Mbao ichague moto ama pepo

Muktasari:

Kwanza alianza beki wa kushoto, Jamal Mwambeleko, aliyehamia pale Mtaa wa Msimbazi, Simba SC. Wakafuata Salmin Hoza na kipa Benedict Haule waliokwenda Azam FC. Kisha Pius Buswita akaonekana kutimkia Yanga, lakini katua Simba na mwisho ameondoka kipa mwingine, Emmanuel Mseja, pia kaenda zake Simba.

MBAO FC ipo njia panda. Wachezaji sita wa kikosi chake cha kwanza tayari wamejiunga na timu nyingine za Ligi Kuu Bara kwa ajili ya msimu ujao. Mbao sasa imeharibiwa nyuma na mbele. Inatia huruma.

Kwanza alianza beki wa kushoto, Jamal Mwambeleko, aliyehamia pale Mtaa wa Msimbazi, Simba SC. Wakafuata Salmin Hoza na kipa Benedict Haule waliokwenda Azam FC. Kisha Pius Buswita akaonekana kutimkia Yanga, lakini katua Simba na mwisho ameondoka kipa mwingine, Emmanuel Mseja, pia kaenda zake Simba.

Maisha ya Mbao yanaonekana kuwa magumu zaidi kwani mabeki wao wawili wa kigeni, Asante Kwasi na Yusuf Ndikumana, nao wanatajwa kuwa mbioni kutimkia kati ya Mbeya City au Singida japo haijawa rasmi. Zipo dalili kwamba hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu, kikosi chote cha kwanza kinaweza kuwa hakipo tena.

Maisha ndivyo yalivyo. Siku zote mwenye kisu kikali ndiye anayekula nyama nyingi. Timu zenye nguvu ya pesa ndizo zinagawana mastaa wa Mbao. Pengine wataondoka wengi zaidi ya hawa tunaowatarajia.

Swali kubwa linalokuja ni ipi hatma ya Mbao msimu ujao? Mbao itayumba ama la? Hapa ndipo mjadala mkubwa ulipo. Hata hivyo, nina imani kwamba Mbao itaendelea kuwa Mbao hata kama wachezaji wote wataondoka.

Kwa Mbao, pigo kubwa ni pale kocha, Ettiene Ndayiragije, naye atakapoamua kuondoka. Huyu ndiye mwenye Mbao yake. Haijalishi wachezaji wangapi wanaondoka ama wanabaki, kama Ettiene ataendelea kuwepo, ninaamini Mbao haiwezi kutikisika hata kidogo. Zipo sababu nyingi za kuamini hivyo.

Kwanza, Mbao ilitoka kusikojulikana na ikafanya makubwa, nani alitarajia? Mbao ilinyanyuliwa tu mchana na kuambiwa ikashiriki Ligi Kuu. Haikuwa imejiandaa wala kuwa katika ushindani wa Ligi Kuu, lakini iliweza.

Tukumbuke kwamba katika Ligi Daraja la Kwanza, Mbao ilishika nafasi ya nne. Ilimaliza nyuma na JKT Oljoro, Geita Gold Sport na Polisi Tabora. Iliachwa mbali kabisa, lakini ilipopewa nafasi ya kushiriki Ligi Kuu, ilijipanga na kuweza.

Hakuna aliyewahi kumfahamu Mwambeleko wala Ndikumana kabla ya kutua Mbao. Hakuna aliyemfahamu Hoza wala Buswita. Mbao ilikwenda ilikofahamu na kuwasajili, wakafanya kazi ya maana. Leo hii kwanini tuamini kwamba Mbao itayumba kwa wachezaji hao kuondoka?

Kocha wa Mbao, Ettiene ana jicho la kuona vipaji. Alipandisha vijana wengi kutoka timu yao ya pili na wakafanya kazi kubwa. Nina imani kama atabaki, anaweza kupandisha vijana wengine na wakafanya vizuri. Huyu ndiye aliyeishika timu.

Pili, Mbao ilikuwa inacheza kitimu zaidi. Ilitegemea zaidi mbinu za Ettiene hasa katika Kombe la FA na walifika fainali. Ettiene alikuwa na mbinu sahihi katika kila mchezo. Aliwajenga wachezaji wake kisaikolojia na kuwaaminisha kuwa wanaweza. Huyu ndiye anayeshika pepo ya Mbao sasa. Kama ataondoka, si ajabu Mbao ikashuka daraja mapema zaidi. Hata kama wachezaji wote wangebaki, kama Ettiene anaondoka, timu lazima itayumba. Huo ndiyo ukweli mchungu.

Kuna wakati kocha anafanya kazi kubwa kuliko wachezaji. Mfano Mtibwa Sugar, punde baada ya kuondoka kwa Mecky Maxime, imeshindwa kuzalisha mchezaji mwingine wa maana. Kwa mara ya kwanza, katika dirisha la sasa la usajili, Mtibwa haina mchezaji wa maana wa kumuuza sokoni.

Hivi ndivyo ilivyo kwa Etienne. Alitengeneza timu na siyo wachezaji. Wachezaji wengi kuondoka ni matokeo tu. Katika dirisha dogo mwaka jana, aliyekuwa staa wao, Ludovic Venance, aliondoka na wala hawakuyumba.

Tatu, lengo la Mbao kuwepo Ligi Kuu si kutwaa ubingwa. Mbao ipo Ligi Kuu ili isishuke daraja. Hata kama wenyewe hawatasema, ila huo ndio uhalisia. Kwenye Kombe la FA wanaweza kuwa na nia ya ubingwa, lakini si Ligi Kuu.

Hii ndiyo sababu walifika fainali ya FA, lakini walimaliza katika nafasi ya 12 Ligi Kuu. Hawana mafanikio yoyote katika upande wa Ligi Kuu. Kama unasema Mbao itaanguka, ni kwamba unasema itashuka daraja. Je ni kweli kwamba Mbao haiwezi kusajili wachezaji wa kuibakiza Ligi Kuu? Itashangaza sana. Mbao bado inaweza kupata wachezaji wazuri wa kuiwezesha kufikia malengo yake ya kubaki Ligi Kuu. Kama iliwapata akina Mwambeleko, Hoza na Buswita, kwanini tusiamini kwamba wanaweza kupata wachezaji wengine wa maana zaidi. Hakuna wasiwasi juu ya hilo. Wasiwasi upo tu kama kocha wao Mrundi ataondoka. Tukirejea upande wa pili, Mbao, ina tatizo katika uongozi. Inaonekana viongozi wake wengi si watu wenye uzoefu na soka la Tanzania. Kutokana na uzoefu wao mdogo, wameishia kuona timu yao ikisambaratika.

Kosa walilofanya viongozi hao ni kuwapa wachezaji wote mikataba ya mwaka mmoja mmoja. Kwa timu inayoshiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza, inapaswa kuwapa wachezaji angalau mikataba ya miaka miwili ama mitatu.

Hapo unakuwa umejihakikishia maisha marefu kidogo katika ligi husika.

Mbeya City walivyopanda, wachezaji wao walikuwa na mikataba ya miaka miwili hadi mitatu. Hii iliwasaidia kwani Simba na Yanga hazikuweza kuvuna wachezaji wao kirahisi.

Historia inaonyesha namna Simba na Yanga zilivyo na tabia ya kuchukua wachezaji kutoka kwa timu zinazotikisa.

Mbao hawakujipanga katika hilo na matokeo yake sasa wachezaji wanaondoka bure. Wakati mwingine wajifunze kutoka kwa wazoefu.