NABIL FEKIR : Lionel Messi wa Kifaransa anaekaribia kutua Emirates

Muktasari:

Ni nani huyu jamaa ambaye Rais wa Lyon, Jean-Michael Aulas, anamfananisha na Lionel Messi wa Barcelona?

LONDON, UFARANSA. SIKU tatu zilizopita, vyombo vya habari vya Ufaransa na England viliripoti kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, anakaribia kumnasa kiungo wa Lyon, Nabil Fekir, anayesakwa pia na Barcelona na Real Madrid. Ni nani huyu jamaa ambaye Rais wa Lyon, Jean-Michael Aulas, anamfananisha na Lionel Messi wa Barcelona?

Ndugu mwingine wa Zidane

Fekir alizaliwa Julai 18, 1993 jijini Lyon, Ufaransa. Wazazi wake ni Waalgeria kama ilivyo kwa staa wa zamani wa Ufaransa, Zinedine Zidane. Alianza kukipiga katika timu ya vijana ya Lyon akiwa na miaka 12.

Baadaye aliachwa ikielezwa hakuwa na nguvu za kutosha. Akajiunga na Vaulx-en-Velin na kutesa nayo, hatimaye Lyon ilikiri kukosea na kumrudisha Fekir mwaka 2011.

Lyon klabu pekee

Baada ya kukipiga timu ya vijana, Fekir alijumuishwa kikosi cha kwanza Lyon kwa mara ya kwanza Julai 30, 2013. Ilikuwa ni katika pambano la kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Grasshopper ya Uswisi wakishinda 1-0. Lakini hakucheza.

Mechi yake ya kwanza ilikuja Agosti 28, 2013 ikiwa ya mtoano kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Sociedad akichukua nafasi ya Yassine Benzia. Klabu yake iliondolewa kwa kuchapwa mabao 4-0.

Siku tatu baadaye alicheza pambano zima la Ligi Kuu Ufaransa dhidi ya Evian walilochapwa 2-1 ugenini. Akafunga bao lake la kwanza Aprili 27, 2014 dhidi ya Bastia huku akipika mabao pia kwa Bakary Kone na Alexandre Lacazette. Msimu wake wa kwanza alicheza mechi 17, akafunga moja.

Msimu wa pili wa 2014–15 alikuwa mchezaji wa kudumu kikosi cha kwanza akifunga mabao 11 na kupika saba kufikia Machi 2015. Hilo lilisababisha aitwe timu ya taifa. Mei 17, 2015 alitajwa Mchezaji Bora Kijana wa Mwaka huku akiwa katika timu ya msimu baada ya kumaliza na mabao 13 na pasi za mabao tisa.

Agosti 29, 2015, Fekir alipiga Hat Trick katika ushindi wa 4-0 dhidi ya Caen ugenini. Hata hivyo alikosa sehemu kubwa ya msimu wa 2015-16 kutokana na matatizo ya goti.

Alipiga Hat Trick nyingine Februari 23, 2017 katika pambano la Europa dhidi ya Az Alkmaar na kupika bao la Mouctar Diakhaby dakika ya 89 wakishinda mabao 7-1. Hayo yalikuwa mabao yake ya kwanza Ulaya.

Kufikia Februari alikuwa amefunga mabao 10 na kupika 10 katika michuano yote. Agosti 2017 alitangazwa nahodha wa Lyon baada ya Maxime Gonalons kuhamia AS Roma. Novemba 5, 2017 alifunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya wapinzani wa jadi AS Saint-Etienne.

Bao lake la pili nusura livunje mechi baada ya kuvua jezi na kuwaonyesha mashaki wa Saint-Etienne walioanzisha vurugu na kurusha vitu mbalimbali uwanjani kiasi cha mwamuzi Clemet Turpin kuwapeleka wachezaji vyumbani kwa dakika 40.

Aitosa Algeria

Fekir aliichezea Ufaransa mechi moja tu katika soka la vijana wakati alipoingia katika pambano la kufuzu Euro chini ya umri wa miaka 21 dhidi ya Sweden akichukua nafasi ya Corentin Tolisso dakika ya 75 mnamo Oktoba 15, 2014.

Baadaye Algeria walimtaja katika kikosi cha maandalizi ya mechi za kirafiki dhidi ya Oman na Qatar Machi 2015. Lakini alijitoa na kwenda kikosi cha Ufaransa kilichomuita kwa mechi dhidi ya Brazil na Denmark.

Aliichezea Ufaransa mechi ya kwanza Machi 26, 2015 dhidi ya Brazil akiingia dakika 16 za mwishoni kuchukua nafasi ya Antoine Griezmann huku wakichapwa mabao 3–1. Aliifungia Ufaransa bao lake la kwanza Juni 7, 2015 katika kichapo cha mabao 4-3 walichopewa na Ubelgiji. Septemba 4, 2015 aliumia goti walipocheza na Ureno na alitazamiwa kukaa nje miezi sita. Hilo lilikuwa pambano lake la kwanza kuanza. Aliitwa tena Agosti 25, 2016 kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Italia na pambano la kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Belarus. Lakini alijitoa siku tatu baadaye, aliumia.

Akaibuka Oktoba 7, 2016, katika pambano la kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Bulgaria waliloshinda 4-1 akichukua nafasi ya Antoine Griezmann. Akacheza mechi nyingine mbili za kufuzu dhidi ya UHolanzi na Luxembourg zote akitokea benchi. Alizikosa Bulgaria na Belarus.