Mbona hapo moto utawaka Arachuga

MITAA ya Arusha kwa sasa gumzo kubwa ni fainali za Kombe la FA maarufu kama Azam Sports Federation Cup. Fainali hiyo itapigwa Juni 2 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini hapa ikizikutanisha Mtibwa Sugar na Singida United.

Pambano hilo limerejesha ule uhondo ambao mashabiki wa soka wa Arusha walianza kusahau tangu timu zao ziliposhuka kutoka Ligi Kuu Bara miaka ya nyuma kama Ndovu, Pallsons, AFC Arusha na Oljoro JKT.

Mpambano huo umekuwa gumzo kwelikweli, lakini pia inaweza kuwa darasa tosha kwa viongozi mbalimbali wa Serikali na vyama vya michezo kuweka mikakati ya kuhakikisha wanapata timu inayoshiriki Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Siku chache zilizopita Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo kupitia ukurasa wake wa Facebook alihitaji maoni kwa wadau juu ya kuanzishwa kwa timu na kuipa jina la Arusha United Sc huku wengi wakieleza hakuna haja ya kufanya hivyo bali kuweka mkazo kwa timu zilizopo.

MAANDALIZI YA FA

Ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda vyema, Chama cha soka Mkoani hapa (ARFA) kilipeleka maombi kwa wamiliki wa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kutotumika kwa wiki mbili uwanja huo hasa eneo la kuchezea kwa ajili ya kusubiri FA pekee.

Katibu mkuu wa ARFA, Zakayo Mjema alisema kuimalika kwa uwanja huo kunaweza kufungua milango mingine ya kukaribisha michezo ya kimataifa kufanyika mkoani Arusha na hata timu kuweka makazi yake msimu ujao wa ligi kuu.

Uongozi wa chama kimepokea barua kutoka Shirikisho la soka Tanzania (TFF) ukihitahiji kujua idadi ya watazamaji wanaoingia Sheikh Amri Abeid.

Mjema alisema kuwa uwanja huo unaingiza watazamaji 11,000 na ndio idadi waliyowasilishwa TFF kwa ajili ya maandalizi ya tiketi za mchezo huo na mambo mengine ya mchezo huo yatakuwa yakiendelea kadri siku zinavyosogea.

Mwaka uliopita Simba SC ilikutana na Madini SC kwenye mchezo wa robo fainali wa mashindano ya FA na kuingiza idadi ya watazamaji 14,056 na kuingiza Sh 81,427,000 milioni.

FAIDA INASUBIRIWA

Arusha itanufaika kwa asilimia kubwa kupitia mchezo huo, sio tu kwa sababu wataushuhudia moja kwa moja kwa wale watakaoingia uwanjani bali hata kwa wajasirimali wa vitu mbalimbali.

Wamiliki wa nyumba za kufikia wageni pamoja na wauza vyakula watapiga pesa ndefu kuelekea kwenye mchezo huo kwani taarifa za chini ya jamvi zinaeleza kuwa watazamaji kutoka mkoani Singida watawasili na wakiwa zaidi ya 200 kuja kuisapoti timu yao.

Ugeni huo wote ni faida kwa wawekezaji wa Mkoani hapa ambao wanatakiwa kuimarlisha na kujipanga katika utoaji wa huduma zao kuliko hata walivyozoea siku za nyuma.

KILA TIMU IMEJIPANGA

Singida United tayari imewasili mkoani hapa ikiwa na kikosi cha wachezaji 15 kikiongozwa na kocha Mkuu wa timu hiyo Mholanzi, Hans Pluijm ambaye alielezea kufurahishwa na mwonekano wa uwanja utakaotumika siku ya fainali.

Kutokana na umuhimu wa mchezo huo Singida imekigawa kikosi chao huku kingine kikielekea Mkoani Mbeya kumaliza mchezo wao siku ya Jumatatu dhidi ya Tanzania Prison kikiwa na wachezaji 18 chini ya kocha msaidizi Jumanne Charles.

Inasemekana Singida wataendelea kupiga kambi mkoani hapa wakijifua na Mashindano ya Sport Pesa yatakayoanza kutimua vumbi mapema mwezi ujao nchini Kenya.

Hata hivyo, Mtibwa nao hawakuwa nyuma kwani tayari Thobias Kifaru amewasili kuweka mambo sawa kabla ya kikosi kizima kutua wiki ijayo baada ya mchezo wao wa Ligi kuu Bara dhidi ya Mbeya City.

MCHEZO WA KISASI

Katika Mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa uwanja wa Namfua pale Singida, wenyeji walilala kwa mabao 3-0 yaliyofungwa na Stamil Mbonde, Kelvin Sabato “Kiduku” pamoja na Salum Kihimbwa wakati mchezo wa kwanza waliokuta Mkoani Morogoro katika uwanja wa Manungu walitoshana nguvu ya bila kufungana.

Mtibwa ni moja ya timu inayotoa wachezaji wengi chipukizi kwenda timu kubwa ikiwemo Simba na Yanga huku mfano mzuri akiwemo Shiza Kichuya ni moja ya zao lililotoka Mtibwa ambaye ameng’ara na Simba Msimu huu.

Singida walitinga hatua ya Fainali baada ya kuitoa Yanga kwa Mikwaju ya penalti 4-2 hatua ya robo fainali huku nusu fainali wakiitoa JKT Tanzania kwa kuifunga bao 2-1. Mtibwa wao waliisambaratisha Azam Fc kwa kuifunga mabao 2-0 katika robo fainali kabla ya kuitoa Stand United katika mchezo wa nusu fainali na sasa watakutana ugenini juni mbili mkoani hapa.

FUNZO KWA ARUSHA

Miaka mitano sasa imepita tangua Arusha ishuhudie Ligi Kuu Bara tangu kushuka kwa JKT Oljoro msimu wa mwaka 2012/2013 na tangu hapo soka limekuwa likiendelea kushuka.

Licha ya baadhi ya wadau kueleza kuwa kinachoiangusha Arusha ni kutopata viongozi waliojikita zaidi kwenye soka ndio maana inashuka kila kukicha kwenye michezo pamoja na migogoro iliyokuwepo huko nyuma ndio chanzo cha soka mkoani hapa kuporomoka.