Piga ua lazima wasepe

MSIMU wa Ligi Kuu Bara 2017-2018 unafikia tamati kesho Jumatatu kwa mechi nane za kufungia msimu zitapigwa kwenye viwanja tofauti.

Hakuna jipya katika ligi hiyo, ila ipo vita ndogo ya kuwania nafasi ya pili, huku mkiani timu mbili za Majimaji na Ndanda zinachuana kuepuka kushuka daraja kuungana na Njombe Mji iliyotangulia mapema kama Simba ilivyobeba mapema taji la msimu huu.

Kumalizika kwa ligi hiyo kunatoa nafasi ya kufunguliwa kwa dirisha jipya la usajili kwa lengo la klabu kuimarisha vikosi vyao kwa msimu ujao, huku nyota wengine wakitafuta chaka la malisho mapya baada ya kazi nzito ya msimu huu.

Tayari Donald Ngoma aliyekuwa Yanga ameshajihakikishia maisha mapya Azam baada ya kumalizana na mabosi hao na sas anasubiriwa tu kupelekwa Afrika Kusini kufanyiwa vipimo kabla ya kuliamsha Chamazi.

Mwanaspoti inakuletea orodha ya nyota kumi ambao piga ua lazima wasepe kwenye timu zao za sasa ili kuliamsha dude katika klabu nyingine mpya kwa msimu ujao.

Marcel Kaheza

Straika huyu wa Majimaji licha ya timu yake kushika nafasi ya tatu kutoka mkiani mwa msimamo na kuwa kwenye hatari ya kushuka daraja, lakini Kaheza ameifungia mabao 13 akishika nafasi ya tatu nyuma ya John Bocco na kinara Emmanuel Okwi.

Kaheza amewazidi hata mastraika wengine wa kigeni wa klabu kubwa nchini kwa kasi yake ya kutupia kambani.

Kiwango alichoonesha Kaheza aliweza kuchuguliwa Mchezaji Bora wa Aprili na kuwaacha John Bocco na Emmanuel Okwi wa Simba ambao alingia nao katika tatu bora ya kinyang’anyiro hicho.

Baada ya kuonesha kiwango aliwavutia mabosi wa Simba ambao juzi walimsainisha mkataba wa awali wa miaka mitatu na kwa maana hiyo msimu ujao atakuwa na kikosi cha mabingwa hao.

Mohammed ‘Mo’Rashid

Kama ilivyo kwa Kaheza, straika huyu wa Prisons naye hawezi kubaki kwa maafande hao kwani mipango yake kuelekea Msimbazi imeshatiki mapema.

Dalili za Mo Rashid kutimka kikosini, zilianza tangu katika dirisha dogo alipohusishwa kwenda Yanga kabla ya kuahirisha na kusalia Prisons, lakini mabao yake 10 aliyofunga mpaka sasa yamemfanya awe njiani kutua Msimbazi.

Kabla hata ligi haijamalizika mabosi wa Simba walishakaa naye mezani na kumsanisha mkataba awali wa miaka mitatu na kwa maana hiyo msimu ujao atakuwa na mabingwa hao ambao wataiwakilisha nchi katika michuano ya Kimataifa.

Adam Salamba

Alianza Ligi akiwa na kikosi cha Stand United lakini katika dirisha dogo alisajiliwa na kikosi cha Lipuli ambapo aliweza kuendeleza kasi yake ya kufunga na kuzifunga timu kubwa kama Simba.

Salamba katika Ligi amefunga magoli nane ambaye yamemfanya kuwa mchezaji nyota anayewaniwa na Simba, Yanga na Azam na huenda msimu ujaoa akawa na moja ya timu kati ya hizo tatu.

Salamba alichaguliwa Mchezaji Bora wa Machi, akiwazidi Salum Kimenya wa Prisons na Mwadini Ali wa Azam.

Kelvin Yondani

Beki kisiki wa Yanga ameshamaliza mkataba na timu yake na sasa yupo kama mchezaji huru tayari viongozi wa Simba na Azam wameshaonesha nia ya kutaka kufanya kazi na beki huyo kongwe hapa nchini.

Yondani ameshafanya mazungumzo na Azam ambao muda wowte wanasubili saini yake huku mwenyewe akiwapa siku kadhaa uongozi ya Yanga kama utashindwa kumuongezea mkataba anatimka zake.

