Na ujanja wangu sijagusa Stars -2

Muktasari:

Hata hivyo, ndoto hizo ziliyeyuka kutokana na mzuka wake wa soka na hasa baada ya Yanga kumtia ndimu na kumleta jijini Dar es Salaam.

JUMANNE iliyopita tulianza simulizi la nyota wa zamani wa Coastal Union, Yanga, AICC Arusha, Ndovu FC na timu ya taifa ya vijana, Ayoub Shaaban ‘Nailon’ akielezea namna alivyokuwa na ndoto za kuwa Sheikh.

Hata hivyo, ndoto hizo ziliyeyuka kutokana na mzuka wake wa soka na hasa baada ya Yanga kumtia ndimu na kumleta jijini Dar es Salaam.

Nyota huyo aliyeanza kufahamika miaka ya 1970 anasema hata wazazi wake walikuwa na kiu ya kutaka kumwona akiwa mmoja wa viongozi wa kidini ndiyo maana walimpeleka kusomea udini Chuo cha Kiislam (Tamta).

Anaeleza baada ya Yanga kumwona akiwa na Coastal Union katika mashindano ya Ofuma, ikawa mwanzo wa kutupa kando ndoto yake ya Usheikh na kuanza kutiririka uwanjani.

Anasema hata hivyo katika namna ya ajabu, buku tisa (Sh9,000) za AICC Arusha zilimng;oa Jangwani mwaka 1981. Kiwango hicho kwa miaka hiyo kilikuwa kikubwa na kilimfanya Nailoni kujisikia freshi.

Baada ya kutua AICC na kuichezea kwa miaka minne anasema mambo yalibadilika kwake na kuamua kurejea tena Jangwani? Kipi kilichomrejesha Yanga? Ungana naye katika hitimisho la mahojiano yake na Mwanaspoti.

UBINADAMU WAMREJESHA YANGA

Anasema alidumu AICC na kucheza mashindano mbalimbali kwa takriban miaka minne hivi kabla ya baadaye mambo kubadilika.

Baada ya kumalizana na AICC, aliamua kurudi Yanga kutokana na moyo wake kutaka kulipa fadhila.

“Unajua nilipokuwa Yanga kabla ya kwenda AICC, walikuwa wakinnisomesha bure kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne na nilikuwa napewa posho kama wachezaji wengine wanavyopewa hadi nilipoondoka. Tena nilipoondoka niliaga na waliniruhusu,” anasema.

“Katika maisha ubinadamu una faida yake, kwa vile sikuondoka kwa ugomvi ndiyo maana nikajitoa kulipa fadhila kwa mema waliyonitendea, Yanga walinielewa na wakanipokea japo hiyo mara ya pili kuna viongozi wa awali hawakuwepo tena.”

Anasema aliendelea na maisha ya soka ndani ya Yanga hadi alipoamua kurudi Arusha mwaka 1988 baada ya kuona umri umeanza kumtupa mkono na kushindwa kuhimili soka la ushindani.

AJIUNGA NA NDOVU FC

Baada ya kutua Arusha akaikuta Ndovu ikiwa katika harakati za kupanda Ligi Daraja la Kwanza (Ligi Kuu sasa), ikabidi aongeze nguvu ya kuhakikisha timu hiyo nayo inafanikiwa.

“Huo mwaka kuna wachezaji wa Tanzania walikuwa wametoka Kenya walikokuwa wanachezea timu iliyokuwa inaitwa Volcano, lakini kuna mambo ya kisiasa hayakuwa mazuri, ikabidi warudi Tanzania, mmoja wao alikuwa Jamhuri Kihwelu ‘Julio’,” anasema.

“Walipofika Arusha baadhi yao wakachukuliwa na Ndovu, nawakumbuka kina Lila Shomari, James Kisaka, Mohammed Mateneke na Mwanga Luheya. Mimi pia nikachukuliwa na kuna walioongezwa akiwamo Charles Mgodo (CDA), Hamisi Gaga (Simba), Ally Pande (Mseto), Hamis Mpemba (African Sports) na Mohammed Omary (Kilitex).

