chacha

NDIO wamejikataa baada ya kubaini kuwa kwa sasa wamekua. Na katika ukuajia hufanya baadhi ya mambo uachane nayo, ili kuonyesha kukua kwako.

Kuna wasanii ambao wakati wanaibuka kwenye fani kwa uwezo wao, walijipachika majina yenye kurahisisha utambulisho wao. Kwa namna walivyoibuka wakiwa wadogo wengi wao walitanguliza neno Dogo kabla ya majina yao kisanii. Majina hayo yalibamba kinoma, lakini kwa kuwa binadamu hukua, hata wao nao walijishtukia kuwa wamekuwa na kulazimika kuyakataa majina yao ya utotoni.

Wao sio wa kwanza kufanya hivyo kwani hata duniani, kuna wasanii walijipachika majina kama hayo kuutambulisha udogo wao, kama kina Lil Bow Wow, Lil Romeo, Lil Wayne ambao kwa sasa wameyatema majina ya lil na kubakia na majina yao halisi.

Mwanaspoti inakuletea orodha ya wasanii waliolazimika kubadili majina yao ya udogo baada ya kubaini kuwa hayaendani na ukubwa walionao, wasikie wanachokisema na namna mashabiki wao walivyo na mitazamo tofauti katika suala hilo.

Abdul-Aziz Abubakar Chende ‘Dogo Janja’

Msanii huyo anasema hata akiwa na miaka 50 hawezi kubadilisha jina la Dogo Janja. Japo kuwa kujiita Janjaro pia limezoeleka ila yote ni majina yake kwa hiyo hakuna sababu ya yeye kubadilisha jina.

Dogo Janja anayetamba na nyimbo kama ‘Kidebe’, ‘Ukivaaje Unapendeza’ na nyingine anasema; “ Hili jina nilipewa na mashabiki wangu, naliheshimu sana kwa sababu ndilo lililonifikisha hadi hapa na kupata umaarufu kutokana na kukubalika. Licha ya umri kusonga mbele lakini siwezi kulibadili. Labda mashabiki wangu watake wao lakini mimi sitabadili hadi mwisho wangu,” alisema Janjaro.

Asilahi Isihaka ‘Dogo Aslay’

MSANII wa muziki wa kizazi kipya nchini, Asilahi Isihaka ‘Dogo Aslay’, anasema kutokana na umri wake kusogea, angependa kuitwa Aslay.

Hata hivyo, anasema jina hilo lilianza baada ya kupata umaarufu na wimbo wake wa ‘Nitakusemea’ na mashabiki kuanza kumwita Dogo kutokana na umri wake mdogo na yeye kumalizia kwa kujiita Dogo Aslay.

Msanii huyu anatamba na nyimbo zake kama ‘Mhudumu’, ‘Angekuwepo’ na nyingine

Dogo Hamidu

Kwa upande wake yeye anasema, amelikataa hilo jina baada ya kujiona ameshakua mkubwa na kusema anapenda kwa sasa ajulikane kwa jina la Nyandu Tozi. Jina la Dogo Hamidu alianza kulitumia tangu akiwa anasoma ambapo alikuwa akisimamiwa na Dudu Baya.

Lameck Ditto ‘Dogo Ditto’

Msanii huyu aliibuliwa na rapa mkongwe, Afande Sele mwaka 2003 katika tamasha la kuibua vijana wadogo wenye vipaji lilioandaliwa na kituo cha Redio Ukweli kilichokuwa na makazi yake mkoani Morogoro. Kipindi hicho akiitwa Dogo Ditto.

Alianza kutumia jina la Lameck Ditto baada ya kujiunga na kundi la La Familia lililokuwa likiongozwa na Chid Benz ambalo pia liliundwa na Cassim Mganga, Tunda Man, O Ten, Chiku Ketto na Mc Koba.

Msanii huyu ambaye anatamba na wimbo wa Moyo Mashine na nyingine alizoimba wakati akiwa na kundi la Watu Pori na La Familia.

Mashabiki wanasemaje?

Aidha baadhi ya mashabiki wamekuwa wakipingana na kusema kuwa,wasanii hao wanaotumia jina la Dogo ni vema wakaliacha kutokana na umri wao kuwa mkubwa kwa sasa. Pia wako wanaowaunga mkono wasanii hao kwa kuendelea kutumia jina hilo la Dogo kwani ndilo lililowatambulisha, hivyo kukaa sana midomoni mwa mashabiki tofauti na wale wanaobadilisha majina ambapo inakuwa vigumu kumtambua msanii huyo.

Ashraf Mmbaga wa Tabata Relini anasema, “Dodo kama tu lilivyo linamaanisha mdogo. Wasanii wetu wanakuwa na wale waliokuwa wadogo mi naona wote wamekua hivyo ni vyema wakaachana na majina hayo na kutambulisha mengine. Kama ni kukubalika wameshakubalika na majina yao lazima yatakubalika.”

Mwanaidi Mussa wa Sinza Mugabe yeye yupo tofauti. Anasema: “Wangebaki nayo tu hayo. Kubadili jina kunachanganya watu. Tumeshawazoea kwa majina hayo hayo na ndio yaliyowapa umaarufu. Wengine wanajulikana hadi nje ya nchi, ninadhani kubadili kwao majina kutaweza pia kuwapotezea mashabiki kwa kiasi kikubwa.”

Francis Michael wa Sinza naye anapinga kutumika kwa majina hayo, anasema. “Umri unaenda, ndio maana kuna watoto, vijana watu wazima na wazee. Kuendelea kutumia jina dogo kwa wasanii wetu ni sawa na kukataa kukua. Mi sidhani kama wasanii hao kuna mwenye umri chini ya miaka 18. Wawaachie madogo wengine.”