Mastaa hawa wataukosa mwanzo wa Ligi England

MUDA si mrefu klabu mbalimbali zitaanza mazoezi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya England. Bado safari ni ndefu kuanza msimu ujao, lakini tayari kuna mastaa wapo kando na usitazamie kuwaona mwanzo wa msimu ujao.

Eden Hazard (Chelsea)

Jina kubwa zaidi ambalo litaanzia nje msimu ujao. Mmoja kati ya wachezaji wenye vipaji zaidi katika soka kwa sasa. Msimu uliopita alikuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha kocha, Antonio Conte akiwapa Chelsea ubingwa wao wa tano katika historia. Bahati mbaya kwa Chelsea, Hazard aliumia mwanzoni mwa mwezi huu wakati akiwa katika majukumu na timu yake ya taifa ya Ubelgiji na anatazamiwa kukaa nje mpaka Septemba. Kwa kuanzia Hazard atalikosa pambano la ngao ya jamii dhidi ya Arsenal, Agosti 6 mwaka huu katika dimba la Wembley na kuna hatari akazikosa mechi nyingine muhimu za mwanzo za Chelsea.

Yannick Bolasie (Everton)

Winga wa kimataifa wa DR Congo aliyekulia England. Bolasie alianza Ligi iliyoisha kwa kasi baada ya kununuliwa kwa dau la pauni 25 milioni akitokea Crystal Palace. Alishaonyesha ushirikiano wa kutosha na nyota mwingine mwenye asili ya Congo, Romelu Lukaku.

Hata hivyo, aliumia goti lake vibaya katika pambano la Ligi Kuu dhidi ya Manchester United, Februari mwaka huu na alifanyiwa operesheni ambayo itamuweka nje hadi mwaka 2018. Hatarajiwi kuanza Ligi na wababe hao wa jiji la Liverpool. Kitu kibaya zaidi kwa kocha, Ronaldo Koeman na mashabiki wa Everton ni kwamba, Everton ndio timu yenye mwanzo mgumu zaidi wa Ligi Kuu ya England msimu ujao.

Callum Wilson (Bournemouth)

Mshambuliaji mahiri wa Bournemouth ambaye amekuwa na bahati mbaya kubwa na majeraha. Septemba 26, 2015, Wilson aliumia vibaya goti lake la kulia na alilazimika kukaa nje kwa miezi sita. Hata hivyo, alikaa nje kwa mwaka mzima. Aliporudi uwanjani aliumia tena goti na safari hii lilikuwa ni goti lake la kushoto. Na sasa staa huyo analazimika kukaa nje mpaka Oktoba mwaka huu na ataikosa Ligi hii walau kwa miezi miwili tangu kuanza kwake.

Santi Cazorla (Arsenal)

Mmoja kati ya mastaa ambao wanaigharimu Arsenal katika nyakati hizi ni kiungo wao mahiri mchezeshaji, Santiago Cazorla maarufu kama Santi Cazorla. Kwa misimu miwili sasa amekuwa akicheza kwa kusuasua katika kikosi cha Arsene Wenger. Amecheza mechi 23 tu katika kipindi cha miezi 24 kilichopita ikiwa ni wastani wa mechi moja tu kila mwezi. Msimu huu ulioisha Cazorla aliumia tena na kukosa kipindi kirefu cha msimu na anatazamia kukaa nje mpaka Novemba mwaka huu.

Ilkay Gundogan (Man City)

Wadadisi wengi wa mambo walikuwa wanajiuliza kwanini kocha wa Manchester City, Pep Guardiola alikuwa ameamua kutoa kiasi cha pauni 20 milioni katika dirisha kubwa lililopita la majira ya joto kwa ajili ya kumnasa kiungo wa Borussia Dortmund, Ilkay Gundogan.

Alikuwa na rekodi mbaya ya majeruhi na kuanzia hapo ameendelea kuwa majeruhi na ameichezea Dortmund mechi 10 tu za Ligi ingawa alionyesha kiwango kizuri. Mei 2017 wakati Ligi ikielekea ukingoni staa huyu wa Ujerumani mwenye asili ya Uturuki, aliumia tena na anatazamiwa kukaa nje mpaka Septemba mwaka huu. Anatazamiwa kuikosa Ligi Kuu ya England kwa mwezi mmoja na zaidi

Son Heung-min (Tottenham)

Msimu ulioisha ulikuwa bora sana kwa mshambuliaji huyu nyota wa Tottenham, ambaye aliziba vema pengo la Harry Kane alipokosekana. Awali, alianza kwa kusuasua White Hart Lane lakini msimu ulioisha alishika kasi na alifunga mabao 21 katika mechi 47. Staa huyu ambaye alinunuliwa kutoka Bayer Leverkusen kwa dau la pauni 22 milioni katika dirisha kubwa la majira ya joto 2015, aliumia vibaya mkono wake katika pambano la kufuzu kombe la dunia kati ya Korea Kusini dhidi ya Qatar wiki iliyopita. Baadaye alifanyiwa operesheni ambayo inatazamiwa kumuweka nje katika sehemu kubwa ya maandalizi ya msimu ujao katika kikosi cha kocha, Mauricio Pochettino na kuna uwezekano mkubwa akakosekana katika mechi za mwanzo.