Kutokana na kusukwa vilivyo, anasema kikosi hicho cha Ndovu kilifanikiwa kupanda Daraja la Kwanza kwa kishindo, kwani timu ilikuwa bora na waliweza kutamba katika mechi nyingi wakizitoa jasho hata timu kubwa.

ATUNDIKA DALUGA KWA LAZIMA

Anasema mwishoni mwa mwaka 1992, serikali ilikuja na sera ya kubana matumizi na hapo timu nyingi hasa zile za mashirika ya umma zikafa. Kutokana na yeye pia umri kuwa umeanza kumsonga, akaamua kuachana na soka la kimashindano na kutundika daluga zake.

AFURAHIA JINA NAILONI

Huku akitabasamu, anasema: “Unajua kila mchezaji anapaswa kuwa na staili yake ya uchezaji, zamani tulizingatia sana hilo. Ndiyo maana ilikuwa ukimsikia mtu anaitwa ZigZag (John Makelele), Computer (Sunday Manara) ilimaanishwa hivyo kweli. Mimi nilikuwa nateleza kweli siyo mchezo!

“Lakini wachezaji wa sasa viwango vyao haviendani na majina wanayojipachika wenyewe, sisi tulipachikwa majina na mashabiki kulingana na kazi tuliyokuwa tukifanya uwanjani.”

HAWEZI KUMSAHAU BRUCE LEE

Unamkumbuka Bruce Lee? Yule mbabe wa zamani wa sinema za Kung Fu, sasa si kwamba Ayoub Shaaban aliwahi kupigana naye hapana.

Anasema pale Simba wakati huo kulikuwa na beki mmoja mbabe sana, Daud Salum kiasi cha kupewa jina hilo.

“Kuna mechi moja hivi jamaa alitaka kunitoa uhai. Ilikuwa mwaka 1986 ambapo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-1. Aliitwa Bluce Lee kutokana na uchezaji wake wa hatari hatari, yaani yeye hakuona shida kumrukia mtu hata kichwani na washambuliaji wengi tulimkoma,” anasema.

“Unajua wakati ule hata sheria ya soka hazikuwa ngumu sana, ni tofauti na kipindi hiki. Ndiyo maana aliweza kutufanya ubabe sana.”

Mchezaji mwingine ambaye hawezi kumsahau ni aliyekuwa kipa wake pale Yanga, Hamis Kinye, ambaye alisababisha kung’oa meno Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’ wa Simba baada ya kumrukia kwa miguu.

“Kweli nilikuwa Yanga, lakini tukio lile liliniumiza moyo sana. Unajua pamoja na kuwa Mogella alichezewa vile na kushindwa kuendelea na mchezo, lakini refa wala hakumtoa Kinye uwanjani, jambo hilo liliniumiza kuona kipa wetu hakucheza kiungwana.”

SOKA LA SASA LAMKERA

Nailoni anaeleza kuwa, sifa mojawapo ya mchezaji ni kuhakikisha anamudu na kuilinda nafasi yake katika timu, lakini anasema anachokiona sasa ni tofauti.

“Wachezaji wa sasa hawajitumi ipasavyo, ndiyo maana ni wachache sana wanaokuwa na namna za kudumu. Kosa hili pia linatoa mwanya mkubwa kwa wachezaji wa kigeni kumiminika katika klabu zetu za Ligi Kuu Bara,” anasema.

“Kwa mfumo huo, ndiyo maana tunakuwa na Taifa Stars dhaifu. Huwezi kuwa na timu ya taifa imara kama wachezaji wazawa hawana nafasi hata katika klabu za nchini.

“Ndiyo maana makocha wa Stars wanabaki kuteua wachezaji wa Simba, Yanga na Azam.

“Ushindani ulikuwa zamani bwana. Ndiyo maana mimi na ujanja wangu wote niliishia timu ya taifa ya vijana chini ya Kocha Joel Bendera (sasa Mkuu wa Mkoa wa Manyara), sikugusa Taifa Stars sababu ya ushindani.

“Ninaweza kukutajia majina ya wachezaji wa Stars ambao kwa miaka mitano wamekuwa wakiitwa si kwa sababu wana uwezo mkubwa, bali hakuna mwenye kuleta ushindani,” anasema mkongwe huyo huku akionyesha msisitizo kuwa anafuatilia kwa undani soka la Tanzania.