NJE YA BOKSI: Sio kila kitu huwa ni kiki mchezoni

Muktasari:

Kwa kawaida wachezaji huvaa vitambaa vyeusi mikononi, pia kunakuwa na utaratibu wa kutenga wakati wa ukimya kabla ya mapambano kuanza.

WANASEMA kile penye wengi pia huwa pana mengi. Katika mchezo wa soka ambao imezoeleka kujaza maelfu ya mashabiki katika viwanja, imekuwa ni kawaida pia kutumia mjumuiko huo wa watu kufanya kumbukumbu za heshima kama kuomboleza majanga, vifo na kadhalika.

Kwa kawaida wachezaji huvaa vitambaa vyeusi mikononi, pia kunakuwa na utaratibu wa kutenga wakati wa ukimya kabla ya mapambano kuanza.

Mastori ya leo bwana yanaturudisha mpaka Machi, 1993 katika Ligi Ndogo ya Northern Premier League, England.

Mchana wakati timu ya Congleton Town ikijiandaa na pambano lao dhidi ya Rosseland FC zilikuja taarifa za kifo cha mmoja wa mashabiki maarufu wa Congleton, Fred Cope (85).

Kutokana na hali hiyo, Mratibu na Mtangazaji wa Jukwaa Kuu alilazimika kutoa tangazo la kuwepo kwa wakati wa ukimya kabla ya pambano kuanza.

Cha ajabu sasa wakati wachezaji wakijiandaa kuingia uwanjani, dakika chache kabla ya pambano kuanza Fred Cope aliyedhaniwa amefariki alitokea uwanjani hapo na kuwastaajabisha watu wengi. Kila mtu alishangazwa na kuibuka kwake, wakati ilitangaza kuwa ameaga dunia.

Hata hivyo, mwenyewe alipoulizwa kuhusu habari za kifo chake, alidai yeye ni mzima wa afya na taarifa hizo sio za kweli na hajui zilitokea wapi.

Katika kubadili mazingira hayo ya uzembe uliofanyika, mratibu wa pambano hilo ilibidi aombe radhi na kusema wakati huo wa ukimya utakuwa kwa kumbukumbu ya nyota wa soka nchini Uingereza, Bobby Moore aliyefariki wiki moja iliyopita.

Licha ya kuzushiwa yote hayo haikumnyima usingizi Fred Cope kwani alipata furaha ya kushuhudia ushindi wa mabao 6-1 wa timu yake ya Congleton katika pambano hilo.

Sasa piga picha tukio kama hilo lingetoka kwenye soka la Tanzania. Bila shaka watu wangedhani aliyezushiwa kifo amefanya hivyo kusudi ili kutafuta kiki ya kutangaza kifo chake kisha kuibuka tena uwanjani.

Hisia hizo zingeaminika zaidi kama aliyefanyiwa hivyo ni mtu maarufu, wakati ukweli muda mwingine hutokea kwa bahati mbaya.

Katika soka mambo ya kiki huwa hakuna, labda huko kwa watu wa fani nyingine hasa uigizaji na sanaa ya muziki. Labda!

Nimefikisha.