Kamati haitakuwa na jipya sana-2

Muktasari:

  • Labda tumalizie kwa eneo hilo ambalo baadhi ya wanachana wanaona kwamba Mkwasa kupitia rekodi yake ya ukocha kwamba angekuwa msaada mkubwa kwa klabu yao hali hiyo imekuwa tofauti kutokana na bosi huyu ambaye ninamuheshimu kwa ubora wake kama kocha lakini linapokuja suala la utendaji sidhani kama ni mtu sahihi kutokana na mambo mengi yalipungua tofauti na watu walivyotarajia.

TOLEO lililopita tuliona jinsi Yanga ilivyoyumba katika eneo la sekretarieti ya klabu hiyo ambayo kimsingi ndiyo iliyotakiwa kusimamia ustawi wa timu ambayo kutokana na upungufu huo mambo yaliharibika na kuiangusha timu hiyo.

Labda tumalizie kwa eneo hilo ambalo baadhi ya wanachana wanaona kwamba Mkwasa kupitia rekodi yake ya ukocha kwamba angekuwa msaada mkubwa kwa klabu yao hali hiyo imekuwa tofauti kutokana na bosi huyu ambaye ninamuheshimu kwa ubora wake kama kocha lakini linapokuja suala la utendaji sidhani kama ni mtu sahihi kutokana na mambo mengi yalipungua tofauti na watu walivyotarajia.

Unaweza kuvuta picha wapo wachezaji wa zamani ambao unaweza kuwaleta katika utendaji kisha wakafanikiwa kama Lawrence Mwalusako ambao wana taaluma ya utawala kitu ambacho nina wasiwasi na Mkwasa kama hilo liko sawa kwake kwakuwa rekodi zinaonyesha hakuna sehemu aliyofanya kazi katika utawala ambayo ingemsaidia kuwa na njia nzuri kujidai eneo la utawala wake.

Huu ni upungufu ambao ndani ya Yanga kuanzia uongozi wa juu unayajua lakini tatizo ni kushindwa kuchukua hatua wakiendelea kugugumia maumivu ya ndani kwa ndani huku klabu ikizidi kuangamia taratibu sioni kama Yanga inaweza kusimama kwa aina ya uongozi uliopo.

Ujio wa kamati ya watu 12

Yanga imeunda kamati ambayo inakuja kusaidia majukumu ya kuendesha timu ambayo ilitangazwa katika mkutano uliopita na Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa Yanga George Mkuchika ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Kuundwa kwa kamati hii kunaweza kukaleta vurugu kubwa ndani ya Yanga na hii inaweza kuanzia kwanza katika usafi wa muundo wa kamati hii.

Ipo shaka kwamba uhalali wa baraza la wadhamini kuunda kamati hiyo hali ya kuwa Yanga bado ina uongozi halali ambao wanachama na mkutano mkuu wanautambua kama ilivyotokea katika mkutano huo.

Manji alitangaza kujiuzulu lakini udhuru wake huo bado hauna baraka kutoka kwa wenye timu kutokana na pande zote kugomea uamuzi huo wakisema bado wanamtambua kuwa ni mwenyekiti wao.

Chini ya Manji kuna makamu wake ambaye kwasasa anakaimu kama mwenyekiti Sanga na chini ya Sanga kuna wajumbe wa Kamati ya Utendaji ukiondoa watatu ambao wamejiuzulu.

Hadi hapo asilimia 100 ni kwamba Yanga bado ina uongozi kamili sasa ujio wa kamati hiyo kunaweza kukaigawa Yanga na hili linatakiwa kuangaliwa kwa jicho la tatu na baraza la Mkuchika ili waweze kuliwahi lisije likaibomoa haraka klabu ya Yanga.

Kwasasa kuna vuguvugu wa mgawanyo wa madaraka kwa kamati iliyoundwa na zile zilizopo katika klabu hiyo kabla ya kuundwa kwa kamati hiyo mpya inayoongozwa na mwenyekiti Abbas Tarimba.

Zipo taarifa kwamba baadhi ya wajumbe wa kamati hizo wanapinga kuteuliwa katika kamati hiyo wakiona hawakutendewa haki kwa kuulizwa awali na wao kuridhia kubeba majukumu hayo jambo ambalo linaweza kuleta kas ndogo ya majukumu waliyotakiwa kuyafanya.

Kwa mujibu wa mamlaka ya juu ya Yanga ni kwamba licha ya kamati hiyo kuundwa bado kamati zilizokuwepo awali zile za usajili na mashindano zipo palepale na majukumu yake yaleyale.

Lakini sekunde chache baada ya kutangazwa kwa kamati hiyo Tarimba alitangaza kwamba wanakuja kufanya usajili mkubwa wakianzia kusajili mchezaji namba moja mpaka 11, hapo panatosha kwamba tayari kutakuwa na mgogoro wa kamati moja kupoka majukumu ya kamati nyingine.

Uongozi wa Yanga umetamka kwamba kamati hii ya Tarimba inakuja kusaidia kutafuta fedha na kushauri juu ya kuitengeneza timu kauli ambayo pia nilimsikia mjumbe wa kamati hiyo, Ridhiwani Kikwete akisema hilo katika moja ya kipindi cha michezo cha asubuhi ndani ya wiki hii.

Zipo taarifa kwamba hotuba fupi ya Tarimba katika mkutano ule haikupokewa kwa shangwe na viongozi wa juu wa klabu wakiona alizungumza vitu ambavyo havikuwa katika muundo halisi wa kamati.

Sakata hili linaweza kuleta vurugu zaidi kutokana na kwamba inaonyesha kuna mambo ambayo hayajaweka bayana juu ya mgawanyo wa madaraka na wakulitatua hili ni Sanga ambaye anapaswa kuziita kamati zote na kuzipa miongozo ya majukumu yao kabla ya mambo hayajaharibika.

Kunapokuwa na mkanganyiko wa namna hiyo kisha ukija kuongeza na upungufu wa sekretarieti ni wazi kwamba mambo yanaweza kuja kuharibika zaidi katika klabu ya Yanga na kuididimiza timu.

Hapa ndipo tunaposema kwamba mkutano uliopita unaweza usiwe umetibu matatizo ya Yanga kama sio kuongeza ukubwa wa tatizo kwa mlango wa nyuma na linaweza kurudisha makundi ndani ya klabu kama yale ya Yanga asili na Yanga kampuni yaliyotokea huko nyuma.

Kamati itapotea njia au kufa

Kwa hali ilivyo sasa endapo juhudi za haraka hazitachukuliwa lengo la kuunda kamati hii linaweza kupotea kama hakutakuwa na mwafaka wa jinsi kamati hizi zitakavyofanya kazi naona dalili ya kamati husika kushindwa mapema hata kabla ya kuanza kazi kutokana na msigano huo lakini pia kamati hii inaweza kufa haraka hata kabla ya kukamilika kwa jukumu walilopewa.