Kuna Ustaadhi mmoja tu wa mwendokasi

Sunday April 15 2018

 

PALE England msimu huu kuna vitu viwili vyenye maajabu. Kwanza kabisa ni Manchester City ya Pep Guardiola. Ndiyo timu ya maajabu zaidi kwa msimu huu wa mashindano. Imefanya kile ambacho timu nyingine zote zimeshindwa.

City ya Guardiola imekaribia kabisa kutwaa taji la Ligi Kuu England (EPL). Timu hiyo imekaa kileleni mwa EPL kwa tofauti ya pointi zaidi ya 10 kwa miezi minne sasa. Inahitaji kushinda mechi mbili tu kati ya sita zilizosalia (kabla ya mechi ya jana) ili kuwa bingwa. Wanashindwaje kwa mfano!

Kitu kingine cha maajabu kwenye EPL ni Mohammed Salah. Huwa napenda kumwita ‘Ustaadhi wa Mwendokasi’. Ni Ustaadhi kweli kweli. Kwenye maisha yake kwa sasa ni vitu viwili tu anavyovifanya kwa ustadi mkubwa.

Ni kusali pamoja na kufunga. Akiwa nje ya uwanja, Salah ni mtu wa Sala. Akiwa ndani ya uwanja ni mtu wa kupachika mabao tu. Hivyo ndivyo vitu viwili anavyofanya vizuri kwa sasa. Inafurahisha sana.

Ni wachezaji wachache sana duniani wako kama Salah. Ni wachezaji wachache sana ambao wakitoka mazoezini wanapitiliza kwenye nyumba za ibada. Wachezaji wengi wanapitiza kwenye kumbi za starehe.

Kabla ya Salah kulikuwa na Kaka wa Brazil. Huyu alikuwa Mlokole na ibada kwake ilikuwa kitu kikubwa sana. Kaka hakuwa mtu mwenye mambo mengi nje ya uwanja. Muda mwingi alitumia kwenye sala.

Kwenye maisha ya kawaida, Wachezaji wengi wakitoka kwenye mechi wanakwenda kula bata. Wachezaji wengine kama Paul Pogba wanatumia muda mwingi zaidi saluni. Ndiyo wameumbwa hivyo.

Kwa Salah hadithi ni tofauti. Kadri anavyozidi kufunga ndivyo anavyozidi kuhudhuria nyumba za ibada. Hayo ndiyo yamekuwa maisha yake siku zote. Siyo mtu mwenye mambo mengi sana nje ya uwanja.

Hii ndiyo sababu kubwa Salah amebadilika na anazidi kuwa imara kila siku. Presha ya Chelsea ilikuwa kubwa hivyo kuamua kuondoka kwa hiari yake mwenyewe.

Baada ya kuondoka Chelsea kiwango chake kilipanda maradufu. Aina yake ya maisha inaruhusu kiwango chake kuwa juu. Msimu uliopita ndio alikuwa staa wa Roma. Aliifungia timu hiyo mabao 15 katika mechi 31 za Seria A.

Msimu huu amekuwa moto hatari. Amevunja karibu rekodi zote pale Liverpool. Amekuwa mchezaji wa kwanza wa Liverpool kufunga mabao 30 katika mechi chache. Amekuwa mchezaji wa kwanza wa Liverpool kuhusika kwenye mabao mengi zaidi ndani ya msimu mmoja.

Mpaka sasa amehusika katika mabao 50, akifunga 39 na kutoa pasi 11 za mabao. Hiyo ni katika mashindano yote.

Wiki iliyopita alikuwa akipigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la Manchester City pale Etihad. Uwezo wake mahiri wa kutumia makosa ya mabeki wa timu pinzani uliipeleka Liverpool nusu fainali ya UEFA kilaini tu.

Katika vitu vya maana zaidi ambavyo Liverpool imefanya kwa msimu huu ni kuwa na Salah. Liverpool inaweza kukaa meza moja na timu kubwa za Ulaya na kuzunguza jambo wakaelewana.

Wakati Real Madrid ikiwa na Christiano Ronaldo, Barcelona ikiwa na Leonel Messi, Liverpool wao wana Salah. Ni wachezaji ambao wako moto zaidi duniani kwa sasa. Hawakamatiki.

Baada ya Luis Suarez kuondoka, Liverpool kwa sasa ndiyo imepata mbadala wake halisi. Kwingine ilikuwa ikipoteza muda tu.

Philippe Coutinho alijaribu kuvaa viatu hivyo lakini hakuwa kama Salah. Coutinho ni mchezaji wa viwango vya juu. Ni fundi wa mpira kweli kweli. Hata hivyo hana uwezo mkubwa wa kufunga kama Salah. Siyo mtu wa kutisha kama Salah. Coutinho anaufanya mpira kuwa rahisi, siyo hatari.

Salah amefiti vilivyo kwenye mfumo wa kocha Jurgen Klopp. Anaweza kukaba kuanzia juu. Ni mshapu kwenda kushambulia. Ana matumizi mazuri ya nafasi. Amekamilika kila idara.

Kwa sasa Salah amebakisha hatua chache tu kuwa mchezaji bora wa dunia. Kwanza kabisa ni kuibeba Liverpool mbele ya timu yake ya zamani, Roma kwenye nusu fainali ya UEFA. Baada ya hapo njia yake inaweza kuwa nyeupe.

Liverpool ikifika fainali ya UEFA huenda Salah akawa mchezaji bora wa dunia kwa mwaka huu. Haitajalisha kama Liverpool imepoteza fainali hiyo ama la, ila Salah atakuwa na nafasi kubwa zaidi. Liverpool ikichukua UEFA njia yake itakuwa nyeupe zaidi.

Kazi kubwa zaidi kwa Salah ipo kwa Roma. Ni lazima ahakikishe Liverpool inaitoa Roma. Bila kufanikisha hilo, ndoto zake za kutwaa tuzo hiyo zitayeyuka kama barafu iliyokutana na jua la Khartoum pale Sudan.

Salah ndiye mtu pekee anayeweza kumzuia Ronaldo asitwae tuzo hiyo kwa mwaka huu. Kombe la Dunia linaweza kubadili upepo, lakini Salah anaweza kumaliza ubishi hapa hapa kwenye UEFA.

Kwa upande mwingine napata wasiwasi kama Liverpool itaweza kumzuia Salah asiondoke msimu ujao. Liverpool haina tabia ya kuzuia wachezaji wake mahiri wasiondoke hivyo kama Real Madrid itaweka mzigo wa maana mezani, huenda wakamuuza.