Sapraizi usajili wa England

Muktasari:

  • Hakukuwa na habari zaidi ya kuishuhudia Chelsea tu ikiweka rekodi ya kumsajili kipa kwa Pauni 72 milioni, ilipomnasa Kepa kutoka Athletic Bilbao. Hata hivyo, Kepa hakuwa sapraizi pekee iliyotokea kwenye kipindi cha usajili huko kwenye Ligi Kuu England kwa majira haya ya kiangazi.

WAKATI dirisha la usajili wa majira ya kiangazi likifungwa juzi Alhamisi, akili ya wengi ilikuwa huko Manchester United, nani angesajiliwa?

Hakukuwa na habari zaidi ya kuishuhudia Chelsea tu ikiweka rekodi ya kumsajili kipa kwa Pauni 72 milioni, ilipomnasa Kepa kutoka Athletic Bilbao. Hata hivyo, Kepa hakuwa sapraizi pekee iliyotokea kwenye kipindi cha usajili huko kwenye Ligi Kuu England kwa majira haya ya kiangazi.

6. Jack Wilshere kuhamia West Ham bure

Staa mwenye kipaji matata kabisa kuwahi kutokea kwenye kikosi cha Arsenal. Jack Wilshere aliibukia kutokea kwenye akademia ya Arsenal na alikuwa mchezaji ambaye kuna wakati Barcelona iliwaza kuwa na huduma yake.

Ni mchezaji ambaye hakuna Mwingereza asiyeamini katika uwezo wake anapokuwa ndani ya uwanja. Lakini ndiyo hiyo, kufumba na kufumbua, Wilshere ameondoka Arsenal kwenda kujiunga na West Ham United na mbaya zaidi, amekwenda bure kabisa.

Majeraha ya mara kwa mara ndiyo yaliyomfanya staa huyo asiongezwe mkataba na Arsenal na kuruhusiwa kwenda West Ham United bure.

Hata hivyo, ni faida kwa wengine, kazi ni kwake sasa Kocha Manuel Pellegrini kuvuna ubora wa kiungo huyo Mwingereza.

5. Joao Moutinho kutua Wolves kwa Pauni 5milioni tu

Vijana wapya kwenye Ligi Kuu England, Wolves wamewaduwaza wengi baada ya kufanya usajili matata wa kumnasa kiungo fundi wa mpira, Mreno, Joao Moutinho, tena wamefanya hivyo kwa pesa kidichu kwelikweli, Pauni 5 milioni tu.

Wolves inaamini kwa kuwa na huduma ya wachezaji wenye uzoefu litaiweka kwenye wakati mzuri wa kukwepa masuala la kushuka daraja.

Moutinho ni mchezaji mkubwa sana na kiwango chake cha ndani ya uwanja hakina shaka kutokana na huduma yake aliyokuwa akitoa huko AS Monaco, hivyo kwa mchezaji wa aina yake, ambaye angepaswa kucheza timu kubwa kwenda kujiunga Wolves, tena kwa Pauni 5 milioni, hilo ni jambo linaloshangaza. Sawa, umri wake ni miaka 31, lakini Moutinho si mchezaji ambaye ungekuja kuwaza angekuja kuichezea Wolves siku moja. Ameichezea Ureno mechi 113.

4. Richarlison kwenda Everton kwa Pauni 50milioni

Brazil ina makinda wengi sana wanaoibukia kwa kasi kwenye soka kwa sasa. Baadhi yao ni kama Gabriel Jesus, Malcom na Richarlison, ambao watakuwa kwenye umri sahihi kabisa wakati fainali za Kombe la Dunia 2022 zitakazofanyika huko Qatar.

Hata hivyo, hakuna aliyetarajia kama Everton italipa Pauni 50 milioni kunasa saini ya winga wa Kibrazili, Richarlison akiwa na umri wa miaka 21 tu.