Katika kipindi hiki cha usajili Yondani ni miongozi mwa wachezaji nyota ambao wanahusishwa kuziacha timu zao na kusajiliwa na nyingine.

Juma Abdul

Beki wa kulia wa Yanga ameshindwa kupata nafasi ya kucheza kwa sasa kutokana na ubora ambao anauonesha Hassan Kessy, aliyesajiliwa akitokea Simba.

Abdul licha ya kushindwa kucheza Azam wameonesha nia ya kumtaka kutokana msimu huu kucheza bila ya kuwa na beki wa kulia asili na kuwalazimisha Himid Mao na Daniel Amoah kuziba nafasi ya Shomary Kapombe aliyetimkia Simba msimu huu.

Kama Yanga watashindwa kumpa mkataba mpya maana ule wa awali umemalizika atajiunga na Azam na msimu ujao atakuwa huko.

Obrey Chirwa

Straika wa Yanga Obrey Chirwa ndio kinara wa mabao katika timu hiyo akiwa na mabao 12, lakini amekuwa akishindwa kucheza baadhi ya mechi kwa kuwa majeruhi mfululizo.

Mchezaji Bora huyo wa Oktoba mkataba wake unamalizika jambo ambalo viongozi wa Simba wamekuwa wakimuwinda kimya kimya bila ya watani zao kufahamu.

Ingawa Chirwa anahusishwa kuondoka Yanga na kwenda nje ya nchi tayari Simba walishafanya nae mazungumzo lakini hayakufikia muafaka jambo ambalo anaingia katika orodha ya wachezaji ambao wataondoka msimu huu.

Habib Kyombo

Mchezaji Bora wa Desemba amekuwa na mwenendo mzuri katika kiwango chake kwani ameweza kufunga magoli yaliyowadatisha vigogo, Simba, Yanga na Azam na kuanza kumfuatilia.

Straika huyo wa timu ya taifa ya Vijana U20, ni miongozi mwa wachezaji walio mbioni kutimka katika walizozichezea msimu huu, kwani amekuwa wakihushiwa tangu dirisha dogo kwamba asingesalia katika kikosi cha Mbao.

Timu yoyote itakayoamua kukomaa naye ni wazi, Kyombo atasepa katika timu yake na kwenda kuanza maisha mapya sehemu nyingine. Wapi? Tusubiri tuone!

Jamal Mwambeleko

Beki wa kushoto wa Simba ameshindwa kupata nafasi ya kucheza katika kikosi hiko kwani msimu mmoja amecheza mechi moja tu kati ya 29 ambazo timu yake imecheza na kubeba taji la Ligi Kuu Bara mapema.

Mwembeleko alicheza mechi dhidi ya Majimaji lakini tangu hapo amekuwa mchezaji wa kuishia benchi lakini Singida United wamevutiwa na beki huyo na kutuma barua ya kwa uongozi wa Simba kumuomba kwa mkopo.

Kama Mwambeleko itashindikana kwenda Singida basi anaweza kwenda Lipuli na akaachana na Simba msimu ujao na kumalizia mkataba wa mwaka mmoja alionaki nao.

Juma Liuzio

Mshambuliaji mwingine matata wa Simba katika msimu mzima amefunga bao moja katika mechi ya kwanza walipocheza na Ruvu Shooting na kuwafunga mabao 7-0, lakini tangu hapo amekuwa mchezaji wa kuishia jukwaani tu.

Liuzio amemaliza mkataba na Simba na kuna uwezekano mkubwa akaenda kati ya Mtibwa, Kagera, Lipuli au Singida United kwani amekuwa na mawasiliano ya karibu na viongozi wa timu hizo.

Benno Kakolanya

Kipa wa Yanga ameshindwa kucheza katika kikosi cha Yanga kwa kusumbuliwa na tatizo la goti, lakini muda mwingine aliugomea uongozi wa timu hiyo kwa kutaka alipwe stahiki zake Sh 11 Milioni ikiwamo fedha zake za usajili.

Kakolanya ambaye amekuwa akiishia benchi anaweza kuachana na Yanga na kwenda kujiunga na klabu ya JKT Tanzania ambayo imepanda Ligi Kuu msimu huu wakitokea daraja la kwanza kwani mkataba wake ushamalizika na Yanga.