Kocha wa sasa wa Everton alimsajili Mbrazili huyo wakati huo alipokuwa Watford, hivyo baada ya kutua Goodison Park aliamua kumbeba winga huyo na kwenda naye huko.

Kocha ndiye anayefahamu kitu gani atapata kutoka kwa winga huyo, ambaye alifunga mabao matano katika mechi 41 zilizopita. Uhamisho wake haushangazi, ila kinachoshangaza ni hiyo ada iliyolipwa na Everton kumsajili. Kilichopo ni kusubiri kuona ni uwekezaji mzuri au ni makosa yenye gharama kubwa.

3.Rui Patricio kusaini Wolves bure

Usajili huu hakika utakuwa umeshawashangaza wengi, hata mashabiki wa Wolves wenyewe. Kama ilivyokuwa kwenye dili la Moutinho, wakala matata Jorge Mendes, amekuwa na uhusiano mzuri na wamiliki wa Wolves amewasaidia kuwapa wachezaji makini kabisa.

Rui Patricio ni kipa namba moja wa Timu ya Taifa ya Ureno. Aliachwa na klabu yake ya Sporting Lisbon, hivyo akawa huru kwenda kujiunga na Wolves bure kabisa bila ya senti yoyote. Sporting ilivunja mkataba na kipa huyo, hivyo vita ya panzi, sherehe kwa kunguru, Wolves ikajiopolea kipa matata kabisa ambaye atakwenda kusimama kwenye goli lao la kuipatia huduma makini.

Umri wake wa miaka 30, kipa Patricio bado ana uwezo wa kucheza kwa miaka saba hadi minane ijayo.

2.Yerry Mina kuitosa Man United kwenda Everton

Everton ilipania kufanya usajili mkubwa kwenye dirisha la majira ya kiangazi lililomalizika juzi Alhamisi. Moja ya usajili wake, ambao hakika uliwashangaza wengi ni ule wa kumnasa beki Yerry Mina, ambaye alikuwa akiwindwa pia na Manchester United.

Kwa ushawishi wake tu wa kumfanya Mina kuitosa Man United na kwenda kutua kwao kwa ada ya Pauni 27.2 milioni hilo limewaduwaza wengi.

Wakati Man United ikihaha kusaka beki wa kati, inapigwa za uso na kumshuhudia Mina akienda zake Goodison Park badala ya Old Trafford. Everton imemnasa pia Andre Gomes kwa mkopo na Mbrazili Bernard kwa uhamisho wa bure.

Mina, ambaye alitua Barcelona kwenye dirisha la Januari akitokea Palmeiras kwa ada ya Euro 11.8 milioni, ameshindwa kupata namba mbele ya Samuel Umtiti na Gerrard Pique huko Nou Camp. Amecheza mechi sita tu kwa miezi sita aliyokuwa hapo na sasa ametua Everton.

1.Jean Michael Seri kujiunga na Fulham

Utashangaa kiungo ambaye alikuwa hakauki kwenye ndimi za timu vigogo kama Chelsea, Manchester City, Manchester United, Arsenal na hata Liverpool, hakwenda kwenye timu hizo na kuamua kujiunga na Fulham.

Hakika kwenye usajili uliofanyika ndani ya Ligi Kuu England, kiungo wa Nice, Jean Michael Seri kwenda Fulham ni kitu kilichowashangaza wengi.

Staa huyo amenaswa kwa Pauni 18 milioni tu. Mwaka jana alikuwa kwenye rada za Barcelona, lakini kwa sasa ndani ya msimu huu atakuwapo kwenye Ligi Kuu England, tena ndani ya jezi za Fulham, iliyorudi Ligi Kuu England mwaka huu.

Seri ni aina ya wachezaji ambao kama wataendelea kucheza kwa kiwango kilekile, basi hawezi kubaki Fulham kwa miaka mingi, lakini jambo linaloshangaza ni uamuzi wake wa kuzikacha timu za kucheza soka la Ulaya na kuamua kujiunga na timu ndogo hivyo.